Mkuu wa Programu na Ushirikiano wa Wadau (KTO,) Mia Mjengwa Bergdahl akitoa mada kuhusu programu ya 'Mpira Fursa' wakati wa mkutano huo.


* Yakutana na TAMISEMI, TFF, Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia na kujadili namna ya kuinua vipaji vya mpira kwa shule za msingi 86 nchini


TAASISI ya Karibu Tanzania Organization (KTO,) imepongezwa kwa juhudi zao za kuwakomboa wanawake vijana waliokatisha masomo yao kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo ujauzito na hali duni ya maisha kupitia vyuo vya maendeleo ya Wananchi 54 na kubwa zaidi ni kuwaendeleza wanawake wenye kipaji cha mpira wa miguu kupitia programu ya 'Mpira Fursa' inayotekelezwa katika vyuo vyote nchini.


Hayo yameeleezwa leo jijini Dar es Salaam na Makamu Mwenyekiti wa Shirikisho la Mpira Tanzania (TFF,) Steven Mnguto wakati wa mkutano maalumu ulioikutanisha taasisi hiyo, wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia na TAMISEMI na kujadili mpango wa taasisi hiyo wa kuendeleza vipaji vya mpira kwa wanafunzi wakike kwa shule za Msingi 86 nchini.


Mnguto amesema, soka la wanawake nchini linakuwa kwa kasi na linasonga mbele kutokana na ari wanayoonesha vijana hao na kinachotakiwa ni ushirikiano katika kuhakikisha ndoto za vijana hao ya kushiriki na kushinda kombe la dunia zinafanikiwa.


''Jitihada zinazofanywa na KTO zinatakiwa ziungwe mkono kwa asilimia kubwa, wamekuwa mfano wa kuweka nguvu katika soka la wanawake kuanzia ngazi ya chini kabisa...TFF inaunga mkono hili na tutaendeleaa kutoa mafunzo pamoja elimu kwa Umma katika kutambua soka la wanawake wanajamii watambue kuwa sio uhuni kwa sasa ni ajira yenye maslahi mapana nchini na nje ya nchi.'' Amesema.


Kwa upande wake Mkurugenzi msaidizi anayeshughulikia vyuo vya Maendeleo ya Wananchi (FDC's,) kutoka Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Margaret Mussai amesema KTO licha ya kuwasaidia wanawake vijana waliokatisha masomo yao kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo ujauzito bado imeendelea kuwajengea wanawake hao ujasiri, kujiamini na fursa ya ajira kupitia programu ya Mpira Fursa inayotolewa katika vyuo vya Maendeleo ya Wananchi 54 vilivyopo kote nchini.


Amesema kupitia mkutano huo uliowakutanisha na TFF pamoja na TAMISEMI taasisi hiyo imeeleza azma yake ya kuibua wachezaji wanawake katika soka la mpira ili kujenga timu imara ya wanawake.


''Katika kufanikisha hili vyuo vya Maendeleo ya Wananchi wanatoa somo la kujitambua kwa mabinti ili waweze kuelewa kuwa mpira sio kupoteza muda na sio kwa ajili ya wanaume pekee bali ni ajira yenye kuongeza pato kwa wachezaji na taifa kwa ujumla.'' Amesema.


Aidha ameipongeza timu ya Taifa ya wanawake kwa jitihada wanazoonesha katika soka na kueleza kwa Serikali inatambua mchango wao katika kuendeleza soka la wanawake nchini.


Kwa upande wake Mratibu wa Michezo kutoka Ofisi ya Rais TAMISEMI George Mbijima amesema, KTO inafanya kazi nzuri katika kuendeleza soka la wanawake nchini kuanzia ngazi ya chini kabisa na ujio wa kuendeleza soka la wanawake kuanzia shule za Msingi ni hatua kubwa na Serikali itaendelea kushirikiana nao katika kuendeleza soka la wanawake nchini.


Awali Mkuu wa Programu na Ushirikiano wa Wadau (KTO,) Mia Mjengwa Bergdahl amesema, katika vyuo 54 wanavyofanya navyo kazi wamekuwa wakitoa mafunzo kwa walimu ambao wamekuwa wakiwafundisha washiriki ambao ni wanawake katika vyuo vya Maendeleo ya Wananchi.


''Vyuo hivi vimezungukwa na shule za Msingi tukaona ni vyema kuanza kuendeleza vipaji hivyo kuanzia ngazi ya chini kabisa...Ni dhahiri kwamba ili kupiga hatua katika soka la wanawake au wanaume lazima wengi wacheze kuanzia ngazi ya chini kabisa wakiwa wadogo, tutaendelea kuendeleza vipaji na kutoa vifaa na tumechagua Chuo kimoja ambacho kitakuwa Academy kubwa ya kuendeleza soka la wanawake.'' Ameeleza Mia.












Mkutano ukiendelea.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...