Na Stephen Kapiga, Mahakama Kuu-Mwanza
Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Prof Elisante Ole Gabriel amezindua rasmi kisima cha maji safi kwa ajili ya matumizi ya watumishi na wadau wa Mahakama katika jengo la Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki 'IJC' jijini Mwanza ambacho kinakuwa mwarobaini wa kutatua kero ya maji iliyokuwa ikiwakabili Watumishi wa Kituo hicho tangu kuanza kutumika kwa jengo hilo katikati ya mwezi Mei-2022.
Akizungumza jana tarehe 19 Oktoba mwaka huu na watumishi wa Mahakama zipatikanazo katika jengo hilo mara baada ya kumaliza zoezi zima la ufungaji wa pampu itakayokuwa inasukuma maji kutoka katika kisima hicho, Prof. Ole Gabriel alisema kuwa, upatikanaji wa kisima hicho utasaidia kupunguza gharama za upatikanaji wa maji katika jengo hilo tofauti na awali ambapo Mahakama ilikuwa ikilipa kiasi kikubwa cha fedha.
“Tulikuwa tunaumiza kichwa ni jinsi gani hasa tutaweza kuondoa changamoto hii, ila tunashukuru tumeweza kuchimba kisima cha mita 180 ambapo pampu yetu tumeiweka kwa umbali wa mita 170 na kubakiza umbali wa mita 10 kwa ajili ya usafi wa maji,” alisema Mtendaji Mkuu.
Aidha; Prof. Ole Gabriel aliwashukuru wachimbaji wa kisima hicho ambao ni Wakala wa Usambazaji Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) na hivyo kuwarejeshea utulivu Watumishi katika kutenda kazi.
Kwa upande wake, Mtendaji wa Mahakama Kuu-Kanda ya Mwanza, Bw. Tutubi Mangazini amekiri kuwa, upatikanaji wa kisima hicho utapunguza gharama kubwa walizokuwa wakitumia kwa ajili ya maji.
“Tumekuwa tukilipa pesa nyingi kama ankara ya maji kila mwezi, lakini sasa kiasi kikubwa cha pesa kinaenda kuokolewa kutokana na matumizi haya ya pampu ya kusukuma maji kwa kutumia umeme utokanao na jua” alisema Bw. Mangazini.
Akizungumza kwa niaba ya watumishi, Mhe. Helena Ngao alimshukuru Mtendaji Mkuu wa Mahakama kwa kuweza kuiona kero hiyo na kuweza kuishughulikia kwa wakati. “Sio tu tunatoa shukrani kwa hili la maji bali pia tunatoa shukrani kwa mengi ambayo umeweza kuyafanya ukiwa katika nafasi yako, kwani umekuwa ni mtu wa kutimiza ahadi zako, nakumbuka pia, uliahidi kutupatia basi baada ya kuona umbali wa lilipojengwa jengo hili na kweli umetimiza hilo kwa kutupatia basi jipya ambalo limerahisisha usafiri kwa watumishi kuja ofisini na hata kuwarejesha majumbani kwao pia” alisema.
Katika hatua nyingine, Prof. Ole Gabriel aliwapongeza watumishi kwa udumishaji wa usafi wa jengo na pia utunzaji mzuri wa samani ndani ya jengo hilo na hivyo kuonesha thamani halisi ya kuthamini jitihada zinazofanywa na Mahakama katika kuboresha mazingira ya watumishi wake kufanya kazi.
“Kwa sasa kitengo cha Uboreshaji wa Huduma za Mahakama ‘JDU’ tumekuwa na mtu wetu wenyewe ambaye ni Mhandisi wa Ujenzi ambaye atasaidia sana kuhakikisha kuwa majengo yetu yanakidhi ubora tofauti na hapo awali ambapo Watendaji ndio walikuwa wakikagua majengo na vifaa vya ujenzi kazi ambayo hawana utaalam nayo, na kwa kuanzia huyu Mhandisi wetu ataanzia mwanza hapa kuja kukagua suala zima la umeme na kdhalika,” aliongeza Prof. Ole Gabriel.
Zoezi zima la uchimbaji wa kisima hicho chenye mita 180 na ufungaji wa pampu na vifaa mbalimbali limegharimu kiasi cha fedha za Kitanzania milioni 90 hivyo, kitasaidia kuondoa adha ya ukosefu wa maji iliyokuwa ikiwakabili watumiaji wote wa jengo na muda mwingine kulazimu baadhi ya vyoo kufungwa na kutokutumika.
Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante Ole Gabriel akifanya zoezi zima la ufungaji wa pampu ya kusukuma maji toka katika kisima kwa ajili ya matumizi ndani ya jengo la Kito Jumuishi cha Utoaji Haki-Mwanza. Zoezi hilo limefanyika jana tarehe 19 Oktoba, 2022.
Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante Ole Gabriel (aliyesimama mstari wa mbele katikati) akiwa katika picha ya pamoja na watumishi wa jengo la kituo Jumuishi Mwanza, kulia kwake ni Mtendaji wa Mahakama Kuu Kanda ya Mwanza, Bw. Tutubi Mangazini
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...