Benki ya Taifa ya Biashara (NBC) ambae ni mdhamini Mkuu wa Ligi Kuu ya Soka ya Tanzania Bara, NBC Premiere League imesisitiza kuhusu dhamira yake ya kuboresha zaidi ligi hiyo kwa kuendelea kuziwezesha timu zinazoshiriki ligi hiyo ili ziweze kujenga uwezo wa kujitegemea.

Dhamira hiyo imesisitizwa na Mkurugenzi wa Fedha wa benki hiyo Bw Waziri Barnabas mapema jana wakati akizungumza na washiriki wa Mkutano Mkuu wa kawaida wa 17 wa Shirikisho la Mpira wa Miguu nchini (TFF) uliofanyika jijini Mwanza.

“Kimsingi ni kwamba sisi kama wadhamini wa ligi hii tunajivunia sana kuona ligi yenye ushindani na viwango bora vya kiuchezaji vinavyoendelea kuonekana kwenye ligi hii. Hii inatokana na timu zinazoshiriki ligi hii kuweza kusajili na wachezaji wazuri kutoka ndani na nje ya nchi sambamba na kuweza kuwahudumia vema wachezaji hao ikiwemo kuwapatia maslahi yao.’’ alisema

Kwa mujibu wa Bw Waziri, mbali na udhamini wa ligi hiyo benki hiyo imebuni mikakati mbalimbali inayolenga kufanikisha dhamira hiyo muhimu ikiwemo mikopo ya mabasi kwa vilabu mbalimbali vinavyoshiriki ligi hiyo ili kurahisha usafiri kwa vilabu hivyo.

“Ligi hii inahusisha suala zima la usafiri kwa vilabu husika na wakati mwingine timu zinasafiri kwa umbali mrefu sana na hivyo kusababisha uchovu kwa wachezaji. Upatikanaji wa mabasi mazuri ya kisasa utasaidia kupunguza uchovu kwa wacheza ili waweze kuleta ushindani unaohitajika wakiwa viwanjani. Tupo kwenye hatua nzuri na hivi karibuni baadhi ya timu zitapatiwa mabasi yao,’’ alisema.

Zaidi Bw Waziri alitaja huduma nyingine kuwa ni pamoja na utoaji wa Bima kwa wachezaji, benchi za ufundi na familia za wachezaji wote wa ligi hii ya NBC Premier League.

“Tunaamini kuwa Bima hizi ambazo tunazitoa kupitia kampuni washirika za Britam na Sanlam, zimekuwa chachu kubwa kwa kuwaondolea wachezaji hofu za kucheza kwa woga wakihofia kupata majeraha yanayoweza kuathiri ajira zao. Hili limechochea sana wachezaji wetu kuonyesha viwango vyao.’’ Alisema.

Aidha Bw Waziri aliwaomba wadau hao wamichezo vikiwemo vilabu, viongozi wa mchezo huo na wachezaji mmoja mmoja kuhakikisha wanachangamkia fursa ya kuwekeza kwenye Hati Fungani ya NBC Twiga Bond ili waweze kunufaika na faida mbalimbali zitokazo na Hati fungani hiyo.

“Kiasi cha chini cha ununuzi wa hati fungani hiyo ni TZS 500,000. Kupitia uwekezaji huu wahusika wataweza kupata riba kubwa ya 10% kwa mwaka, inayolipwa nusu mwaka katika kipindi chote cha miaka mitano hadi Novemba 2027. Kiwango cha riba kinacholipwa hakina punguzo la kodi. Hivyo nawakaribisha sana wadau wa michezo’’ Alisema.


Mkurugenzi wa Fedha wa benki ya NBC Bw Waziri Barnabas akizungumza na washiriki wa Mkutano Mkuu wa kawaida wa 17 wa Shirikisho la Mpira wa Miguu nchini (TFF) uliofanyika jijini Mwanza hii leo. Alisisitiza kuhusu dhamira yake ya benki hiyo kuboresha zaidi ligi hiyo kwa kuendelea kuziwezesha timu zinazoshiriki ligi hiyo ili ziweze kujenga uwezo wa kujitegemea.



Mkurugenzi wa Fedha wa benki ya NBC Bw Waziri Barnabas (wa tatu kulia) akiwa kwenye picha ya pamoja na viongozi waandamizi wa mchezo wa soka nchini akiwemo Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu nchini (TFF) Bw Wallace Karia wakati wa Mkutano Mkuu wa kawaida wa 17 wa Shirikisho hilo uliofanyika jijini Mwanza hii leo.





Baadhi ya washiriki wa Mkutano Mkuu wa kawaida wa 17 wa Shirikisho la Mpira wa Miguu nchini (TFF) uliofanyika jijini Mwanza hii leo wakijadili mada mbalimbali wakati wa mkutano huo.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...