Waziri wa Viwanda na Biashara Dkt. Ashatu Kijaji akizungumza wakati wa kikao hicho.
 Balozi wa Umoja wa Ulaya nchini Tanzania Mh. Manfredo Fanti (Kushoto,) akizungumza wakati wa kikao hicho.
 
WAZIRI wa Uwekezaji, Viwanda na Biashara Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji (Mb) amesema kuwa Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan imedhamiria kutekeleza kwa vitendo Mpango wa Kuboresha Mazingira ya Biashara (MKUMBI) ili kuvutia wawekezaji nchini.

Mhe. Kijaji ameyasema hayo tarehe 17 Novemba, 2022 alipokutana na kufanya mazungumzo na Balozi wa Umoja wa Ulaya Nchini Tanzania Mhe. Manfredo Fanti aliyeambatana na ujumbe wake.

Mhe. Dkt. Kijaji amemshukuru Mhe. balozi Fanti kwa ushirikiano endelevu uliopo baina ya Tanzania na Umoja wa Ulaya katika utekelezaji wa miradi mbalimbali na kumhakikishia kuwa Tanzania itaendelea kuboresha Mazingira ya Biashara kupitia MKUMBI ambapo sheria na kanuni mbalimbali zimeboreshwa ama kufutwa ili kurahisisha ufanyaji Biashara Nchini Tanzania.

“Mazingira ya kufanya Biashara yameboreka zaidi kwani hivi karibuni tunaenda kuzindua mfumo wa dirisha moja la huduma kwa wawekezaji wa Ndani na Nje ya Nchi ili kurahisisha upatikanaji wa huduma mbalimbali ikiwemo maombi ya leseni, vibali, hati na kurahisisha malipo ndani ya muda mfupi. Amesema Dkt. Kijaji.

Balozi wa Umoja wa Ulaya Nchini Tanzania Mhe. Manfredo Fanti amesema kuwa Mazingira ya Biashara Nchini Tanzania yamezidi kuboreka siku hadi siku na Nchi za Umoja wa Ulaya zimedhamiria kuja kuwekeza Tanzania katika sekta mbalimbali.

Mhe. Balozi Fanti ameongeza kuwa kutokana na Tanzania kuanzisha na kutekeleza MKUMBI, Mpango huo utaenda kuchapishwa katika tovuti ya Umoja wa Ulaya na kupitia Kongamano la Uwekezaji linaloenda kufanyika Mwezi Februari 2023 litawaunganisha wafanyabiashara wa Nchi za Umoja wa Ulaya na Tanzania na utapelekea kuongezeka kwa uwekezaji baina ya Nchi hizi mbili.


 

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...