Na Mwandishi Wetu
Walimu,wazazi na watendaji wa serikai wametakiwa kushirikiana na Taasisi, Jamii na wadau wa maendeleo katika kutokomeza ukatili wa kijinsia kwa watoto.
Hayo yamesemwa na Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia Wanawake na Makundi Maalumu Dkt Dorothy Gwajima alipotembelea miradi ya kimaendeleo na uwezeshaji wa wanawake kiuchumi inayofanywa na Taasisi ya BRAC Maendeleo Tanzania leo Jijini Dar es Salaam.
Dkt Gwajima amesema, anaipongeza kwa mara nyingine tena taasisi ya Brac Tanzania kwa juhudi kubwa wanazozifanya katika kuandaa programu mbalimbali za kimaendeleo ikiwemo malezi na makuzi kwa watoto ambapo inawasadia kuwaandaa kwa ajili ya kuingia shule za awali.
Amesema, juhudi hizo zinazofanywa na taasisi hiyo ni somo kwa taasisi zingine ambapo zinawasaidia katika kuwalinda watoto wasifanyiwe ukatili wa kijinsia pindi wazazi wao wanapokuwa wameenda kwenye shughuli za kiuchumi.
“Najua Brac mmefanya mambo mengi katika jamii hii ila programu hii ya malezi na makuzi kwa watoto ambao mnawachukua kuanzia miaka mitatu inawasaidia katika kuwalinda na ukatili wa kijinsia na hili linatakiwa liangaliwe kwa jicho pana zaidi sababu hata sisi serikali tunashukuru kwa mnavyojitolea,”amesema
Dkt Gwajima ameongeza kuwa, katika takwimu zinaonesha watoto wengi wanaofanyiwa ukatili wa kijinsia asilimia 40 inaonesha ni mashuleni, sasa ni wakati wa walimu kushirikiana na wazazi kuhakikisha wanatoa elimu ya pamoja kwa watoto na kutokuogopa kusema pindi wanapofanyiwa ukatili.
Mbali na hilo, ameagiza kwa maafisa wa ustawi wa jamii kuacha kukaa maofisini bali wanatakiwa waingie mitaani na kutoa elimu kwa ngazi za chini juu ya masuala mazima ya ukatili wa kijinsia ili kutokomeza kabisa.
Dkt Gwajima ameipongeza pia taasisi hiyo kwa kuwawezesha wanawake kiuchumi ambapo wanatoa huduma ya mikopo kwa wanawake wajasiriamali wadogo na wa kati kwani ni suala la kimaendeleo na kuwasihi wakina mama kutumia fursa zilizopo kujiinua kiuchumi na kujiunga na majukwaa ya uwezeshaji wanawake kiuchumi.
Kwa upande wa Mkurugenzi Wa Brac Tanzania Suzane Bipa amesema Brac inatimiza miaka 50 kimataifa ila kwa Tanzania ina miaka 15 na wameweza kutoa huduma mbalimbali za kimaendeleo kwa wananachi sambamba na utoaji wa uwezeshaji wanawake kupitia mikopo ya vikundi.
Bipa amesema, wana vituo zaidi ya 110 vya malezi na makuzi kwa watoto wadogo ambapo vinatoa muongozo kwa watoto kabla ya kwenda shule za awali pia wanatoa huduma ya uwezeshaji wanawake katika mikoa 25 nchini.
Ameongezea kuwa, wataendelea kushirikiana na serikali katika mambo mbalimbali ya kimaendeleo na kijamii.
Brac inafikia kilele cha miaka 50 kesho ambapo hafla hiyo itahudhuriwa na watu mbalimbali ikiwemo viongozo wakubwa wa serikali na wadau wa maendeleo nchini.
Waziri wa Maendeleo ya Jamii,Jinsia, Wanawake na Makundi Maalumu Dkt Dorothy Gwajima akiwa katika picha ya pamoja na wanakikundi cha wajasiriamali cha Chemsha bongo cha Mvuleni Tandale kata ya Manzese.
Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalumu Dkt Dorothy Gwajima akizungumza na baadhi ya wakina mama waliojiunga katika vikundi na kupatiwa uwezeshwaji wa kiuchumi na Taasisi ya Brac kupitia mikopo midogo midogo ya Wajasiriamali na kuwataka Wanawake hao kuwa mstari wa mbele kutokomeza Ukatili wa Kijinsia kwa watoto
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...