Benki ya Mwanga Hakika yafanya mkutano mkuu wa pili na wanahisa wa benki hiyo yaani AGM (Annual General Meeting) wilayani Mwanga, mkoani Kilimanjaro, kwenye ukumbi wa Baobab Retreat Hall, siku ya Jumamosi 27 Agosti 2022.

Mkutano huu una lengo la kutimiza sharia ya nchi, itakayo kila kampuni kufanya mkutano mkuu na wanahisa wao kila mwaka. Mbali na hayo,mkutano huo ulikuwa na lengo la kuimarisha uhusiano uliopo baina ya wanahisa hao na benki hiyo, ili kuwataarifu wanahisa hao kuhusu benki hiyo ilipotoka, ilipo na pia inapokwenda ili kuweza kupata taarifa kamili na Ili wanahisa hao waweze kutathmini maendeleo ya benki hiyo na kubaini changamoto ili ziweze kutatuliwa. Na waweze kutoa ushauri juu ya maswala ya kimaendeleo yatakayo ikuza benki hiyo na kuwa imara zaidi.

Mkutano huu ni mkutano wa pili na wanahisa wa benki ya Mwanga Hakika, ambapo mkutano wa kwanza ulifanyika mwaka jana (2021) na kuhudhuriwa na wanahisa mbalimbali, kwa lengo la kuimarisha uhusiano wao na wanahisa wa benki hiyo. Pia mikutano hii ina chachu ya kukutanisha wanahisa kwa pamoja na kudumisha umoja na mshikamano wao.

Mbali na hayo, benki ya Mwanga Hakika imefanya mkutano huo wilayani Mwanga, mkoani Kilimanjaro kwasababu benki hiyo chimbuko lake ni Mwanga ambapo ilianzishwa mnamo mwaka 2000, ikiwa inaitwa Mwanga Community Bank (Benki ya Wananchi Mwanga) na baadhi ya wanahisa waliohudhuria mkutano huo ni waasisi, kwani walikuwepo tangia benki hiyo ilipokuwa change. Na kama wasemavyo Waswahili “Mcheza Kwao Hutuzwa”. Benki ya Mwanga Hakika inatambua hilo na kuenzi msemo huo.

Mkutano huo uliohudhuriwa na Wanahisa zaidi ya 300, wakiwemo waasisi na viongozi mbalimbali wa benki hiyo nao ni, Eng.Ridhiwani Mringo ambaye ni Mwenyekiti wa bodi ya Wakurugenzi wa benki ya Mwanga Hakika, pia Mhe.Cleopa Msuya(Aliyekuwa Makamu wa Rais, Waziri Mkuu Mstaafu, Mwanahisa wa benki ya Mwanga Hakika, na mshauri wa benki hiyo), Eng. John K Msemo (Mkurugenzi) CPA (T) Zukra Ally (Mjumbe wa bodi) Bw. Christopher Mageka (Mkaguzi wan je wa mahesabu), Mwakilishi kutoka Benki Kuu ya Tanzania (BOT) Bw. Leodgara A. Haule na wengine wengi.

Kabla ya mkutano huo kulikuwa na semina na wanahisa, ambapo waliweza kutoa maoni, pongezi na kutaka ufafanuzi juu ya maendeleo ya benki hiyo miaka ijayo. Pia Mjumbe wa bodi CPA (T) Zukra Ally, alitoa elimu ya uwekezaji kwa njia ya hisa, na alieleza kuhusu gawio la wanahisa, ununuaji na uuzaji wa hisa, na kueleza baadhi ya sheria zinazoongoza benki hiyo. Na kusema kuwa “Sheria ya mapato (2004) inayodhibiti masuala ya teknolojia na tehama sababu mabenki yanakuwa na mtandao mkubwa ila kupitia sharia hizi kunakuwa na siri baina ya mabenki na watu wao”.

