Na Farida Mangube, Morogoro


SERIKALI ya awamu ya sita chini ya Wizara ya Maji kupitia Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Morogoro (MORUWASA),imeanza kutekeleza mradi mkubwa wa maji wenye thamani ya Sh bilioni 185 kwenye Manispaa ya Morogoro.

Fedha hizo zinatokana na ufadhili kutoka Shirika la Maendeleo la Ufarasa (AFD), ambao unalenga kuboresha Bwawa la Mindu na mundombinu ukiwemo ujenzi a mtambo mpya wa kutibu maji eneo la Mafiga.

Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Morogoro (MORUWASA), Mhandisi Tamimu Katakweba alisema hayo jana kwenye taarifa yake mbele ya Kiongozi wa mbio Kitaifa 2022 , Sahil Geraruma.

Mwenge wa Uhuru uliweka jiwe la msingi kwenye mradi wa uboreshaji wa huduma ya maji kwa wananchi wa Mitaa ya Kasanga na Mgaza ambao idadi yao imeongezeka kutoka 3,918 mwaka 2014 na sasa kukadiriwa kufikia wakazi wapatao 10,000

 Mhandisi Katakweba alisema mradi huo wa kimkakati unatarajia kukamilika mwaka 2025 ambao utazalisha maji lita milioni 89 ukilinganisha na mahitaji ya lita 86 kwa siku mwaka 2025.

Alisema umejikita kuboresha Bwawa la Mindu kwa kunyanyua kuta na kuondoa tope , ujenzi wa mtambo mpya wa kutibu maji utakaojengwa eneo la Mafiga, ujenzi wa mabirika ya kuhifadhi maji yenye uwezo wa kuhifadhi lita milioni 11 kwa wakati mmoja na utafutaji wa vyanzo vya maji mbadala ukiwemo maji ya chini ya ardhi.

Mhandisi Katakweba alisema kwa sasa mahitaji ya maji kwa Manispaa hiyo ni lita milioni 73 kwa siku ulilinganisha na lita milioni 35 zinazozalishwa kwa sasa .

Kwa upande wa mradi wa uboreshaji wa huduma ya maji Kasanga ulibuniwa na Manispaa ya Morogoro mwaka 2014 ulikuwa na lengo la kuhudumia wakazi 3,918 wa mtaa wa Kasanga na Mgaza na ulikabidhiwa kwa mamlaka 2017 kwa ajili ya uendeshaji.

Alisema mradi huo ulitekelezwa na fedha za Mpango wa Maendeleo kwa Ustawi wa Taifa na Mapambano dhidi ya Ugonjwa wa Covid -19 ambapo kiasi cha Sh milioni 590.9 zilitolewa na Serikali ,wakati Sh milioni 25.3 zilizotolewa na Moruwasa zilitumika kuboresha mradi huo ili wananchi wa mitaa ya Kasanga na Mgaza wapatao waweze kupata huduma bora ya maji.

Alisema mradi huo ulikabidhiwa kwa Mamlaka hiyo mamlaka 2017 kwa ajili ya uendeshaji na baada ya maboresho makubwa utapunguza tatizo la mgao wa maji kwa wananchi wa Kata ya Mindu kutoka siku 14 za awali na sasa watapata maji kila baada ya siku moja.

Hivyo alisema mradi huo baada ya uboreshaji mkubwa utakuwa na uwezo wa kusambaza maji lita 700,000 kwa siku huku mahitaji yakiwa ni lita 941,500.

“ Mradi huu mwaka huo ulipokelewa ukiwa na changamoto mbalimbali ikiwemo, usanifu ulizingatia kutoa huduma kupitia vizimba badala ya kuunganisha maji kwenye nyumba za wananchi kama sera ya maji ya mwaka 2002 inavyoelekeza” alisema Mhandisi Katakweba

Pia alisema serikali kupitia Mamlaka hiyo imekalisha miradi ya maji ya matokeo ya haraka kwenye maeneo ya Bigwa-Bohmela, Mambogo-Kihonda, Mkundi – Lukobe, Mindu, Mgadu, Kauzeni na Bong’ola ambapo Sh Bilioni 12 na itaongeza lita milioni 17 kwenye mfumo hivyo kuongeza uzalishaji toka asilimia 48 za sasa na kufikia asilimia 71 kufikia Juni 2023.

Kwa upande wake Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa Geraruma licha ya kupongeza hatua hizo aliwataka wananchi wa Manispaa hiyo wakiwemo wa kata ya Mindu kupanda miti kwenye vyanzo vya maji na kuacha kufanya shughuli za kijamii kweye vyanzo hivyo.

“Tusilime kwenye vyanzo vya maji tusifuge kwenye vyanzo vya maji na shughuli nyingine zote tusifanye kwenye vyanzo vya maji cha zaidi ndugu zangu wana Mindu tutunze vyazo vya maji au kupanda miti rafiki kwenye vyanzo vya maji” alisema Geraruma

Kwa upande wake Mbunge wa Jimbo la Morogoro Mjini Abdulaziz Abood alimpongeza Mkurugenzi Mtendaji wa Moruwasa kwa ushirikiano mkubwa anaoutoa kwa ofisi ya mbunge katika kuhakikisha wananchi wa jimbo hilo wanapata huduma ya maji safi na salama.



Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...