Na Khadija Seif,Michuzi Tv.
RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,Samia Suluhu Hassan, ametaja mikakati mitatu mikubwa itakayotekelezwa haraka na serikali ya awamu ya sita kuhakikisha ndani ya miaka 10 kuanzia sasa nchi iweze kufikia asilimia 80 hadi 90 ya uwepo wa nishati safi na endelevu ya kupikia ifikapo 2032.
Akizungumza
jana katika ufunguzi wa mjadala wa nishati safi ya kupikia uliofanyika
ukumbi wa kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere nchini, Rais Samia alisema
mjadala huo ni muhimu kwa mustakabali wa taifa.
Amesema miongoni mwa mikakati hiyo ni pamoja na kuunda kikosi kazi, kutengwa kwa fedha mwaka ujao wa bajeti ya Wizara ya Nishati na kuanzishwa kwa Mfuko wa Nishati Safi na jambo la tatu taasisi zote za serikali zenye kuhudumia watu zaidi ya 300 zianze kutumia nishati mbadala ikiwemo gesi na kuachana na mtumizi ya kuni au mkaa.
Amesema
nishati safi ya kupikia ni mjadala mpana, unaopaswa kuja na mawazo ya
pamoja kwa kuwa suala hilo linaibua changamoto nyingi kwa jamii na ni
lazima kama serikali ianze kuchukua hatua sasa.
''Japo
tumejipa miaka 10 lakini hatupaswi kusubiri huko katika kutafuta
ufumbuzi wa uwepo wa nishati safi ya kupikia. Naelekeza sasa suala hili
tunalokwenda nalo si suala la muda mrefu bali ni suala la muda fupi na
ni lazima tuanze sasa na kwa kasi kubwa.'' anasema.
Kwa
mujibu wa Rais Samia, kuundwe haraka kwa kikosi kazi kitakachojumuisha
sekta binafsi na wadau wa maendeleo ili kupatikane kwa mawazo ya pamoja
na sio kila mtu anakuwa na mipango yake.
''Natambua
suala la nishati safi ya kupikia ni jambo linalounganisha taasisi
mbalimbali ikiwemo Wizara mbalimbali kama Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera,
Uratibu na Bunge, Wizara ya Nishati, TAMISEMI, Maendeleo ya Jamii sasa
nadhani sekta binafsi inapaswa kuwepo na wadau wa maendeleo'' amesema.
Amesema
malengo na mategemeo yake ni kuhakikisha ndani ya miaka 10 aweze kumtua
kuni mama kichwani na hilo anaamini litafanikiwa kama alivyofanikiwa
katika sekta ya maji, ambapo zaidi ya asilimia 80 wananchi wanapata
majisafi na salama.
''Kikosi hiki kiongozwe na
Waziri Mkuu na kwa ngazi ya makatibu wakuu kiongozwe na Wizara ya
Nishati. Lazima twende na nishati safi ya kupikia kwa maendeleo ya nchi
na wanawake kwa ujumla'' amesema.
Pia, Rais
Samia alisema kikubwa kinachotakiwa kwa sasa ni kuwa na mawazo ya pamoja
na kubadilisha mtazamo wa wananchi kutoka katika matumizi ya kuni na
mkaa na kwenda katika nishati safi na endelevu.
''Nina
matumaini makubwa kikosi kazi cha taifa kitakuja maoni bora ili
serikali iweze kuja na sera na mkakati wa pamoja wa nchi kuwa na nishati
safi ya kupikia na ndio maana nataka kiunganishwe na sekta binafsi
pamoja na wadau wa maendeleo'' anasema.
Mkakati
wa pili, Rais Samia alisema katika bajeti ijayo ya fedha kwa Wizara ya
Nishati kutakuwa na ongezeko la fedha kwa ajili ya kuanzishwa kwa Mfuko
wa Nishati Safi ili kuleta mafanikio makubwa.
''Serikali
pekee haiweze lazima kuwa na ushirikiano wa pamoja. Hivyo
tutashirikiana ili kuwe na sera na mpango makakati mzuri, hivyo
kuanzishwa kwa kikosi kazi litasiadia sana katika mipango ya serikali
katika suala hili hususan katika ongezeko la bajeti''alisema.
Pia,
alisema mkakati wa tatu ni kuzitaka taasisi zote za kiserikali ikiwemo
shule, vyombo vya ulinzi na usalama, magereza kutumia nishati safi ya
kupikia na kuchana na matumizi ya kuni na mkaa.
Amesema
kuwezekana kwa mambo hayo, anamatumaini hadi ifikapo 2032 itasaidia
kuwa na nishati safi na endelevu ya kupikia, ambapo aliagiza Wizara ya
Nishati kuanza sasa na wasisubiri hadi ifikapo 2032.
Katika
mjadala huo, Rais Samia alivutiwa na mijadala mbalimbali iliyokuwa
inatolewa ikiwemo mwanasiasa maarufu nchini, Profesa Anna Tibaijuka,
Daktari bingwa wa magonjwa ya kupumua, Dk. Pauline Chale na wataalamu
wengine na kusema ni mjadala wenye mawazo bora na ya kujenga.
