Adeladius Makwega-WUSM
Serikali imesema kuwa itashirikiana kwa karibu na Chama cha Mchezo wa Gofu cha wanawake nchini (TLGU) kufaniksiha mashindano ya mchezo huo ya Afrika yanafanyika kama yalivyopangwa, huku mataifa 35 yanayotarajiwa kushiriki kati ya Septemba 3- 16, 2022 katika Viwanja vya Gymkhana Jijini Dar es Salaam.
Kauli hiyo imetolewa Juni 7, 2022 na Ndugu Said Yakub, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo nchini wakati alipokuwa akizungumza na Mwenyekiti TLGU Sophia Viggo, alipotembelea wizarani hapo, kukamilisha maandalizi ya mashindano hayo ya Afrika, Tanzania ikiwa ni mwenyeji.
“Andaeni mambo matatu, kamati ya maandalizi, barua ya kuomba kwetu juu ya kumuomba Rais wetu Samia Suluhu Hassan kuwa Mgeni Rasmi na mwisho leteni barua ya kuomba wafadhili na wadau kupitia kwetu.”
Naibu Katibu Mkuu Yakub alisema kuwa anatumia fursa hiyo kuuambia umma wa wapenzi wa Gofu na Watanzania wote juu ya kufanyika mashindano hayo na kumuhakikishia Mwenyekiti Viggo kuwa Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo Mohammed Mchengerwa analifahamu hilo na kwa hakika mambo yatakuwa mazuri, mashindano yatafanyika kwa kuwa Serikali inahimiza michezo.
Akifafanua juu ya changamoto za mchezo huo, Mwenyekiti Viggo alisema kuwa Chama chao hakina viwanja na mara zote wamekuwa wakiomba hisani ya viwanja kutoka kwa vilabu kadhaa nchini, huku Tanzania ikishiriki fainali za mashindano ya Afrika tangu mwaka 1992 bila ya kukosa.
“Mchezaji bora nambari moja wa Gofu wa Afrika, kwa mtu mmoja mmoja anatokea Arusha Tanzania. Tuna mashindano ya mtu mmoja mmoja na ya kundi.”
Mazungumzo hayo baina ya serikali na TLGU yalikuwa na nia ya kupata njia ya uhakika kufikia kufanyika mashindano hayo septemba, 2022.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...