Na aliongeza kuwa, “Katika ulimwengu wa leo, kampuni zenye hisa ndio chombo madhubuti ya kuwekeza biashara,mradi tu kuwepo na uimara wa bodi,menejiment ya wwenye taaluma ya biashara husika kama ifanyavyo benki ya Mwanga Hakika, hivyo msisite kuweka hisa zenu’’.

Ambapo mmoja kati ya wanahisa hao, Bwana. Josephat Shirima alisema kuwa “Nipende kupongeza uongozi wote wa benki ya Mwanga Hakika kwa tukio hili linaonyesha kuwa mnatambua mchango wetu, ningeomba pia kama kuna uwezekano tawi mojawapo liwe ni kwa jina la Mhe. Cleopa Msuya, ili kuonyesha kwamba tunatambua mchango wake kwenye benki hii,kwani amepigana vema tangu benki hii ilipokuwa benki ya Wananchi hadi hivi leo”.

Kwenye mkutano huo, Mwenyekiti wa bodi ya Wakurugenzi wa benki ya Mwanga Hakika, Eng. Ridhiwani Mringo, alieleza mapato na matumizi kwa mwaka ulioishia 31 Disemba 2021, utekelezaji wa mpango wa biashara kwa mwaka mmoja uliopita, na kuteua wajumbe wa bodi kwa mwaka 2021/2022.

Mbali na hayo,kwenye mkutano huo yalijadiliwa mapendekezo kutoka kwa wanahisa, na mwanahisa mmoja aliipongeza benki na alipendekeza benki kuongeza mawakala wa kutosha, pia kuongeza matangazo, ili benki ijulikane vizuri.

Pia, Mhe.Cleopa Msuya, Waziri Mkuu mstaafu, alitoa historia fupi ya jinsi walivyoanzisha Mwanga Community Bank (Benki ya Wananchi Mwanga) na kusema kuwa “Tulipoanzisha benki hii tulikuwa na lengo la kuwa benki ya jamii, na nipende kumpongeza Mwenyekiti wa Bodi pamoja na bodi yake kwa kazi kubwa walioifanya na naomba muendelee na kazi nzuri ambayo mmeianzisha, vilevile nipende kuwaomba wanahisa wote kutafakari jinsi benki hii inavyowasaidia kimaendeleo”.

Aliongeza kuwa “Nipende kuomba benki hii iendelee na mchakato wa kuwa benki kubwa ya biashara, na isisahau kuhudumia wateja wadogo wadogo ambao ndio walikuwa lengo kuu la kuanzishwa wka benki hizi za kijamii”.

Na Mwakilishi kutoka Benki Kuu ya Tanzania (BOT), Bw. Leodgar A. Haule, aliipongeza benki kwa kufanya vizuri kwa kipindi cha muda mfupi na aliipongeza kwa mtaji ambao umepata hadi kufikia hatua ya kuwa benki ya biashara. Na kusema kuwa “Nipende kuwapongeza wote,hasa uongozi wa benki ya Mwanga Hakika pamoja na wanahisa wote kwa juhudi mzifanyazo kuhakikisha benki hiyo inapata maendeleo zaidi, pia niiombe benki hii iendelee kufanya kazi kwa bidi na kufuata sheria mbalimbali zilizopo.

Aidha, alisema kuwa, Benki Kuu, itaendelea kusimamia na kutoa ushauri kwa benki kama msimamizi mkuu wa Mabenki nchini.


Huyo ni Mwenyekiti wa bodi ya Wakurugenzi wa benki ya Mwanga Hakika,Eng.Ridhiwani Mringo akizungumza na wanahisa wa benki ya Mwanga Hakika,wilayani Mwanga mkoani Kilimanjaro.
Waziri mkuu mstaafu, mshauri na mwanahisa wa benki ya Mwanga Hakika Mhe.Cleopa Msuya akizungumza na wanahisa kwenye mkutano mkuu wa pili uliofanyika 27-08-2022 Wilayani Mwanga, mkoani Kilimanjaro.




Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...