MSIMU
wa pili wa Tamasha la ‘NMB Kivumbi na Jasho,’ linalokutanisha timu za
michezo mbalimbali za Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Benki
ya NMB, utaunguruma kesho jijini Dodoma, hii ni baada ya leo benki hiyo
kuikabidhi Bunge SC vifaa vya michezo vyenye thamani ya Sh. Milioni 20.
Kivumbi
na Jasho ni bonanza linalolenga kujenga na kuimarisha mahusiano mema
baina ya Bunge na NMB, ambapo Bunge SC imeahidi kulitumia vema kama
ilivyofanya msimu uliopita, ili kuzipa makali timu zao zinazojiandaa na
Mashimdano ya Mabunge kwa nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki (EALA
2022).
Akizungumza wakati akipokea msaada wa vifaa hivyo,
Mwenyekiti wa Bunge SC, Tarimba Abbas, alisema wanalichukulia kwa uzito
mkubwa tukio la leo, na kuwa kwao Kivumbi na Jasho ni zaidi ya bonanza,
na wanalipa hadhi ya mashimdano, kwani limekuwa msaada katika maandalizi
yao ya EALA 2022.
"Tunatambua na kuthamini malengo ya bonanza
hili, lakini tuwe wazi kwamba kwetu ni zaidi ya hapo. Mwaka Jana
lilitupa kipimo sahihi kuelekea EALA 2021, ambako tuliibuka washindi wa
jumla katika michezo nane tuliyoshiriki. Tunatarajia kurejea mafanikio
hayo mwaka huu kupitia bonanza hili," alisema.
Tarimba ambaye pia
ni Mbunge wa Kinondoni, Dar es Salaam, alieleza kuwa wabunge,
wafanyakazi NMB na waalikwa watakaohudhuria hafla ya usiku baada ya
bonanza watapata fursa ya kuangalia 'live' kupitia televisheni kubwa
mechi ya Kombe la Shirikisho Afrika (CAF CC 2022/23), kati ya Yanga na
Zalan FC ya Sudan Kusini.
Kwa upande wake, Afisa Mtendaji Mkuu
(CEO) wa Benki ya NMB, Ruth Zaipuna, awali aliushukuru uongozi wa Bunge
SC na manahodha wa timu za michezo yote, kwa kuipa nafasi NMB ya
kuendelea na msimu wa pili wa bonanza hilo, ambalo hubeba fursa
mbalimbali sio tu kwa Bunge, bali taasisi zingine za Serikali.
“Bonanza
litaanza saa 12 asubuhi kwa matembezi yatakayoanzia Viwanja vya Bunge
hadi Chinangali Park itakochezwa michezo mbalimbali, kuthibitisha faida
za bonanza hili, tukifika pale tutakabidhi vifaa kwa ajili ya Hospitali
ya Uhuru, vyenye thamani ya Sh. Mil. 50 na baada ya hapo, ndipo Kivumbi
na Jasho kitakapoanza.
“Program hii ya Kivumbi na Jasho
tuliianzisha mwaka jana, na tuwahakikishie wabunge kwamba bonanza hili
litakuwa endelevu, na hii yote ni katika kuhakikisha kwamba tunaendeleza
mashirikiano mazuri yaliyopo baina yetu na Wabunge, Ofisi ya Bunge na
Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,” alisema.
Zaipuna
alibainisha kwamba michezo ni afya, ni biashara, ni ajira. Lakini pia ni
kazi na kwamba ushiriki wa wabunge - ambao ni wawakilishi wa wananchi,
unatoa na kuakisi taswira ya umuhimu wa michezo kwa taifa na vijana kwa
ujumla, huku akiwakaribisha wakazi wa Dodoma kuhudhuria bonanza hilo.
Vifaa
vilivyokabidhiwa kwa timu za Bunge ni pamoja na ‘track suit’ maalum na
jezi za soka, netiboli, wavu, kikapu. Baadhi ya michezo
itakayoshindaniwa, ni mpira wa miguu, mikono, kikapu, wavu, kuvuta
kamba, kukimbiza kuku, mbio za magunia, mbio fupi na mingineyo, ambapo
washindi watakabidhiwa vikombe na medali.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...