Na Karama Kenyunko, Michuzi TV
MAHAKAMA Kuu Masijala Kuu, Dar es Salaam imewataka Halima Mdee na Wenzake saba kufika mahakamani hapo Agosti 26 Agosti 2022 ,kwa ajili ya kuhojiwa na Mawakili wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kuhusiana na viapo vyao.
Hatua hiyo imekuja baada ya wakili wa Chadema, Peter Kibatala leo Julai 29, 2022kuwasilisha maombi mahakamani hapo Kuu kuwapatia wito wa kuwaita mahakamani hapo wabunge hao wa viti maalumu pindi kesi yao itakapoanza kusikilizwa ili waweze kuwahoji.
Mapema kesi hiyo inayosikilizwa na Jaji Cyprian Mkeha iliitwa kwa ajili ya kutajwa na kutolewa Maelekezo maalumu
Akiwasilisha maombi Hayo Kibatala amedai siku ya usikilizwaji wanakusudia Kuwaita Halima Mdee, Nusrat Hanje, Grace Tendega, Ester Matiko, Ester Bulaya, Cecilia , na Mwaifunga ma Jesca Kishoa kwa ajili ya kuwahoji juu ya viapo vyao walivyowasilisha mahakamani hapo
Hata hivyo, mawakili wanaowakilisha kina Mdee wakiongozwa na Aliko Mwamanenge amedai baada ya mawakili wa wajibu maombi kuwasilisha kiapo kinzani na wakiona ipo haja ya kuwaita baadhi ya viongozi wa Chadema mahakamani hapo kwa ajili ya kuwahoji basi watafanya hivyo.
Baada ya maelezo hayo, Jaji Mkeha ameridhia ombi la Chadema la kuwaita wabunge hao ili waweze kufika mahakamani kuhojiwa siku ya usikilizwaji wa kesi.
Aidha amewataka wajibu maombi ambao ni Chadema na, NEC na Mwanasheria Mkuu wa Serikali kuwasilisha kiapo kinzani mahakamani hapo Agosti 5 mwaka huu na iwapo wapeleke maombi watakuwa na majibu basi wajibu Agosti 10,2022. Kesi itaanza kusikilizwa Agosti 26,2022
Halima Mdee na wenzake 18 wamefungua kesi mahakamani hapo wakipinga kuvuliwa uanachama wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema).
Mdee na wenzake walifungua shauri hilo namba 36/2022 Julai 22, 2022 wakiomba Mahakama hiyo ipitie mchakato na uamuzi wa kuwafukuza uanachama na kisha itoe amri tatu.
Katika shauri hilo, wabunge hao wanaiomba mahakama itengue mchakato na uamuzi wa kuwavua uanachama na pia iwalazimishe Chadema kuwapa haki ya kuwasikiliza.
Pia, wanaomba amri ya zuio dhidi ya Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania naTume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) kutokuchukua hatua yoyote hadu malalamiko yao yatakapotolewa uamuzi.
Pamoja na mambo mengine, wabunge hao wanadai kuwa mchakato na uamuzi wa kuwafukuza uanachama haukuzingatia matakwa ya kisheria na misingi ya haki, wakidai kuwa hawakupewa haki ya kusikilizwa.
Uamuzi wa Baraza Kuu uliwafanya Mdee na wenzeke kukata rufaa iliyosikilizwa tarehe 12 Mei 2022 na Kamati Kuu ya Chama hicho na kupelekea kufukuzwa uanachama wao.
Mdee na wenzake wanawashtaki Bodi ya Wadhamini ya Chadema hicho kwa niaba ya Chama hicho, Mwanasheria Mkuu wa Serikali na Tume ya Taifa ya Uchaguzi ya Taifa (NEC).



Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...