Na Mwandishi Wetu- Dodoma
SERIKALI kupitia Wizara ya Elimu,Sayansi na Teknolojia imesema kuwa ili kupata matokeo mazuri ya elimu ni lazima kuhakikisha upatikanaji wa lishe bora shuleni ili kuwajengea wanafunzi afya bora na kupata utulivu wa akili wawapo madarasani.

Akizungumza Jijini Dodoma wakati wa hafla fupi ya Utiaji Saini Fomu ya kujiunga na Muungano wa Chakula Shuleni Naibu Waziri wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Mh.Omary Kipanga amesema kuwa Pamoja na kuwepo kwa sera hiyo, utoaji wa huduma ya chakula shuleni umekuwa ukitekelezwa katika shule kwa namna na viwango tofauti.

Alisema Katika kuboresha mazingira ya ufundishaji na ujifunzaji, upatikanaji wa matokeo mazuri ya elimu hutegemea afya aliyonayo mwanafunzi huku Sera ya Elimu na Mafunzo ya mwaka 2014 ikifafanua upatikanaji wa huduma muhimu katika shule na vyuo ikiwemo huduma ya chakula bora, maji safi na salama na upatikanaji wa huduma za afya kwa wanafunzi.

" Sera ya Elimu na Mafunzo ya mwaka 2014 inafafanua kuhusu upatikanaji wa huduma muhimu katika shule na vyuo ikiwemo huduma ya chakula bora, maji safi na salama na upatikanaji wa huduma za afya kwa wanafunzi ndio maana leo kwa pamoja hapa tunatia saini fomu ya kujiunga na Muunganowa ChakulaShuleni nia ni ile ile ya kuhakikisha wanafunzi wanasoma vizuri na kupata matokeo mazuri . "Amesema Mh.Kipanga .

Mh.Kipanga amesema Mwezi Oktoba, 2021 Wizara ya Elimu ilizindua Mwongozo wa Kitaifa wa Utoaji wa Huduma ya Chakula na Lishe kwa Wanafunzi wa Elimumsingi ili kuweka utaratibu wa kitaifa ambao utawezesha wanafunzi kupata huduma hiyo muhimu.

"Kutokana na hali hiyo, baadhi ya wanafunzi wamekuwa wakinufaika na wengine kukosa huduma hiyo muhimu sasa naamini kupitia Muungano huu utasaidia kuziba yale mapengo yaliyokuwepo na wanafunzi sasa hawatakuwa na sababu yeyote ya kutopata matokeo mazuri," Amesema Mh.Kipanga.

Katika hatua nyingine ,amesema kuwa utoaji wa huduma ya chakula na lishe shuleni ni suala mtambuka linalohitaji ushiriki wa sekta na wadau mbalimbali na kwa upande wa Tanzania, Muungano huu, ni jukwaa muhimu la kupata uzoefu wa namna nzuri ya kutekeleza mpango wa chakula shuleni kwa kushirikisha jamii na kufahamu wadau ambao tayari wapo kwenye muungano na wangependa kufadhili shughuli mbalimbali za kuwezesha upatikanaji wa chakula shuleni.

"Kujiunga na muungano huu kutawezesha wadau wetu wa maendeleo,mashirika yasiyo ya kiserikali, Makampuni binafsi pamoja na vyombo vya Habari, kuendelea kushirikiana na Serikali katika kuhamasisha jamii kuhusu umuhimu wa chakula na lishe shuleni,"Amesema Mh. Kipanga.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkaazi Shirika la Mpango wa Chakula Duniani (WFP), Sarah Gordon-Gibson amesema kuwa moja ya njia ya kufikia malengo kwa taifa lolote Duniani ni lazima kuwekeza kwa watoto hivyo ili kufikia huko lishe ni eneo linalohitaji maboresho makubwa.

Naye Mkuu wa Ofisi Ndogo ya Shirika la Mpango Chakula Duniani (WFP) Dodoma Nima Sitta amesema ni Muungano wa kimataifa wa chakula shuleni ni jukwaa la kuhakikisha nchi zote duniani ifikapo 2030 kila mtoto anapata angalau mlo mmoja shuleni.

Nao baadhi ya wanafunzi wakiwemo Beatrice Mtembi wa shule ya Sekondary Dodoma na Lucas Mathias anayesoma shule ya msingi ya mfano Chifu Mazengo wameishukuru Serikali kwa hatua hiyo muhimu kwani itasaidia kuongeza ufaulu darasani na kuepuka vishawishi vitakavyosababisha kutotimiza ndoto zao.
Naibu Waziri wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Mhe.Omary Kipanga (kushoto) na Mkurugenzi Mkaazi Shirika la Mpango wa Chakula Duniani (WFP),Sarah Gordon-Gibson (Kulia) wakikabidhiana Fomu ya Makubaliano ya kujiunga na Muungano wa Chakula Shuleni baada ya kutia saini katika hafla iliyofanyika Jijini Dodoma.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...