KAMPUNI ya Japan Tobacco Incorporation (JTI) imeahidi kununua kilo milioni 30 za tumbaku kutoka kwa wakulima wa Tanzania katika msimu ujao wa kilimo.

 

Ahadi hiyo imetolewa leo (Jumatatu, Septemba 26, 2022) na Rais na Mtendaji Mkuu wa JTI, Bw. Masamichi Terabatake mbele ya Waziri Mkuu Kassim Majaliwa aliyetembelea ofisi zao ili kuwahakikishia utekelezaji wa mazungumzo yaliyofanyika wakati wa mkutano wa TICAD 8, jijini Tunis, Agosti, mwaka huu.

 

Akizungumza baada ya kikao hicho, Waziri Mkuu amesema uamuzi wa kampuni hiyo kuongeza kiwango cha ununuzi wa tumbaku utatoa ahueni kwa wakulima wa Tanzania ambao walikuwa hawana uhakika wa soko la zao hilo.

 

“Leo Bodi ya Wakurugenzi imetangaza uamuzi wa kununua kilo milioni 30 za tumbaku kutoka kilo milioni 14 ambazo walinunua msimu uliopita. Hii ni fursa kubwa kwa wakulima wetu kwani kiasi hicho ni zaidi ya uzalishaji wa zao la tumbaku Tanzania,” amesema.

 

“Miaka ya nyuma makampuni yaliyokuwa yakinunua tumbaku yalizoea kuwapangia wakulima wetu idadi ya kilo za kununua, kwa hiyo hata uzalishaji haukuwa mkubwa sana. Nikiwa ziarani Tabora, nilikutana na viongozi wakuu wa vyama vya wakulima wa zao hili, na waliomba kupewa fursa ya kuongeza soko, kwa hiyo wakulima sasa waongeze uzalishaji ili tufikie lengo hili,” amesisitiza.

 

Mazungumzo hayo yalihudhuriwa na Mwenyekiti wa Bodi ya JTI, Bw. Mutsuo Iwai na Meneja Mkuu wa Kampuni ya Sigara Tanzania (TCC), Bw. Takashi Araki.

 

Waziri Mkuu yuko Japan akimwakilisha Rais Samia Suluhu Hassan kwenye mazishi ya Waziri Mkuu mstaafu wa nchi hiyo, Bw. Shinzo Abe yanayotarajia kufanyika kesho.

 


 

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...