Na Mwandishi Maalum – Dar es Salaam
TAASISI ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) imesaini mkataba na chuo Kikuu cha Jagiellonian kilichopo nchini Poland kwa ajili ya kushirikiana katika kubadilishana ujuzi wa kutoa huduma za kibingwa za matibabu na upasuaji wa moyo.
Mkataba huo ambao utaanza kutumika mapema mwakani ulisainiwa jana jijini Dar es Salaam na Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Peter Kisenge na Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Jagiellonian cha nchini Poland Prof. Bartlomiej Guzik.
Akizungumza na waandishi wa habari hizi Dkt. Kisenge alisema JKCI imesaini mkataba na chuo hicho ili kuweka ushirikiano ambao umelenga kuongeza wigo katika kutoa tiba ya magonjwa ya moyo pamoja na upasuaji wa moyo katika Taasisi hiyo.
“Tumesaini makubaliano ambayo yatawawezesha wataalam wetu kwenda nchini Poland kwa ajili ya kujifunza namna wenzetu wanavyotoa huduma za matibabu ya moyo lakini wao pia watakuja hapa kwetu kuona na kujifunza jinsi tunavyotoa huduma za tiba na upasuaji wa moyo”,
“katika ushirikiano huu pia tumekubaliana wenzetu hawa watatuletea wataalam ambao watashirikiana nasi katika kuwahudumia wagonjwa kwa kufanya matibabu ya kibingwa ya upasuaji wa moyo hasa kuzibua mishipa ya damu ambayo imeziba, kubadilisha valvu za moyo bila kupasua kifua upasuaji unaoitwa TAVI procedure ambao kwa hapa nchini kwetu bado haujaanza kufanyika”, alisema Dkt. Kisenge
Dkt. Kisenge alisema JKCI imeongeza wigo wa kuwa na ushirikiano na mashirika yanayotoa huduma za kibingwa za matibabu ya moyo kutoka nchi 18 ikiwemo nchi hiyo ya Poland ambayo itaanza rasmi kubadilishana ujuzi na wataalam wa Taasisi hiyo mapema mwakani.
“Tutaendelea kuongeza ushirikiano huu wa kubadilishana uzoefu na nchi nyingine ambazo tunaamini zinatoa huduma za kibingwa za matibabu ya moyo nia ikiwa ni kuifanya JKCI kutoa matibabu ya kibingwa ya magonjwa ya moyo katika Afrika yote”, alisema Dkt. Kisenge
Naye Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Jagiellonian kilichopo nchini Poland Prof. Bartlomiej Guzik alisema wamevutiwa kufanya kazi na wataalam wa afya wa JKCI ili kwa pamoja waweze kutoa huduma za kibingwa za matibabu na upasuaji wa moyo kwa wagonjwa wanaohitaji huduma hiyo.
“Kujenga uhusiano baina yetu na JKCI kutasaidia kuboresha huduma za kibingwa za matibabu na upasuaji wa moyo lakini pia kutaongeza ubobezi kwa wataalam hawa wa afya”, alisema Prof. Bartlomiej.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...