NA Said Mwishehe, Michuzi TV
ASASI ya AGENDA imeshauri kwamba umefika wakati kwa sasa kufanyika utafiti kwa ajili ya kuangalia madini ya risasi yanayotumika kwenye utengenezaji wa rangi ili kuwa na uhakika ikiwa nchi yetu haizalishi tena, kusambaza, kuuza au kutumia rangi zenye risasi.
Ushauri huo umetolewa leo Oktoba 27,2022 jijini Dar es na Asasi ya AGENDA wakati wa maadhimisho ya Wiki ya kimataifa ya kuzuia madhara ya madini ya risasi na dhamira kuu ni kulinda afya ya watoto kwa kuongeza kasi ya utekelezaji hatua za kuondoa matumizi ya rangi zenye madini ya risasi.
“Tangu mwaka 2009 , asasi na mashirika wanachama wa IPEN zimefanya tafiti zaidi ya 100 kwenye rangi zaidi ya 4,000 kutoka nchi 59 ikiwemo Tanzania ambako AGENDA ilishiriki , na utafiti wa mwisho ulifanywa na GENDA mwaka 2017 ambapo asilimia 46 ya rangi za mafuta zinazotumika kupamba majengo na vitu vinavyotumia na zinazouzwa nchini Tanzania zilionekana kuwa na kiwango cha risasi zaidi ya sehemu 90 kwa mamilioni baadhi zikiwa na kiwango cha juu sana vya risasi hadi sehemu 84,000 kwa milioni,”amesema.
Hivyo amesema kwa sasa kuna haja ya kufanya utafiti sawa na huo ili kuwa na uhakika ikiwa nchi ya Tanzania haizalishi tena, kusambaza, kuuza na kutumia rangi zenye risasi huku akieleza ushahidi wa miongo kadhaa umeonesha kuwa hakuna kiwango salama cha madini ya risasi.
“Risasi ni sumu kali inayoathiri mifumo mingi ya mwili nan i hatari sana kwa watoto wadogo walio chini ya miaka sita, Hata katika kipimo cha chini , risasi inaweza kuathiri ukuaji wa ubongo na watoto na hivyo kusababisha kupungua kwa kiwango cha uelewa au uakili(IQ)…
“Mabadiliko ya kitabia kama vile kupungua figo, viungo vya uzazi na mifumo wa kinga na kusababisha upungufu wa damu na shinikizo la damu.Athari katika mfumo wa fahamu na za kitabia zinazosababishwa na risasi kwa kawaida haziwezi kutenduliwa au kuondolewa,”amesema.
Kwa upande wake Ofisa Programu Mkuu wa AGENDA Silvani Mng’anya amesema ili kukomesha matumizi ya rangi zenye risasi nchini Tanzania , AGENDA inatoa mwito kwa Serikali ikijumuisha Shirika la Viwango Tanzania(TBS), ofisi ya makamu wa Rais –Idara ya mazingira , Mamlaka ya Mkemia Mkuu wa Serikali, Baraza la Taifa la Mazingira la Usimamizi wa Mazingira(NEMC),Mamlaka ya Usalama wa Afya Mahali pa Kazi(OSHA) na wadau wengine kutekelez kwa uthabiti kiwango cha udhibiti wa risasi katika rangi ambacho kilipitishwa mwaka 2017.
Aidha watengenezaji wa rangi, waagizaji, wasambazaji na wauzaji waunge mkono juhudi za Serikali kwa kushughulika na rangi isiyo na risasi pekee .Hilo linawezekana kabisa na tayari baadhi ya watengenezaji wa rangi wamekuwa wakitengeneza rangi isiyo na risasi kwa zaidi ya mitano sasa.
“Serikali na wadau wengine kutoa elimu ya uelewa kwa umma kuhusu madhara yatokanayo na matumizi ya rangi zenye risasi.Pia wanatoa mwito kufanyika utafiti mpya ili kujua hali ya sasa kwa rangi nchini Tanzania, miaka mitano baada ya kiwango cha kitaifa kuidhinishwa,”amesema.
