Na Mwandishi Wetu , Michuzi Tv
MFUKO wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) wamepewa hati ya ubia wa uwekezaji kwenye Benki ya Biashara na Maendeleo (TDB) kwa hisa ambazo wamenunua kwenye benki hiyo.
Akizungumza wakati wa kukabidhiwa kwa hati hiyo ,Mkurugenzi Mkuu wa NSSF Masha Mshomba amesema ni siku muhimu kwa mfuko wao wa NSSF kwa sababu wanashuhudia wakipewa hati ya ubia kwa hisa ambazo walizonunua kutoka benki ya TDB ambayo imekuwa ikifanya vizuri hasa miaka mitano iliyopita.
“Uwekezaji wa hisa katika benki ya TDB unafikia dola za Marekani milioni 11 na ambao unatupa hisa 800 ni moja ya uwekezaji mzuri kabisa ambao NSSF umekuwa ukifanya katika siku za karibuni. Lakini yote hii inakwenda sambamba na lengo la kuhakikisha uwekezaji tunaofanya unatoa mapato mazuri.
“Mwenyekiti wetu wa bodi umekuwa ukishuhudia ambavyo tumekuwa tukifanya juhudi kubadilisha mazingira ya uwekezaji wetu ili tuweze mapato makubwa ambayo yatalinda thamani ya mfuko na kufanya wanachama kuwa na amani na hatimaye kulipwa kile ambacho wanastahili kutoka katika mfuko,”amesema.
Ameongeza lakini sio tu kwenye uwekezaji huo pia bali mfuko uwe imara na kuhisi nafasi yao hasa katika kuwalipa wanachama wao mafao.
“Uwekezaji huu ni mzuri kwasababu benki ya TDB imekuwa ikifanya vizuri na kwa sasa ina mali zinazokaribia kufikia dola bilioni nane , ni fedha nyingi na kwasababu ya uwezo wake ndio maana katika ukanda huu wa Afrika Mashariki hasa wenzetu wa NSSF Uganda , NSSF Rwanda walishachangamkia fursa hii muda mwingi uliopita
“Na sisi tukasema hatujachelewa tunaanza na pengine kwa nguvu yetu tutawafikia na kuwapita, hayo ni matumaini yetu na kwa uwekezaji kama huu tufanya vizuri sio kama mfuko lakini pia kama nchi, “amesema Mshomba .
Amesisitiza NSSF katika eneo la pafomansi wameendelea kuwa vizuri sana kwani katika mwaka uliopita mfuko ulifikia thamani ya Sh.trilioni 6.2 lakini kabla ya hapo Juni mwaka 2021 walikuwa na Sh.trilioni 5.1 wakati Juni 2020 walikuwa na Sh. Trilioni 4.35.
“Sasa kukua huku ambako ni kwa kasi kunasababishwa na uongozi mzuri wa bodi ya wakurugenzi , pia mazingira mazuri ya biashara pamoja na jitihada za watumishi na menejimenti kwa ujumla .
“Katika hili la mazingira mazuri ya biashara tunapongeza kazi nzuri iliyofanywa na Rais Samia Suluhu Hassan tangu aingie madarakani kwa kubadilisha kabisa mazingira ya biashara nchi na hatimaye kuvutia wawekezaji wengi , filamu yake ya Royal Tour imechangia sana kwenye jambo hili.
“Tunaipongeza Serikali kwa hatua inazochukua kwani hivi sasa tunaweza kwenda kuwekeza hata kwenye nchi nyingine ambazo ziko ukanda wa Afrika Mashariki kitu ambacho hakikuwepo huko nyuma.”
Amefafanua kutokana na mabadiliko hayo mfuko utaendelea kukua na manufaa yatakayopatikana hayataishia kwenye mfuko tu bali na nchi kwa ujumla.“Tunahakika wimbi hili la uwekezaji ambalo ni kubwa litafanya kipato chetu kama taifa kuongeza.
“Na hatimaye tutaondoa hata umasikini kwa Watanzania.Pia itasababisha kufikia malengo ya dunia 17 na mojawapo ni kuondoa umasikini wa watanzania na kuboresha afya na tayari kuna dalili za kufanya hivyo zipo kwani tayari tuna muswada wa bima ya afya kwa wote.”
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini ya NSSF Balozi Ali Idi Siwa amewapongeza NSSF kwa wazo hilo kwani ni hatua ya kuruka kufikia lengo mapema zaidi na bodi itawasadia katika kila hatua ili kufikia malengo ya kitaifa.
Aidha wakati wa hafla hiyo imeelezwa
Serikali kupitia Benki Kuu iliboresha muongozo wa uwekezaji katika mfuko wa hifadhi ya jamii nchini mwaka 2021 na kuruhusu mifuko kuwekeza katika masoko mbalimbali kwenye nchi wanachama wa Jjumuiya ya Afrika Mashariki.
Hivyo kwenye kuzingatia hilo mfuko huo ulifanya upembuzi na ulipata kibali cha kuwekeza, kwenye benki ya biashara na maendeleo(TDB) na kukamilisha kununua asilimia 0.64 za hisa za daraja B Septemba 2022.
Aidha TDB zamani iliyokuwa ikujulikana kama PTA yenye makao makuu yake nchini Mauritius na Burundi ni taasisi ya kifedha ya kimataifa yenye msingi wa mikataba yenye kinga na kipaumbele kama vile benki ya maendeleo ya Afrika (AFDB) na kundi la Benki ya Dunia.
Benki hiyo ina jumla ya nchi wanachama 22 barani Afrika na taasisi za kimataifa zikiwemo AFDB ,Benki ya Watu wa China, Benki ya Maendeleo ya Belarusi .Aidha kuna taasisi kutoka nchi wanachama kama mifuko ya hifadhi yajamii kama vile mifuko ya taifa ya hifadhi ya jamii Uganda(NSSF-Uganda)na Baraza la la Hifadhi ya Jamii Rwanda(RSSB)
Serikali ya Tanzania ni miongoni mwa nchi wanahisa wa TDB ambayo kwa sasa inamiliki asilimia 6.03 ya hisa za daraja A. Aidha kutokana na kuwa nchi wanachama, Benki imewezesha miradi minane (8)hapa nchini yenye thamani ya takriban dola za marekani milioni 580.00(sawa na Sh.trilioni 1.3).


Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini ya NSSF Balozi Ali Idi Siwa akiwapongeza NSSF kwa wazo hilo la kununua Hisa za Uwekezaji katika benki ya TDB na kueleza kuwa ni hatua ya kuruka kufikia lengo mapema zaidi na kwamba bodi itawasadia katika kila hatua ili kufikia malengo ya kitaifa. Hafla ya makabidhiano ya hati miliki ya umiliki wa hisa katika benki ya Biashara na Maendeleo kwa mfuko wa NSSF,imefanyika jijini Dar es Salaam.







Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...