Na Peter Stephen, Morogoro
Timu za Netiboli za Tamisemi Queens na JKT Mbweni
zinatarajia kumenyana leo katika mchezo mkali na wa kusisimua
wa Ligi ya Muungano utakaochezwa katika uwanja wa Jamhuri
mjini Morogoro.
Mchezo huo ni miongoni mwa michezo minne itakayochezwa leo
katika mfululizo wa mechi za ligi ya Muungano ambayo
inashirikisha timu tano za kutoka Tanzania Bara na timu tano
kutoka Zanzibar.
Kwa mujibu wa ratiba iliyotolewa jana na wasimamizi wa ligi
hiyo, mchezo huo umepangwa kuchezwa saa 10 jioni katika
uwanja wa Jamhuri na unatarajia kuwa mkali na wa kusisimua
kwani katika siku za hivi karibuni, timu hizo zimekuwa
zikionyeshana upinzani mkali.
Wakati Tamisemi Queens ikijivunia mastaa kama Sophia,
Komba, Mersiana Samwel, Lilian Jovin, na Gloria Benjamin
waliopo timu ya Taifa, nao JKT Mbweni wana wachezaji
wazoefu wa ligi hiyo na inaongozwa na Kocha Hafidhi Tindwa
ambaye pia ndiye Mwalimu wa timu ya Taifa ya Netiboli.
Akizungumza mbele ya Naibu Waziri, Ofisi ya Rais Tamisemi
anayeshughulikia Afya Dkt. Festo Dugange, ambaye alifika jana
mjini Morogoro kufunga michezo ya Shimisemita, Nahodha wa
Tamisemi Queens, Dafrosa Luhwago aliahidi kushinda mechi
hiyo na michezo mingine yote iliyobaki ili kuiwezesha timu yake
kulitetea kombe la ligi ya Muungano.
“Hadi sasa timu yetu imecheza michezo mitano, na
tumeshinda yote, hivyo tuna kila sababu ya kulitetea kombe
letu,” alijigamba Dafrosa.
Naye, Naibu Waziri Dkt. Dugange aliwataka wachezaji hao
kushinda michezo iliyobaki ili warudi na kombe la ubingwa, na
pia aliwapa salamu za Waziri wa Nchi, Mhe.Angela Kairuki za
kuwataka wachezaji hao wahakikishe kuwa wanatetea na
kulinda heshima ya Tamisemi katika michezo hiyo.
Mapema jana ilichezwa michezo minne ya ligi hiyo ambapo timu
ya Nyika Queens kutoka mkoani Pwani ilikubali kipigo kutoka
kwa timu ya Tamisemi Queens kwa magoli 56-32, JKT Mbweni
iliifunga Mafunzo ya Zanzibar magoli 26-24, na KVZ iliichapa
JKU magoli 47-42.
Bingwa wa Netiboli wa Ligi hiyo ya Muungano anatarajiwa
kupatikana tarehe 3 novemba, 2022 katika uwanja wa Jamhuri
kwa mchezo baina ya Tamisemi Queens na KVZ ya Zanzibar.
Mchezaji Lilian Sylidion (GA) wa Tamisemi Queens akitafuta mbinu ya jinsi ya kumfikia mchezaji mwenzake Lilian Jovin (GS) ambaye amezongwa na wachezaji wa nyuma wa timu ya Nyika Queens katika mojawapo ya patashika zilizotokea katika goli la Nyika Queens, katika moja ya michezo minne iliyochezwa jana ambapo Tamisemi ilishinda mchezo huo kwa magoli 56-32
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...