Alisema
amesikia suala la bei kuwa nafuu huku wengine wakidai mkaa ni bei
rahisi kuliko gesi, lakini bei wengine wamedai kuwa gharama rahisi ya
mkaa ni mbaya zaidi kutokana na madhara anayoyapata mwananchi.
''Suala
hili ni jambo pana na linahitaji mawazo ya pamoja na sio serikali
pekee. Lengo ni kuhakikisha suala linakuwa afforadabilty na pia kubadili
mtazamo wa wananchi juu ya masuala haya'' alisema.
Rais
Samia alisema anaipongeza Wizara ya Nishati kwa mjadala huu, umekuja
wakati mwafaka ambao sasa duniani inahamisisha matumizi ya nishati safi
na salama kama sehemu ya kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi na
nishati safi na kuachana na kuni na mkaa.
''Nawapongeza
wote mlioshiriki. Nawapongeza mkutano huu ulipaswa kuwa zaidi ya elfu
100 lakini sasa kuna watu elfu 300, naelewa kumbi zetu haziwezi kuchukua
watu wengi. Wawekezaji sasa changamkeni hii fursa kuhakikisha mnakuwa
na kumbi zenu'' amesema.
Rais
Samia alisema ukataji wa miti ni suala ambalo linaharibu mazingira na
ripoti iliopo mikoa vinara ya ukataji miti iko Pwani, Morogoro, Tabora,
Lindi na Ruvuma, ambapo misiti na miti.
''Pwani
inaongoza kwa ukataji miti sana ndio chanzo cha uhaba wa maji ndani ya
Jiji la Dar es Salaam na hili naagiza wakuu wa mikoa ya Pwani, Dar es
Salaam na Dawasa kukaa pamoja na Waziri Mkuu kuhakikisha wanaondoa watu
wote wanaofanya shughuli zao katika vyanzo vya maji'' alisema.
Aliongeza
''Miti ina umuhimu mkubwa, watoto wanashindwa kufanya shughuli zao
nyumbani kutokana na kutumia nguvu kubwa kukata kuni, utafutaji wa kuni
unaleta vitendo vya ukatili wa kijinsia ikiwemo kubakwa na kuchelewa
kupigwa.''
Pia, alisema sasa ni wakati wa
kubadilisha mtazamo wa watu wa upandaji miti na kila mkoa waanze
mikakati ya kuangalia ni miti gani inamea zaidi hususan ya matunda na
hilo aliwahi kutoa maagizo kwa kila mkoa kupanda miti milioni 1.5.
Rais
Samia alisema nishati ya kupikia italeta suluhu ya mambo mengi katika
jamii kwa kuwa ni suala linalopaswa kupewa kipaumbele katika miaka
mitano mbele, ambapo sasa ni kubadilisha mitazamo ya watu kutoka hapa na
kwenda mbele kwa kupata utatuzi wa jambo hilo.
Alisema
ni lazima twende na nishati safi ya kupikia kwa maendeleo ya nchi,
maendeleo ya jamii zetu na kukinga haki za wanawake. Wanawake wanafanya
kazi nyingi kwa kujitolea bila malipo, kina mama wanasonga ugali na
machozi yanamtoka lakini na wengine hata watoto wenyewe hawawatunzi.
Kwa
upande wake, Waziri wa Nishati, January Makamba alisema wamejipanga
kutumia mjadala huo kuja na mawazo mbadala ili kusaidia upatikanaji wa
nishati safi ya kupikia kwa kuwa suala hilo kila mtu analitumia.
Alisema
kupika ni moja ya tukio pekee linalounganisha watu wa hali zote wa juu,
kati na chini na jambo muhimu kwa kila mtanzania, Watanzania wengi
hawajui na wala hawahoji aina ya nishati inayotumika katika kupika
vyakula vinaliwa kila siku”.
Waziri Makamba
alisema matumizi ya nishati ya tunayotumia kupikia yanahusishwa na
madhara mbalimbali ya afya ikiwemo magonjwa ya mfumo wa upumuaji,
uharibifu wa mimba na vifo vya watoto wachanga.
''Takriban
watu 33,000 hupoteza maisha kila mwaka nchini Tanzania kutokana na
magonjwa yanayotokana na nishati chafu za kupikia zinazotumiwa majumbani
ikiwemo kuni na mkaa. Wanawake na watoto ndio waathirika wakubwa wa
janga hili'' alisema.
Hivyo, alisema Wizara
imeona kufanyike kwa mjadala wa kitaifa utakaofanyika katika Ukumbi wa
Mwalimu Nyerere, jijini Dar es Salaam ili kuweka mikakati ya kisera,
kiuchumi na kuwezesha upatikanaji wa nishati safi ya kupikia kama njia
ya kulinda afya za wanawake.
Rais wa Jamhuri wa Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, Akitoa maelekezo kwa Waziri wa Nishati.
EWaziri wa Nishati, January Makamba akizungumza wakati wa kufungua mjadala juu ya Masuala ya Nishati Safi ya Kupikia.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...