Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi amesema Serikali kupitia Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini unaoratibiwa na Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) imejenga bweni katika Shule ya Sekondari Bukundi iliyopo Kijiji cha Bukundi wilayani Meatu, ili kuweka mazingira rafiki ya kuongeza ufaulu wa wanafunzi ikiwa ni pamoja na kuwaepusha na changamoto ya mimba za utotoni.

Naibu Waziri Ndejembi ameyasema hayo, mara baada ya kukagua bweni la wanafunzi wa shule ya Sekondari Bukundi akiwa katika ziara yake ya kikazi ya kukagua utekelezaji wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini katika Halmashauri ya Wilaya ya Meatu mkoani Simiyu.

Ndejembi amesema, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan ametafuta fedha hizo za TASAF na kujenga bweni hilo kwa ajili ya kutatua changamoto na adha zinazowakabili wanafunzi wa eneo hilo ambao kwa muda mrefu wamekuwa wakilazimika kusafiri umbali mrefu ili kuhudhuria masomo.

Kutokana na umuhimu wa bweni hilo, Mhe. Ndejembi ametoa mwenzi mmoja kwa viongozi na wasimamizi wa ujenzi wa bweni hilo kushirikiana kikamilifu na TASAF ili likamilike kwa wakati na kuanza kutoa huduma.

“Bweni hili likikamilika kwa wakati litaongeza ufaulu na kusaidia kuondoa changamoto ya mimba za utotoni, kwani wanafunzi wataishi katika eneo hili la shule badala ya kwenda kuishi kwenye jamii ambayo ina changamoto nyingi,”Amesema Ndejembi.

Ndejembi ameongeza kuwa, licha ya TASAF kuwezesha mradi wa bweni hilo lakini imejenga miradi ya maji, zahanati na vituo vya afya katika kipindi kifupi cha uongozi wa Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan, hivyo amewataka wananchi wa Kijiji cha Bukundi kulinda miradi hiyo ili iwanufaishe wananchi wa kijiji hicho na vijiji jirani.

" Sisi wananchi wa Bukundi tuna jukumu moja la kulinda miradi hii kwa manufaa yetu kwani serikali imetumia fedha nyingi kuitekeleza miradi hiyo,” Amesema Naibu Waziri Ndejembi.




 

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...