Na Said Mwishehe, Michuzi TV

SERIKALI kupitia Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari imesema kuna mkakati wa kampeni ya kitaifa itakaofanyika nchi nzima kutoa elimu mtandao kwa wananchi ili kuhakikisha sheria,kanuni na miongozo iliyopo inafuatwa kwa lengo la kuepuka changamoto zinazojitokeza kutokana na matumizi ya mitandao.

Akizungumza jijini Dar es Salaam wakati akifungua mkutano wa vijana wa kujadili Usimamizi wa masuala ya mitandao uliondaliwa na Shirika la Intanet Society Tanzania(IST), Mkurugenzi Msaidizi sehemu ya usalama mitandao Wizara ya Habari ,Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Mhandisi Stephen Wangwe amesema kampeni hiyo inatarajia kuanza rasmi Oktoba mwaka huu.

“Pamoja na mambo mengine lakini kwa ngazi ya Wizara tunahusika zaidi na utengenezaji wa sera, sheria miongozo na taratibu mbalimbali za kutusaidia na kuwasaidia wananchi kuwa na matumizi salama ya mitandao yetu , hivyo siku ya leo miongoni mwa mambo niliyowasilisha kwa vijana hawa nimewaeleza Septemba 23 kwenye Bunge letu ule muswada wa Sheria ya Ulinzi wa taarifa binafsi umesomwa rasmi na sasa ni nyaraka ya umma.

“Kwa hiyo watu ambao hawakupata fursa tangu mchakato umeanza huu ndio muda wao wa kupitia na kuaingalia wanaweza kutoa maoni gani na yote ni kuhakikisha tunakuwa na Sheria itakayokuwa nzuri kwa sisi wote.Pia ni wakati mzuri kwa umma kutafuta muda na wakati kuielewa hii sheria na kujua ni mambo gani ya kwenda kushughulikia,”amesema.

Ameongeza kuwa uwepo wa Sheria hiyo itakwenda kufungua fursa kwani kuna baadhi ya wawekezaji wakubwa wanaoshughulika na masuala ya TEHAMA wanabanwa na nchi zao kuja kuwekeza kwenye nchi ambazo hazina mfumo wa kisheria wa ulinzi wa taarifa binafsi.Hivyo ujio wa sheria ni matarajio ya Serikali wawekezaji wakubwa kutoka nchi mbalimbali watakuja kuwekeza nchini kwenye masuala ya mtandao.

“Lingine ambalo nimesisitiza ni kwamba katika masuala ya usalama wa mtandao ni muhimu kupata uelewa yaani elimu kwa umma kwani watu wengi huwa wanapata matatizo kwasababu uelewa wao, inawezakana hayupo vizuri katika maeneo fulani fulani hususan wanaweza kupata madahara fulani anapofanya jambo fulani kwenye mtandao.

“Unakuta watu wanafanya jambo fulani kwa faragha au starehe zao lakini baadae inawaletea matatizo. Hivyo Serikali tunao mkakati wa kitaifa wa kutoa elimu kwa umma kuhusu elimu mtandao na tutazunguka katika makundi yote kuanzia ngazi za Serikali na binafsi, makundi ya wanafunzi, kaya mbalimbali na kuhakikisha makundi yote ya umma yanafikiwa na kuelimishwa namna gani ya kuweza kutumia mitandao vizuri ili isituletee changamoto katika siku za usoni,”amesema Mhandisi Wangwe.

Amesisitiza kampeni itaanza Oktoba mwaka huu kwa kuwa mwezi huo ndio mwezi wa usalama katika mtandao duniani, hivyo wameona ndio utakuwa wakati muafaka wa sisi kuanza kampeni hiyo rasmi.

Kwa upande wake Rais wa Shirikisho la Intanet Tanzania ambaye pia ni Mratibu wa Jukwaa la Usimamizi wa Mitandao nchini Nazar Kilama amesema mkutano wa usimamizi wa masuala ya mitandao kwa upande wa vijana unalenga kuwajengea vijana uwezo wa kushiriki katika mifumo ya Intanet au mifumo ya masuala ya mitandao duniani.

“Hii mikutano imekuwa ikifanyika katika kila nchi, kikanda , Afrika na Dunia, kwa upande wa Tanzania ndio inaitwa foramu ya Tanzania , upande wa Afrika Mashariki inaitwa foramu ya Afrika Mashariki, Afrika na dunia ambayo iko chini ya umoja wa mataifa.Kwa hiyo lengo la hii foramu kwanza ni kuendelea kuwajengea vijana uwezo wa namna ya kushiriki hii mikutano ya kitaifa, kikanda na kidunia kwenye masuala ya usimamizi wa mtandao.

“Kwa hiyo hii foramu ya kwetu hapa kwanza ni kuwapa vijana uwezo wa kuweza kushiriki kwenye mijadala mbalimbali ambayo inafanyika kwenye hayo maeneo mengine ambayo nimeyataja mkapa kuelekea huko umoja wa mataifa, tunaamini vijana wana uwezo mkubwa tu wa kushiriki lakini inahitaji pia watu wanaojua kama sisi na wengine ambao wako kwenye hii mifumo ya Tehama kutoa muda wao ili kuwajengea uwezo vijana na kushiriki vizuri kama Tanzania kwenye hayo maeneo mengine.

“Leo tumekuwa na mkutano wa pili , mkutano wa kwanza ulifanyika mwaka 2021 na huu ni mkutano wa pili na mwakani tutaendelea kuwajengea vijana uwezo maana watakuwepo tu na wenye uwezo tungependa waendelee kuwajengea vijana uwezo.Pia tunawashukuru Wizara kuja kutuunga mkono,”amesema.

Wakati huo huo Mwenyekiti wa Foramu hiyo Catherine Fungo amesema mkutano huo umeshirikisha vijana 50 ambao wamepatkana baada ya kujaza fomu na wengi ni wanafunzi kutoka vyuo vikuu mbalimbali.“Lengo vijana kujengewa uwezo ambao utawawezesha kuzungumza na kutoa maoni na ushauri kabla ya maamuzi kufanyika.”

Washiriki wakiwa kwenye Mkutano huo.
Mkurugenzi Msaidizi wa Usalama Mtandao kutoka Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Mhandisi Shephen Wangwe ( wa kwanza kushoto) akifuatilia majadiliano wakati wa mkutano wa vijana unaohusu masuala ya Mtandao.
Baadhi ya washiriki wakiwa kwenye Mkutano wa Vijana wenye lengo la kujengewa uwezo kuhusu masuala ya Mtandao.
Mmoja ya washiriki akitoa maoni yake kuhusu matumizi sahihi ya masuala ya Mtandao kwa vijana


Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...