MBUNGE wa Jimbo la Mlimba, Godwin Kunambi amemshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuwezesha upatikanaji wa Kituo cha Afya katika Kata ya Uchindile na hivyo kuondoa adha ya wananchi wa kata hiyo kutembea umbali wa km 70 kufuata huduma za afya.
Kunambi ametoa kauli hiyo wakati alipofanya ziara ya kukagua ujenzi wa kituo hicho cha afya sambamba na kuzungumza na Wananchi wake ikiwa ni pamoja na kuwaeleza mafanikio ambayo Serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan imeyaleta.
" Kipekee sana nimshukuru Rais Samia Suluhu Hassan ambapo kwa muda mfupi tangu aingie madarakani amesikia kilio chetu wananchi wa Uchindile cha kutembea umbali wa km 70 kufuata huduma za afya na sasa ametuletea kiasi cha Sh Milioni 500 kwa ajili ya ujenzi wa Kituo cha Afya ambacho kinaelekea kumalizika ili kianze kutoa huduma kwetu wananchi.
Na sisi kama Wananchi kupitia mapato ya ndani ya Halmashauri ngazi ya Kijiji tumetenga Sh Milioni 90 kwa ajili ya kujenga nyumba za watoa huduma wetu wa afya ambapo tutajenga nyumba ya kuwezesha kuishi watoa huduma wetu watatu, lengo letu ni kuunga mkono juhudi za Rais Samia katika kuleta maendeleo," Amesema Kunambi.
Kuhusu miundombinu ya Barabara, Kunambi amesema ndani ya kipindi cha mwaka mmoja wamepokea Sh Milioni 500 kwa ajili ya kuboresha miundombinu ya barabara ambayo inaunganisha Kata ya Kamwene na Kata ya Uchindile.
" Pamoja na kutupatia fedha za ujenzi wa Kituo cha Afya lakini pia Rais Samia ametupatia fedha kiasi cha Sh Milioni 500 kwa ajili ya maboresho ya miundombinu ya barabara yetu inayounganisha Kata zetu mbili za Uchindile na Kamwene, maboresho haya ya barabara yatasaidia pia kuchochea uchumi wa pande zote mbili," Amesema Kunambi.

Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...