Na Karama Kenyunko Michuzi TV
WAFANYABIASHARA watatu wanaoishi jijini Dar es Salaam, wamefikishwa katika mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu wakikabiliwa na mashtaka 13 yakiwemo ya kukwepa Kodi na kuisababishia Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) hasara ya zaidi ya Sh. Bilioni 10.5
Katika hati ya mashtaka iliyosomwa Mahakamani hapo na wakili wa Serikali Mwandamizi kutoka TRA Medalakini Emmanuel, imewataja washtakiwa hao kuwa ni, Joseph Msaki, (35), Gifti Msaki (40) na Constantino Romani (38).
Mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi Ramadhani Rugemalira amedai washtakiwa wametenda makosa hayo kati ya Januari 2018 na Juni 15,2022 jijini Dar es Salaam.
Katika kesi hiyo washtakiwa wanakabiliwa na mashtaka manne ya kukwepa kodi, mashtaka manne ya kutoa risiti zisizo halali za mashine ya EFD, mashtaka manne ya matumizi yasiyo sahihi ya mashine ya EFD na pamoja na shtaka moja la kuisababishia TRA hasara.
Katika shtaka kukwepa Kodi washtakiwa hao wanadaiwa kati ya Januari, 2018 hadi Juni 15, 2022 jijini Dar es Salaam washtakiwa kwa pamoja wakiwa na nia ovu walijihusisha na kutoa risiti isiyo halali kwa kutumia mashine ya EFD iliyosajiliwa kwa jina la Romani Shirima ambayo kwenye taarifa ilikuwa na mauzo ya Sh 18,668,611,770 na kusababisha ukwepaji Kodi wa ongezeko la thamani ya sh bilioni 5,580,002,499/=
Pia washtakiwa hao wanadaiwa kutumia mashine ya EFD iliyosajiliwa Kwa jina la Ahmada Ally na kusababisha ukwepaji Kodi wa Sh 784,734,295 Huku mashine hiyo hiyo ikitumika tena kusababisha ukwepaji wa Kodi ya Sh 582,551,181/=
Katika shtaka la kutoa risiti isiyo sahihi inadaiwa katika kipindi hicho washtakiwa walitoa risiti isiyo sahihi Kwa kutumia mashine ya EFD iliyosajiliwa Kwa jina la Ahmada Ally wakati mashine hiyo ilikuwa na taarifa ya mauzo ya Sh 2,622,040,982 na kusababisha ukwepaji Kodi wa Sh 784,734,295.
Katika shtaka la matumizi yasiyo sahihi ya mashine ya EFD inadaiwa, kwa pamoja washtakiwa walitumia mashine hiyo isiyo sahihi yenye jina la Ngarasoni Shirima ambayo ilikuwa na mauzo ya Sh.18,668,611,770 kwa nia ya kumdanganya Kamishna Mkuu wa TRA na kusababisha ukwepaji Kodi ya ongezeko la thamani ya Sh 5,580,002,499
Katika shtaka la kuisababishia Mamlaka hasara inadaiwa, katika kipindi cha January 2018 na June 15, 2022 washtakiwa hao Kwa pamoja huku wakiwa na nia ovu ya kukwepa kodi waliisababishia TRA hasara ya Sh 10,507,755,190 .
Hata hivyo washtakiwa hawakuruhusiwa kujibu kitu chochote mahakamani hapo kwa kuwa mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu haina mamlaka ya kusikiliza kesi za uhujumu uchumi.
Kesi hiyo imeahirishwa hadi Julai 8, 2022 itakapokuja kwa ajili ya kutajwa. Kwa mujibu wa upande wa mashtaka upelelezi katika kesi hiyo bado haujakamilika
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...