MAMLAKA ya Kudhibiti Ununuzi wa Umma (PPRA) imesema maafisa maendeleo ya jamii ndilo daraja muhimu kwa makundi maalum ambayo ni wanawake, vijana, wazee na watu wenye ulemavu kupata fursa za zabuni za umma zilizotengwa kwa ajili yao.

Hayo yameelezwa na Afisa Mtendaji Mkuu wa PPRA, Bw. Eliakim Maswi alipokuwa anazungumza na Wakuu wa Vitengo na Idara za Maendeleo ya Jamii, Mamlaka za Serikali za Mitaa ngazi ya Mkoa waliokutana kwenye kikao kazi hivi karibuni jijini Dodoma.

Bw. Maswi aliwaambia maafisa hao kuwa baada PPRA kufanya kampeni maalum ya kuhamasisha ushiriki wa makundi maalum kwenye zabuni za umma kwenye mikoa saba nchini, imebaini kuwa hatua ya usajili wa makundi maalum ambayo ni jukumu la maafisa maendeleo ya jamii ni muhimu katika kufanikisha azma ya Serikali.

Hata hivyo, Afisa Mtendaji Mkuu huyo alieleza kuwa kupitia kampeni hiyo iliyofanyika katika mikoa ya Rukwa, Tabora, Mwanza, Dodoma, Arusha, Mtwara na Manyara wamebaini kuwa maafisa maendeleo ya jamii wengi hawakuwa na uelewa kuhusu uwepo wa fursa hizi hali iliyosababisha kuwa na vikwazo na urasimu katika baadhi ya Halmashauri, hatua ambayo inafifisha juhudi za Serikali katika kuwawezesha wananchi kupitia makundi maalum.

“Uzoefu tuliopata kupitia kampeni ya elimu kwa umma kuhusu hizi fursa za makundi maalum, ambapo mwaka huu wa fedha kuna zaidi ya Shilingi trilioni tisa (9,000,000,000/=) zilizotengwa kwa ajili ya haya makundi maalum, tumebaini kulikuwa na vikwazo na urasimu ambao unakwamisha usajili,” alisema Bw. Maswi na kuwataka maafisa hao kuboresha utendaji wao wa kazi katika eneo hilo.

Aliongeza kuwa anatarajia kuwa endapo wataboresha utendaji wao katika usajili wa vikundi, kutakuwa na ongezeko la vikundi nchini vitakavyoorodheshwa na PPRA kwa ajili ya fursa hizo, kwani hadi sasa kuna vikundi 195 tu nchi nzima vilivyoorodheshwa, idadi ambayo haiendani na uhitaji na ukubwa wa nchi.

Aliwataka maafisa hao kuiga mfano wa wakuu wa mikoa, makatibu tawala wa mikoa na viongozi wengine katika mikoa waliyotembelea ambao walionesha ushirikiano mzuri katika kufanikisha kampeni hiyo ambayo itaongeza fursa za ajira na kusaidia kuboresha maisha ya wananchi kupitia ununuzi wa umma.

“Kwa pamoja, kwa kushirikiana na Wizara inayohusika na vikundi maalum, tunaweza kupata suluhu na kuweka mazingira rafiki zaidi ya kusajili vikundi. Natoa wito kwenu, kila mmoja akifanya kazi yake ipasavyo itawezesha haya makundi maalum kupata sehemu ya Sh.9 trilioni iliyotengwa na Serikali kwa ajili yao kwa mwaka huu,” amesema Bw. Maswi.

Sheria ya Ununuzi wa Umma Sura ya 410 inaitaka kila taasisi nunuzi kutenga asilimia 30 ya bajeti yake ya mwaka ya ununuzi wa umma kwa ajili ya makundi maalum ambayo ni vijana, wanawake, wazee na watu wenye ulemavu.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...