Pamoja na hayo amesema AGENDA ni asasi isiyo ya kiseikali inayokusudia kukuza utamaduni wa kuwajibika kwa mazingira miongoni mwa umma kwa ujumla kupitia uhamasishaji , utetezi , kujenga uwezo na ushiriki wa wadau nchini Tanzania na kwingineko.
Aidha amesema katika Wiki ya kuongeza uelewa duniani, AGENDA imefanya mkutano na wadau ili kushirikishana jitihada zinazochukuliwa katika kutekeleza kiwango cha Taifa cha rangi kilichopitishwa na Shirika la Viwango Tanzania(TBS) mwaka 2017 cha sehemu 90 milioni(milioni 90)kama kiwango cha juu cha risasi katika rangi .Pia inashiriki kutoa habari kwa umma ili kuwafahamisha kuhusu wiki hii muhimu na juhudi ambazp nchi imezifanya katika kuondoa madini ya risasi katika rangi nchini Tanzania.
“AGENDA ni mwanachama wa Mtandao wa Kimataifa wa kutokomeza uchafuzi –International Pollutants Elimination Network(IPEN) unaojumuisha asasi na mashirika ya kutetea watu kutoka nchi 125 duniani kote katika kuondoa kemikali , taka na vichafuzi vya sumu.IPEN ni mwanachama mwanzilishi wa muungano wa kimataifa wa kuondoa risasi katika rangi.”amesema Mng’anya.
Wakati huo huo Ofisa Mazingira kutoka Baraza la Taifa la Usimamizi wa Mazingira(NEMC) Kuruthum Nancy Shushu amesema wao majukumu yao makubwa katika kupunguza madini ya risasi ni pamoja na kuhakikisha maeneo ambayo yanahusika na bidhaa zinazotumia madini hayo ya risasi kwa mfano viwanda vya rangi wanahakikisha viwanda hivyo vinazingatia matakwa ya sheria ya mazingira.
“Miongoni mwa matakwa ya Sheria ya Mazingira ni kuhakikisha viwanda vinakuwa na vyeti vya tathimini ya mazingira ambavyo wamevipata baada ya Baraza kujiridhisha kuwa upo usalama wa kutosha wa kuzuia wafanyakazi kutoathrika na madini hayo wanapokuwa sehemu za kazi kwa maana ya viwandani.Lakini kwa upende mwingine baaza linatoa vibali vya kujishughulisha na taka hatarishi mbalimbali ikiwemo betri na taka nyingine ambazo tunaamini mara nyingi zinakuwa zimetengenezwa sana na madini ya risasi.
“Na bidhaa hizo zikashakuwa taka zinahitaji utaratibu maalumu wa kuharibiwa , kuteketezwa au kurejerezwa kwa maana tuna viwanda vya kurejezwa betri chakavu kwa hiyo viwanda hivyo tunahakikisha pia vinapokea betri kwa watu ambao wamesajiliwa na Baraza kwa ajili ya kukusanya, kusafirisha betri chakavu au taka ngumu zote ambazo tunaamini zinamadini ya risasi ili kuhakikisha madini hayo hayawezi kutoka au kuharibu mazingira na kuifikia jamii,”amesema Shushu.
Kwa upande wake Katibu Mtendaji wa ASASI ya AGENDA Haji Rehani amesema kumekuwa na jitihada mbalimbali za kuondoa madini ya risasi ambapo amefafanua mwanzoni Tanzania iliungana na dunia katika kuondoa madini ya risasi kwenye mafuta ya petroli na ikafanikiwa na sasa wako kwenye kuangalia changamoto nyingine ambazo zinachangia uchafuzi wa mazingira na mojawapo ni matumizi ya rangi yaliyoongezewa madini ya risasi wakati wa uaandaji wake.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...