Na Karama Kenyunko Michuzi TV

MAHAKAMA ya Tanzania imejipanga kuachana na matumizi ya karatasi katika uendeshaji wa mashauri na kuingia kwenye matumizi kamili ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) ifikapo mwaka 2025

Jaji Kiongozi wa Mahakama ya Tanzania, Mustapha Siyani ameyasema hayo leo Septemba 30, 2022 wakati akizindua tovuti ya Mahakama ya Kuu Divisheni ya Kazi jana Dar es Salaam.

Jaji Siyani amesema kuwa kila mahakama inapaswa kutafuta na kubuni namna tofauti kulingana na uwezo wake, kusogeza huduma na kuwafikia wananchi wengi kwa wakati jambo ambalo litapunguza gharama za uendeshaji wa mashauri na kuboresha huduma zao kwa kuwafikia wananchi kwa wakati na mahali popote walipo.

Amesema kuanzishwa kwa tovuti hiyo ni njia mojawapo ya kuwafikia wananchi kwani kwa kutumia simu janja mwananchi anaweza kupata taarifa muhimu zinazohusu mahakama.

“Mahakama ya karne ya 21 ni tofauti na iliyokuwepo kabla kwani sera yetu inatutaka kutumia Tehama katika mahakama zote nchini na tumekusudia ifikapo mwaka 2025 tuwe na matumizi kamili ya mtandao kwa maana ya mahakama mtandao.’’ amesema Jaji Siyani

Amesisitiza kuwa matumizi ya mtandao yamekuwepo kabla ya uzinduzi wa tovuti hiyo, kwani wamekuwa wakisikiliza mashauri kwa njia ya video conference na kusajili mashauri kwa mtandao.

‘’Mahakama za Mwanzo hazina mashauri yanayozidi miezi sita hivyo mahakama nyingine ziige kasi hii kwani tunaamini tutafika tunapotaka,’’ alieleza.

Naye, Jaji Mfawidhi wa mahakama hiyo, Salma Magimbi amesema kuwa Januari mwaka huu walianza na mashauri 1,500 na kufunguliwa mashauri mapya 1,100 hivyo, wamemaliza mashauri 2,050 na kubaki na mashauri 546.

Amesema walikuwa na mashauri zaidi ya 100 ya mwaka 2021 na kwa kuwa mahakama hiyo ilianzishwa kwa lengo la kutatua migogoro ya kazi, walipewa jukumu la kumaliza mashauri ndani ya mwaka mmoja.

“Mashauri mengi yanayokuja huku ni ya marejeo kutoka Tume ya Usuluhishi na asilimia 95 ni migogoro ya kufukuzwa kazi isivyohalali. Hivyo tovuti yetu itasaidia kupunguza mlolongo wa mashauri na kuleta migogoro yenye kesi za msingi ili wengine waweze kuingia kwenye usuluhishi,’’ alieleza Jaji Magimbi.

Kwa upande wake, Jaji Biswalo Mganga, Mwenyekiti wa kamati ya uanzishaji tovuti hiyo, amesema tovuti hiyo inaungana na tovuti ya Shirika la Kazi duniani (ILO), pia inaonesha kesi zilizopangwa kusikilizwa na majina ya majaji au wasajili na kama hawapo ili kupunguza usumbufu kwa wateja wao.

Alisema kwenye tovuti hiyo kuna sheria mbili muhimu zinazotumika kwenye masuala ya kazi, kanuni, mikataba mbalimbali ya ILO sambamba na sera ya ajira ya mwaka 2008 hivyo hakuna haja ya mtu kwenda kutafuta sehemu nyingine.

"Pia kwenye tovuti hiyo tumeweka kiungo ‘links’ kinachoelekeza namna ya kupata maamuzi ya Mahakama Kuu na Mahakama ya Rufani ya mwaka 2016 na 2018 ambazo zimegawanywa katika vipengele tofauti" amesema Mganga.

 

Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Mustapher Siyani akizungumza kabla ya ufunguzi rasmi wa tovuti ya Mahakama Kuu ya Tanzania, Divisheni ya Kazi leo Septemba 30, 2022 Jijini Dar es Salaam

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Divisheni ya Kazi, Mhe. Salma Maghimbi akisisitiza jambo alipokuwa anaongea kwenye ufunguzi wa tovuti ya Mahakama hiyo leo Septemba 30,2022 jijini Dar es Salaam

Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Mustapher Siyani akibonyeza kitufe kwenye kompyuta mpakato kuashiria ufunguzi wa tovuti ya Mahakama Kuu Divisheni ya Kazi leo 30 Septemba, 2022.

Sehemu ya watumishi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Divisheni ya Kazi wakifuatilia ufunguzi wa tovuti hiyo.



Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...