Na WAF- KAGERA.
Katibu mkuu Wizara Prof. Abel Makubi ameelekeza Wataalamu wa afya katika mipaka kuimarisha huduma za uchunguzi wa magonjwa ikiwemo ugonjwa wa Ebola ili kuweza kuutambua na kuuzuia endapo utaingia nchini.
Prof. Makubi ametoa rai hiyo, mapema leo wakati akitembelea Mpaka wa Tanzania na Uganda -MTUKULA na kukagua zoezi la uchunguzi wa abiria wanaoingia nchini Tanzania.
Katika ziara hiyo aliyoambatana na Mkuu wa Wilaya ya Misenyi, Prof. Makubi ameshuhudia upimaji wa kutumia Thermoscans ikiwa ni moja ya njia ya kutambua hali ya maambukizi endapo mgonjwa atatokea.
Hata hivyo, Prof. Makubi ameelekeza kutumika kwa dodoso la kutambua dalili za ugonjwa wa Ebola kama njia nyingine ya kutambua hali ya maambukizi endapo mgonjwa atatokea.
Kwa upande mwingine, Prof. Makubi amekutana na wakazi wa mpakani katika eneo la Mtukura, huku akielekeza Wataalamu wa Afya kutoa elimu kwa wakazi hao juu ya namna bora ya kujikinga dhidi ya ugonjwa wa Ebola ili usiingie nchini.
Aidha, Prof. Makubi ameendelea kuhimiza kuwekwa kwa mifumo ya kunawa mikono katika mitaa, maeneo ya vituo vya abiria, daladala, sehemu za ibada, ofisi na majumbani ikiwa ni sehemu ya mikakati ya kupambana dhidi ya magonjwa ya mlipuko ikiwemo ugonjwa wa Ebola.

Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...