Wananchi wa kijiji cha Ngoji kata ya Madimba Halmashauri ya wilaya ya Mtwara mkoani hapa wameiomba serikali ya awamu ya Sita ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inayoongozwa na Rais Samia suluhu Hassan kumaliza ujenzi wa zahanati yao ili kuondokana na adha ya kutembea umbali wa zaidi ya Km 5 kufuata huduma hiyo makao makuu ya kata Madimba.
Akizungumza na Michuzi blog Julai 3 2022 kijijini hapo Bi Zainabu Hamisi amesema, Juni 2021 binti yake aitwae Fatuma Jafari alijifungulia njiani wakati wanampeleka Zahanati ya Madimba na kuongeza kuwa endapo Zahanati yao ingekuwa imekamilika pengine hali hiyo isingetokea.
"Tulitoka Nyumbani akiwa na uchungu lakini kutokana na umbali uliopo alijifungulia Njiani wakati tunaelekea Zahati ya Madimba kwa ajili ya kupata Msaada kwa wataalamu wa afya laiti Kama hii zahanati ingekuwa imekamilika changamoto hii isingetokea" amesema.
Nae Abdallah Mkamba mkazi wa kitongoji cha Yuvi kijijini hapo amesema Wananchi wanajitolea vyakutosha ikiwa ni pamoja na kutoa mchango wa Sh. 5000 kwa kila kaya ili kuongeza nguvu katika ujenzi wa Zahanati hiyo hivyo wanaiomba serikali Yao sikivu wawasaidie pale palipobaki Ili waweze kupata huduma karibu.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa kijiji hicho ndugu Issa Nampalangula amekili kuwepo kwa wanawake waliowahi kujifungulia njiani na amewaondoa hofu Wananchi wa kijiji hicho kwa kusema kuwa ujenzi huo umefikia hatua nzuri kwa kuwa kinachosubiriwa sasa ni kukamilika kwa nyumba ya mtumishi ambapo tayari Shirika la maendeleo ya petroli Tanzania TPDC kwa kushirikiana na Halmashauri ya wilaya ya Mtwara kwa pamoja wameingiza Fedha ili kukamilisha ujenzi huo.Muonekano wa ujenzi wa zahanati ya Kijiji Cha Ngoji kata ya Madimba halmashauri ya Wilaya ya Mtwara.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...