Mkurugenzi wa Kitengo cha Diaspora, Mhe. Balozi James Bwana na Afisa Mkuu wa Wateja Wakubwa na Serikali, Bw. Alfred Shao wakibadilishana Hati ys Makubaliano ya kutengeneza mfumo wa kidijitali wa kutunza taarifa za Diaspora.
Afisa Mkuu wa Wateja Wakubwa na Serikali, Bw. Alfred Shao na Mkurugenzi wa Kitengo cha Diaspora, Mhe. Balozi James Bwana katika picha ya pamoja na wafanyakazi wa Benki ya NMB baada ya kusainiwa kwa Hati ya makubaliano jijini Dar es Salaam.
…………………………………………………….
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki na Benki ya NMB wamesaini Hati ya Makubaliano ya kutengeneza Mfumo wa Kidigitali, (Diaspora Digital Hub System) ambapo benki hio imedhamini Shilingi Milioni 100 ili kuboresha huduma za mfumo huo zenye kukidhi mahitaji ya Diaspora.
Mkurugenzi wa Kitengo cha Diaspora Mhe. Balozi James Bwana alisema mfumo huo wa kidigitali utaisaidia Serikali kuwatambua, kuwasajili na kuwawezesha Diaspora wa Tanzania waliopo sehemu mbalimbali ulimwenguni kupata huduma mbalimbali ikiwemo za kibenki na kushiriki kidigitali katika shughuli mbalimbali za maendeleo, biashara, uchumi na uwekezaji nchini.
Lakini pia, itafungua uwezekano wa fursa zaidi na kufahamu kwa ufasaha idadi ya Diaspora, ujuzi, elimu na wenyewe wataweza kupata huduma mbalimbali kwa ajili ya mahitaji yao.
Kwa upande wake Afisa Mkuu wa Wateja Wakubwa na Serikali wa NMB, Bw. Alfred Shao alisema kuwa wanaamini kukamilika kwa mfumo huo kutawawezesha Diaspora wa Tanzania kuungana, kutambulika na kuiwezesha Serikali kuwa na Kanzi Data ya uhakika na kuwafikia diaspora wengi kwa wakati mmoja na hivyo kuleta mafanikio makubwa kwa Taifa na Mtanzania mmoja mmoja anayeishi nje ya nchi.
Makubaliano hayo yamesainiwa na Mkurugenzi wa Kitengo cha Diaspora Mhe. Balozi James Bwana kwa niaba, Afisa Mkuu wa Wateja Wakubwa na Serikali, Bw. Alfred Shao na kushuhudiwa na Kaimu Katibu wa Bodi ya Wakurugenzi wa NMB, Consolatha Mosha na Mwanasheria wa Wizara – Miriam Kilo katika Ofisi Ndogo za Wizara jijini Dar es Salaam.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...