Na Humphrey Shao, Michuzi Tv
RAIS Samia Suluhu Hassan ametoa maagizo matatu yatakayosaidia kumaliza tatizo la uhaba wa maji Jijijini Dar es Salaam, ikiwemo kufuatilia vizuizi vya mto Ruvu, kudhibiti watu wanaofanya shughuli za kibinadamu na kwa ujenzi wa bwawa la Kidunda.
Ametoa maagizo hayo jana katika mjadala wa nishati safi ya kupikia, ambapo aliagiza Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira (DAWASA), Mkoa wa Dar es Salaam na Mkoa wa Pwani kufanya operesheni ya pamoja kuwaondoa watu wote wanaofanya shughuli zao.
Rais
Samia alisema tatizo la mgawo wa maji linaloendelea linalotokana na
mabadiliko ya hali ya hewa na tabia nchini ambayo imesababisha kupungua
kwa maji Mto Ruvu kutokana na shughuli za binadamu.
“Hili linatokana na matendo yetu yenyewe, watu wanalima hadi wanaweka vizuizi na kuharibu 'flow' ya maji kwenye mto. Matokeo yake vyanzo vya maji vinakauka na maji hayaendi,” alisema.
Pia, alisema pamoja na uharibifu huo kuna tatizo la ukataji miti kiholela kwa matumizi ya nishati ya kupikia huku wengine wakijenga karibu na mto mabwawa samaki na kufunga pampu kubwa kwa ajili ya kilimo cha umwagiliaji.
“Dawasa, Mkuu wa Mkoa Pwani (Aboubakar Kunenge na wa Dar es Salaam Amos Makalla mhakikishe vizuizi vya mto Ruvu vimeondoka,” aliagiza Rais Samia.
Aliongeza, “Naomba mkazunguke sijui mtatumia helkopta, miguu au magari yenu kasafisheni mto, flow iende watu wapate maji safi na salama,”.
Alisema atamuagiza Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ahakikishe lita milioni 70 za maji kutoka Kigamboni zinaingia mkoani Dar es Saaam.
Aidha, alisema Dar es Salaam miundombinu yake ni mikongwe huenda ilijengwa wakati mkoa huo ukiwa na wakazi milioni tatu lakini kwa sasa wako milioni tano.
“Naomba hili nalo liangaliwe maana kwa kasi tuliyonayo Jiji hili hadi ifikapo mwakani litakuwa na maji kwa asilimia 100. Sasa lazima yawafikie wananchi ipasavyo,” alisema.
Pia, suala la ujenzi holela lisimamiwe ili iwe rahisi kupitisha miundombinu ya maji.
Alisema tatizo la maji mkoani Dar es Salaam litakuwa historia kupitia mradi wa ujenzi wa bwawa la Kidunda ambalo tayari mkataba wake umeshasainiwa na serikali imeshatenga fedha za utekelezaji wake.
“Ujenzi wa bwawa ni miaka miwili lakini baada ya miaka mine mpaka sita mbele Dar es Salaam itakuwa na maji ya kutosha nay a ziada,” alisema.
Awali, Makalla alizungumzia suala hilo la uhaba wa maji na kubainisha kuwa mitambo ya maji ya Kigamboni yenye visima 12 vyenye lita za maji milioni 70 imeshawashwa tangu juzi usiku.
Alisema tatizo hilo la uhaba wa maji linatokana na kudra za mwenyezi Mungu kutokana na tatizo la ukame lililopo.
Hivyo alisema “Rais uliagiza ili kuondokana na tatizo la maji mkataba wa bwawa la Kidunda utekelezwe na tayari jana (juzi) umesainiwa. Naomba wakazi wa Dar es Salaam kuendelea kuwa watulivu wakati serikali ikiendelea kutatia tatizo hilo,.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...