Na Mwandishi Wetu

KATIKA jitihada za kuunga mkono serikali ya awamu ya sita katika kukabiliana na magonjwa yasiyo ya kuambukiza, Hospitali ya KAM Musika ya Kimara Korogwe jijini Dar es Salaam imeendesha kambi ya bure ya kupima saratani ya tezi dume.

Mamia ya wanaume walijitokeza kwenye hospitali hiyo jana kwaajili ya kupatiwa huduma hiyo ya vipimo bure ambapo wengi waliohojiwa waliipongeza hospitali hiyo kwa uamuzi wa kutoa huduma hiyo bure kwani wazee wengi hawana uwezo wa kumudu gharama za vipimo.

Saratani ya tezi dume imekuwa ikiwaathiri sana wanaume wenye umri kuanzia miaka 45 na kuendelea na wamekuwa wakitakiwa kwenda kupima mara kwa mara kupima ili wale wanaobainika kuwa na matatizo wapate matibabu mapema.

Akizungumza jana, Mkurugenzi wa Hospitali ya KAM Musika iliyoko Kimara Korogwe jijini Dar es Salaam, Dk. Kandore Musika alisema wameamua kuwapima bure wanaume saratani ya tezi dume kama sehemu ya kurudisha shukrani kwa jamii.

Alisema ni vizuri kupima mara kwa mara kwani iwapo mtu atabainika mapema kuwa na dalili za saratani ya tezi dume inakuwa rahisi kwake kupata matibabu na kupona kuliko kusubiri mpaka saratani ifikiea hatua mbaya.

Alisema wameamua kuandaa kambi hiyo ya bure ya siku moja kuwapa fursa wananchi wa maeneo ya Kimara kupima saratani ya tezi dume na wale watakaobainika kuwa na tatizo hilo waanzishiwe matibabu mapema.

“Ugonjwa wa saratani ya tezi ndume unawashambulia sana wanaume wenye miaka kuanzia 40 na kuendelea na hospitali ya KAM imeamua huduma hii bure kama shukrani kwa jamii inayotuzunguka,” alisema Dk. Musika

Alisema wanaume wengi hawana uelewa kuhusu saratani ya tezi dume hivyo wamelazimika kuwaelimisha kuhudu dalili zake ili waweze kuwahi hospitali watakapoziona.

Alisema mamia ya wanaume waliojitokeza kwenye kambi hiyo ya bure wamepewa somo la kutosha kuhusu dalili za ugonjwa huo na wameahidi kwenda kuelimisha wenzao.

“Mtu mwenye saratani ya tezi dume akichelewa akikaa nayo muda mrefu matokeo yake inasambaa mwili mzima na kushambulia kila sehemu kwa hiyo kupima mara kwa mara si jambo la kupuuza kwa wanaume watu wazima,” alisema

Alisema wameanza kutoa huduma hiyo bure mwaka huu na wamepanga kuhakikisha huduma hiyo inatolewa kila mwaka ili kusaidia kubaini wanaume wenye shida kama hiyo.

Alisema saratani ya tezi dume inapimwa kwa njia tatu ikiwemo ya kutoa damu, utra sound na njia ya kidole lakini wameamua kutumia njia ya damu ambayo wanaume wengi wanaipendelea.

“Hatutaishia kupima saratani ya tezi dume tu tutafanya utaratibu wa kupima bure saratani ya matiti na saratani ya shingo ya kizazi kwa wanawake kama sehemu ya kutoa shukrani kwa jamii tunayoihudumia,” alisema Dk. Musika

John Rwekaza (80), ambaye alipimwa saratani ya tezi dume aliishukuru hospitali ya KAM Musika kwa uamuzi wake wa kutoa huduma hiyo bure kwani wazee wengi hawana uwezo wa kwenda kupata vipimo hivyo.

“Nawashukuru sana na naomba isiwe mwisho kwasababu uwezo wetu ni mdogo kumudu gharama za matibabu na unaona umati uliojitokeza kuja kupima ni ushahidi kwamba watu wanapenda kupima ila gharama inawashinda,” alisema

Ramadhani Yusuf, alisema alisikia matangazo ya kuwepo kwa huduma hiyo na amefurahi kufika na kupata vipimo hivyo bure kwani wazee wengi waliojitokeza wasingemudu kwenda kulipia kwenye hospitali zingine.

Aliwashauri wanaume kwenda kupima kila wanaposikia fursa kama iliyotolewa na Hospitali ya KAM ili waweze kujua hali ya tezi dume na wanaokutwa na matatizo waweze kupata matibabu mapema.


Mkurugenzi wa Hospitali ya KAM Musika, Dk. Kandore Musika akizungumza na waandishi wa habari wakati wa uzinduzi wa kambi ya kuwapimam bure wanaume saratani ya tezi dume iliyofanyika jana kwenye hospitali hiyo Kimara Korogwe jijini Dar es Salaam.
Wananchi waliofika kwenye kambi ya kupima bure saratani ya tezi dume iliyoandaliwa na hospitali ya KAM Musika iliyoko Kimara Korogwe jijini Dar es Salaam wakipewa elimu kuhusu dalili za saratani ya tezi dume.
Sehemu ya wanaume waliojitokeza jana kupima saratani ya tezi dume kwenye hospitali ya KAM Musika Kimara Korogwe jijini Dar es Salaam wakisubiri kwenda kwenye vipimo.

Wananchi waliofika kwenye kambi ya kupima bure saratani ya tezi dume iliyoandaliwa na hospitali ya KAM Musika iliyoko Kimara Korogwe jijini Dar es Salaam wakisubiri kuingia kwa daktari kwa ajili ya vipimo

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...