Na Khadija Kalili
TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Pwani itawachukulia hatua baadhi ya watu wanaosimamia miradi ya maendeleo ambayo imeonekana kuwa na mapungufu na kuisababishia serikali kukosa mapato.
Yamesemwa hayo leo Novemba 15, 2022 na Kamanda wa TAKUKURU Mkoa wa Pwani Christopher Myava alipozingumza na Waandishi wa Habari Ofisini kwake Kibaha mkoani Pwani amesema taarifa hii ni kwa mujibu wa ripoti ya kipindi cha robo mwaka Julai hadi Septemba mwaka huu, amesema kuwa Takukuru imefuatilia miradi 26 yenye thamani ya shilingi Bil. 5.7 na kuikuta baadhi ikiwa na mapungufu.
Kamanda Myava amesema kuwa kuwa uchunguzi unaendelea kwenye miradi hiyo na wahusika wakibainika watachukuliwa hatua kali kwa mujibu wa sheria.
Ameitaja baadhi ya miradi iliyofuatiliwa kuwa ni kwenye sekta za Elimu, Afya, Maji, Barabara, Ardhi na Maendeleo ya jamii.
Aidha ameweka wazi kuwa mikakati waliyojiwekea TAKUKURU katika kipindi cha miezi mitatu ijayo kuwa ni kufanya ufuatiliaji na uchambuzi wa mifumo ili kuziba mianya ya rushwa itakayobainika.
Kamanda Myava amesema kuwa bila rushwa maendeleo yatapatikana na huduma za jamii zitakuwa bora na zitapatikana kirahisi na kupunguza kero kwa wananchi.
Amesema kuwa kwa kushirikiana na vyombo vingine vya Ulinzi na Usalama imebainika uwepo wa vifaa vya ujenzi visivyo na ubora katika ujenzi wa shule ya sekondari mpya Jibondo iliyopo Wilayani Mafia, ambapo matofali 6,000 hayakukidhi viwango baada ya upimaji wa kitaalam kufanyika hivyo mzabuni aliagizwa kutoyatumia na kunyang'anywa kazi hiyo na akapewa mzabuni Mwingine.
Aidha Kamanda Myava amesema kuwa jumla ya malalamiko 98 yaliyopokelewa kati ya hayo 42 yalihusu rushwa na majalada mapya ya uchunguzi yamefunguliwa na uchunguzi ukikamilika hatua kali za kisheria zitachukuliwa. Malalamiko 56 hayakuhusu rushwa, katika malalamiko hayo yasiyohusu rushwa 25 walalamikaji walishauriwa, malalamiko 11 yalihamishiwa taasisi nyingine na malalamiko 20 yalifungwa baada ya walalamikaji kupata suluhu ya malalamiko yao.
Aidha mashauri mengine 13 mapya yalifunguliwa Mahakamani hivyo kufanya mashauri 29 kuendelea Mahakamani na hakuna shauri lililoamriwa. Amewashukuru wanchi wa Mkoa wa Pwani huku akiwataka kuendelea kuunga mkono juhudi za Taasisi hiyo katika mapambano dhidi ya rushwa.
"Nawasihi wananchi wa Pwani kuendelea kusimamia miradi ya maendeleo inayoendelea katika maeneo yenu ili kuzuia vitendo viovu vya rushwa katika utekelezaji wa miradi hiyo na kwa wale wanaoendekeza vitendo vya rushwa ninawaambia TAKUKURU Mkoa wa Pwani haina uvumilivu kwa wala rushwa hivyo basi tushirikiane katika kutokomeza vitendo vya rushwa" amesema Kamanda Myava.
Kamanda Mkuu wa TAKUKURU Mkoa wa Pwani Christopher Myava akizungumza na waandishi wa Habari hawapo pichani Ofisini kwake leo Kibaha.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...