Na. Damian Kunambi, Njombe.
Hatimaye wakazi wa kata ya Lifuma iliyopo katika tarafa ya mwambao wilayani Ludewa mkoani Njombe sambamba na kata za jirani zinatarajia kuandika historia mpya ya kufikiwa na vyombo vya moto baada ya maeneo hayo kutofikiwa na vyombo hivyo tangu kuumbwa kwa dunia.
Hatua hii inaenda kufikiwa baada ya mradi wa ujenzi wa barabara inayo unganisha kata ya Lifuma pamoja na kata ya Luana ijulikanayo kama barabara ya Mbwila - Lifuma yenye urefu wa km. 18 kuendelea kushika kasi kitu ambacho kimeleta hamasa kwa wavuvi na wakulima wa naeneo hayo kwa kuongeza kiwango cha uzalishaji mali ikiwemo mazao ya biashara.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti wakazi hao wamesema kuwa barabara hiyo ni mkombozi kwao kwani itawawezesha kubadilishana bidhaa kwa upande wa ziwani na milimani huku mmoja wa wakulima wa zao la vitunguu, maharage na mahindi Magreth Haule akisema kuwa kwa sasa mazao yao watauzia shambani kwani wateja wataweza kufika na magari yao mashambani .
Joseph Kamonga ni mbunge wa jimbo la Ludewa amesema wananchi wa kata hizo walimuomba awafikishie ombi lao la fedha za kutengeneza barabara hiyo pindi aingiapo madarakani na alipopata ridhaa ya kuwaongoza akaona ni vyema kutimiza ahadi hiyo kwa kusajili barabara hiyo TARURA na kuiombea fedha za awamu ya kwanza kiasi cha sh. Ml. 100, na sasa wameongezewa tena kiasi cha sh. Ml. 200 ambazo bado zinaendelea kufanyiwa kazi.
Ameongeza kuwa sanjari na maombi ya fedha ya barabara hiyo lakini pia aliiomba serikali kuikomboa tarafa ya mwambao kwa kupeleka barabara ili magari na pikipiki ziweze kufika kwani wakazi wengi wa maeneo ya vijiji hivyo hawajawahi kuona vyombo hivyo vikifika maeneo hayo tangu kuzaliwa kwao hadi wanakufa.
"Tuna kila sababu ya kuishukuru serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan kwani kuna barabara nyinginezo ambazo nazo zinaunganisha kata za mwambao nazo tayari zimekwisha kupata fedha kama barabara ya Mawengi hadi Makonde ambayo mpaka sasa imepewa kiasi cha sh. Bil 1.6 ambazo zitatumika kujenga barabara hiyo kwa ubora na kuondoa vikwazo vyote vya milima na babonde ili magari yaweze kufika ziwani", Amesema Kamonga.
Naye katibu wa siasa na uenezi wilaya ya Ludewa Josaya Luoga amesema chama cha mapinduzi kipo kazini katika kutatua changamoto za wananchi, ikiwa ni utekelezaji wa ilani ya chama hicho huku mhandisi wa TARURA wilaya ya Ludewa James Gowele akisema kwa sasa tayari wamekwisha kamilisha km. 6 kati ya 18 za barabara hiyo na itahusisha uwekaji madaraja kwa haraka ili kuzuia uharibifu wa mvua.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...