
Mkuu wa Wilaya ya Rungwe, Dk. Vincent Anney (katikati) akifungua bomba kuashiria uzinduzi wa kiwanda kipya cha kampuni ya TOL Gases Limited katika kijiji cha Ikama Wilaya ya Rungwe mkoani Mbeya katika hafla iliyofanyika tarehe 29 Julai 2022.
Kampuni ya TOL Gases Limited, mnamo tarehe 29 Julai 2022, imezindua mradi wake wa nne wa gesi ya ukaa (carbon-dioxide) katika kijiji cha Ikama, wilayani Rungwe mkoani Mbeya. Mradi huo mpya unakuza uwezo wa kampuni hiyo kuzalisha gesi ya ukaa kwa matumizi ya viwandani na katika huduma za afya.
Mradi huo uliozinduliwa hivi karibuni ni wa pili katika kijiji cha Ikama na kinatarajiwa kuanza uzalishaji rasmi mnamo Desemba 2022. Hatua hii itaiwezesha kampuni kupanua soko lake katika soko la ndani na la nje katika nchi kama Zambia, Zimbabwe, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na Malawi.
Mradi huo wenye thamani ya shilingi bilioni 13.65, unakadiriwa kuwa na uhai wa miaka 20 na uwezo wa kuzalisha tani 2 kwa saa. Gesi ya ukaa hutumiwa katika matumizi mbalimbali ya viwanda na matibabu kama vile katika uzalishaji wa vinywaji na usindikaji wa bidhaa za chakula. Pia ni nyenzo muhimu katika utengenezaji wa vifaa vya kuzima moto.
Akizungumza katika uzinduzi huo, Mgeni Rasmi, Mkuu wa Wilaya ya Rungwe - Dkt. Vincent Anney aliipongeza kampuni ya TOL Gases kwa kuendelea kuwekeza na kuahidi kuendeleza ushirikiano na kampuni hiyo. “Kama kampuni ambayo imekuwa na mchango mkubwa katika sekta ya viwanda na afya, tutashirikiana kwa karibu na kampuni ili kuhakikisha kazi yake inaendelea kunufaisha jamii na nchi kwa ujumla,” alisema Dkt. Anney.
Akizungumzia mradi huo mpya, Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya TOL Gases Limited, Daniel Warungu alisema, “Gesi ya ukaa inayozalishwa na kampuni ya TOL Gases Limited ina mchango mkubwa katika ukuaji wa uchumi wa viwanda na maendeleo ya nchi kwa ujumla. Uzinduzi wa mradi huu mpya ambao ni wa pili katika kijiji hiki cha Ikama, ni mwendelezo wa jitihada zetu za kuunga mkono dira ya serikali ya uchumi wa viwanda kupitia utengenezaji wa bidhaa za ndani."
Warungu pia aliongeza kuwa kampuni hiyo inaendelea kuzalisha aina nyingine za gesi za viwanda na za hospitalini katika viwanda vyake vitatu vilivyopo Dar es Salaam, Mwanza na Mbeya. Kiwanda kipya cha Ikama kitaongeza maradufu uwezo wa kampuni wa kuzalisha gesi ya ukaa na kuhakikisha upatikanaji wa gesi hiyo.
“Tunatarajia ongezeko la shilingi bilioni 8.2 katika mapato ya mwezi ikiwa ni ongezeko la asilimia 42 ya mapato yatokanayo na gesi ya ukaa pekee, hii itakuza mchango wetu katika mapato ya Serikali kupitia ulipaji wa kodi na tozo za huduma katika halmashauri ambazo kampuni yetu inafanya kazi.", aliongeza Warungu.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...