JUMLA ya wananchi 3,222 kisiwani Pemba wakiwemo wanawake 1,971 na Wanaume 1,251 wamefikiwa kupitia mikutano mbali mbali inayofanywa na wahamasishaji jamii ambayo inalenga kuhamasisha jamii kuacha dhana potofu na kuunga mkono jitihada za wanawake ili kupata haki ya kushiriki katika demokrasia na kushika nafasi za uongozi.
Mikutano hiyo na wana jamii pia imeibua changamoto mbali mbali ikiwa ni pamoja na wanawake wengi kutokujua kusoma na kuandika katika shehia mbali mbali, ambacho ni kikwazo kikubwa kinachowakwamisha wanawake wengi, pia ukosefu wa huduma muhimu za kijamii ikiwemo maji, umeme na barabara za vijijini, jambo ambalo hupelekea wanawake wengi kukosa uwezo na misingi imara ya kupata haki zao za msingi kutokana na vikwazo hivyo.
Sambamba na hilo vikwazo vingine vilivyobainika vinavyokwamisha juhudi za wanawake kutimiza malengo yao yakuwa viongozi ni uwepo wa rushwa ya ngono na fedha, wanawake kukosa misingi imara ya kiuchumi, ukosefu wa elimu ya uongozi na uraia, kutokujua sheria za uchaguzi, ukosefu wa elimu ya ujasiriamali na upatikanaji wa masoko kwa bidhaa wanazo zalisha.
Changamoto nyingine ambayo iliibuliwa ni ukakasi katika upatikanaji wa vitambulisho vya ukaazi na vyeti vya kuzaliwa kwa wananchi ambao umesababishwa na sababu mbali mbali ikiwemo ukosefu wa vyeti vya kuzaliwa ambapo wahamasishaji jamii waliibaini changamoto hiyo zaidi kwenye Wilaya ya Micheweni iliyobainika kuwa inatokana na uelewa mdogo wa jamii katika kufua tataratibu sahihi za kufuata ili kupata vitambulisho lakini pia na kukosa vyeti vya kuzaliwa.
Kufuatia changamoto ya upatikanaji wa itambulisho vya ukaazi na vyeti vya kuzaliwa kwa wananchi, wahamasishaji jamii kwa kushirikiana na maafisa kutoka ofisi za Wakala wa Usajili wa Matukio ya Kijamii kwenye Wilaya husika walichukua hatua za kuwaelimisha jamii juu ya taratibu za upatikanaji wa vitambulisho pamoja na vyeti vva kuzaliwa hasa kwa wale wanaoandikishwa kwa kuchelewa ambapo jumla ya watu 11 walielekezwa na kufuata taratibu hizo na watu wane (4) wapo katika hatua za mwisho kupata vitambulisho vyao.
MAFANIKIO:
Miongoni mwa mafanikio ambayo yamepatikana kupitia mikutano ya uhamasishaji jamiini pamoja ni ujenzi wa nyumba tatu kwa jamii zenye mahitaji maalum katika Shehia za Kwale, Kangagani na Wesha, Madarasa matatu ya elimu ya watu wazima kwa wanawake katika Shehia ya Mjini Kiuyu yameanzishwa yakiwa na jumla ya wanafunzi 82 ambapo katiyao mwanamme ni mmoja tu na tayari wameanza kujua kusoma na kuandika.
Pia wanawake zaidi ya 40 wameonesha utayari wa kugombania nafasi mbali mbali za uongozi katika ngazi za kijamii na za kisiasa.
WITO:
Tunaiomba Serikali kuongeza jitihada za kuboresha miundombinu ya upatikanaji wa huduma za kijamii ikiwemo maji, umeme na kuongeza madarasa ya kisomo cha elimu ya watu wazima katika maeneo ambayo kuna ukosefu wa huduma hizo ili kuondoa adha kwa wananchi hasa wanawake ambao ndio waathirika wakubwa wa kadhia hizo.
Kwa upande wa changamoto ya upatikanaji wa vitambulisho tunatoa wito kwa Serikali kuongeza kasi ya upatikanaji wa vyeti vya kuzaliwa hasa wale walioandikishwa kwa kuchelewa ili kurahisisha upatikanaji wa vitambulisho kwa wakati kwa sababu hii ni haki yao ya msingi.
Aidha jitihada za ziada zinahitajika kwa Serikali na asasi za kiraia kuongeza wigo wa kuwafikia wanajamii na kuwaelimisha kuhusu hakiz ao za kiraia ikiwemo haki za uongozi na kushiriki katika demokrasia.
Pia jamii inatakiwa kuwa tayari kuwaunga mkono wanawake, sambamba na kubadili mitazamo hasi iliyojengeka ya kumkandamiza mwanamke kwa kutotoa fursa sawa kwa jinsia zote kupata haki zote za msingi katika kila nyanja.
Aidha ipo haja kwa Serikali na mamlaka husika kuongeza kasi ya kufanya maboresho ya sheria zote zenye kasoro ambazo hazizingatii usawa wa kijinsia ikiwemo rushwa ya fedha nay a ngono ili kuweka mfumo unaotoa fursa sawa kwa makundi yote katika jamii kupata haki zao za msingi zikiwemo za uongozi.
Pia kuweka utaratibu maalum kwa Tume ya Uchaguzi na Taasisi za Serikal ikuripoti masuala ya rushwa ya ngono.
Mradi wa kushajihisha ushiriki wa wanawake katika uongozi na demokrasia ni mradi wa miaka minne (2020 – 2023), wenye lengo la kukuza ushiriki wa wanawake katika uongozi ambao unatekelezwa na Jumuiya ya Wanasheria Wanawake Zanzibar (ZAFELA), taasisiya Pemba Gender Advocacy and Environmental Organization (PEGAO) na Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania, Zanzibar (TAMWA ZNZ), kwa kushirikiana na Ubalozi wa Norway chini Tanzania.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...