MWANASHERIA  Mkuu wa Serikali  Mhe. Jaji Dk. Eliezer Feleshi ( AG) ameutaka uongozi mpya wa Chama cha Mawakili wa Kujitegemea Tanzania Bara ( TLS)  kuwa na  mifumo  ya kiutendaji ambayo pamoja na  mambo mengine itasaidia na kurahisisha ushirikiano   kati ya Chama hicho na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali.

Ametoa  rai hiyo  mwishoni mwa wiki  jijini  Dodoma, wakati Ujumbe wa Baraza la Uongozi la TLS ukiongozwa na Rais wa Chama hicho Profesa   Edward Hosea ulipomtembelea  Mwanasheria Mkuu wa Serikali  kwa lengo la  kujitambulisha na kubadilishana naye mawazo  kufuatia uchaguzi  wa chama hicho uliokamilika hivi karibuni.

Katika mazungumzo hayo, uongozi  wa TLS uliwasilisha hoja mbalimbali ambazo wamemwomba  Mhe. AG kuwasaidia kuzifutailia.

Baadhi ya  hoja hizo ni  pamoja na  ombi la kurejeshwa sehemu ya malipo ya wanachama wao zinazolipwa Mahakamani ombi ambalo wamesema kwa msaada wa AG Feleshi linaendelea  vizuri.

“Niwapongeze kwa  kuchaguliwa kwenu,  wanachama wenu wamewaamini,  TLS ni  mdau muhimu katika  tasnia ya  sheria na hususani  katika  utawala wa sheria. Hivyo niwaombe muwe na  mifumo mizuri ya kuitendaji ambayo pamoja na  mambo mengine itawezesha kubaini  mawakili  wabobezi katika  maeneo mbalimbali ambao  Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali itapenda kuwatumia pale itakapohitaji kufanya hivyo” amesisitiza  AG Feleshi.

Kuhusu  hoja   ambazo TLS wameomba Mwanasheria Mkuu wa Serikali kusaidia kuzifutalia. AG Feleshi   ameahidi  kuendelea kuwasaidia kufuatilia  kwa  baadhi ya hoja ambazo zimo ndani ya mamlaka yake, ikiwamo ya kiwanja ahadi ambayo aliitoa   mbele ya Rais  wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia  Suluhu  Hassan.

Aidha kwa  hoja ambazo  zipo nje ya  mamlaka yake zikiwamo  za  mabadiliko ya kisheria ili pamoja na  mambo mengine, kuongeza muda wa kufanya uchaguzi wa viongozi wa TLS, ameutaka uongozi huo kufuatilia katika     Taasisi husika  ikiwamo  Wizara ya Katiba na Sheria.

AG Feleshi   ameahidi utayari wa Ofisi yake wa kushirikiana na  TLS katika  kutekeleza majukumu ya kisheria kwa maslahi mapana ya umma wa watanzania na akawataka TLS kuwa mabalozi na jicho katika utekelezaji wa majukumu hayo.

 Kwa upande wao  Uongozi  TLS pamoja na mambo mengine umetumia  nafasi hiyo kumpongeza kwa  mara nyingine Mhe.  Mwanasheria Mkuu wa Serikali kwa  kuteuliwa kwake kuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali. Na  kumshukuru kwa  namna ambavyo  amekuwa tayari  kushirikiana na TLS ikiwa ni pamoja na kusukuma hoja zao mbalimbali.

 

 

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...