Na Said Mwishehe,Michuzi TV- Nanyumbu

KATIBU wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya CCM, Itikadi na Uenezi Shaka Hamdu Shaka ameiagiza Serikali ya Mkoa wa Mtwara kuacha urasimu kwa kuchelewesha ugawaji wa pembejeo kwa wakulima wa korosho mkoa humo.

Shaka ametoa maagizo hayo leo Juni 2 ,2022 baada ya kuwasili Mkoa wa Mtwara kwa ziara ya kikazi akitokea mkoani Lindi ambapo alipata nafasi ya kusikiliza kero za wananchi na miongoni mwa kero hizo ni baadhi ya vijiji kutopata pembejeo hali inayotia wasiwasi kwamba huenda itachelewesha maandalizi mikorosho kuelekea msimu mpya wa zao hilo.

Pamoja na mambo mengine, Shaka ameitaka Serikali ya Mkoa wa Mtwara kuhakikisha inagawa pembejeo za kilimo mara moja kwani hakuna sababu ya kuzichelewesha wakati Rais Samia alishazitoa na zilishafika mkoa huo. "Tumetoka asubuhi tumezungumza na Mkuu wa Mkoa taarifa ambayo nimepatiwa pembejeo zimefika.

“Hivyo niitake Serikali ya Mkoa wa Mtwara waache urasimu, ndani ya wiki moja pembejeo ziwe zimetoka, tunataka wananchi wanufaike na uwepo wa Rais Samia ambaye ameamua kutoa bure pembejeo za kilimo, lengo kuhakikisha wakulima wananufaika na kilimo chao," alisema Shaka.

Kuhusu miradi ya maji ambayo Shaka ameitembelea na kukagua ujenzi wake, ametumia nafasi hiyo kutoa maagizo kwa Mkuu wa Mkoa wa Mtwara Marko Gagiti kufanya uchunguzi kwa kutumia vyombo vya ulinzi na usalama baada ya kubainika uwepo wa mradi wa maji Nandete ambao unasuasua wakati Wananchi wakikabiliwa na changamoto ya uhaba wa maji.

Akiwa wilayani Nanyumbu katika kijiji cha Maratani Shaka amesema anazo taarifa za kutosha za mradi wa maji Nandete, hivyo ametaka kupata majibu kabla ya kuondoka Mkoa wa Mtwara. "Nimepokea malalamiko mengi sana kuhusu huu mradi wa maji Nandete. Serikali ya Rais Samia na CCM itasimama na wananchi.

"Hatuwezi watu wachache ambao maslahi yao binafsi wanakwamisha miradi ya maji. Huu mradi wa maji Natende nataka majibu yake na Mkuu wa Mkoa tumia vyombo vyako kupata taarifa na bahati nzuri taarifa zote ninazo. Kuna mambo mengi yamefanyika na hawasemi, kuna mambo mengi yamejificha," alisema Shaka akitoa maelekezo baada ya kufika katika mradi huo.

Aliongeza kuwa, changamoto ya maji katika Kata ya Nandete zimekiugusa Chama Cha Mapinduzi, zimemgusa Rais Samia Suluhu Hassan na ndio maana amefika kwa ajili ya kupata majibu.

"Tumekagua mradi wa maji na Ilani ya CCM ibara ya 100 inasema tutasimamia usambazaji wa maji mijini na vijiji, ili uchumi ukue lazima tuboreshe huduma za kijamii na miongoni mwao ni huduma ya maji, maji ndio kila kitu.

"Serikali inachukua hatua kadhaa kuondoa changamoto ya maji na Serikali katika Mkoa wa Mtwara imeleta Sh. Bilioni 13.9 kwa lengo la kuimarisha upatikanaji maji. Tunataka ikifika mwaka 2025 utekelezaji wa Ilani iwe imefikia asilimia 95 na moja ya eneo ambalo tunataka kuona linafanikiwa ni maji," aliema Shaka.

Aidha, alitoa rai kwa watumishi waliopewa jukumu la kusimamia utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo kuifanya kwa uadilifu na kwa uzalendo mkubwa lengo kuhakikisha wananchi wanapata huduma na kuongeza Serikali ya Rais Samia inajitajidi kutoa fedha za maendeleo,hivyo wanaosimamia wahakikishe miradi hiyo inatekelezwa.

"Nitoe kwa watumishi waliopewa dhamana ya kusimamia miradi ya maendeleo ya wananchi waifanye kwa uadilifu, wakiitekeleza vizuri sifa zitakuwa za kwao lakini wakikosea wajue hawatafika mbali .Wengi walioaminiwa ni vijana na wanayo nafasi ya kuwepo kwenye utumishi wa muda mrefu.

"Hivyo wawe wazalendo.Katika Mkoa huu wa Mtwara Rais Samia ameleta fedha za maendeleo zaidi ya Sh.bilioni 114 kutoka Sh.bilioni 59 huko nyuma, ni matarajio fedha hizi zinakwenda kujenga miundombinu ya huduma muhimu za kijamii,"amesema Shaka na kuongeza Rais Samia ataendelea kuwatumikia wananchi wa Mkoa wa Mtwara na Watanzania kwa ujumla.









Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...