Na. Catherine Sungura, WAF-Dodoma
Tanzania ni miongoni mwa nchi 5 kati ya 17 za awamu ya kwanza barani Afrika zitakazotekeleza mradi wa kuwajengea uwezo wa sekta ya afya kujiandaa, kugundua na kukabiliana na dharura na majanga. Wataalamu wa sekta ya mbalimbali wanaoshirikiana na sekta ya afya katika kukabiliana na dharura na majanga wameshiriki.
Mradi umepanga kuendeleza kutumia mifumo na juhudi zilizopo na kuboresha zaidi. Hii itahusisha ushirikiano na sekta mbalimbali katika kufikia utayari wa kukabiliana na matukio ya dharura na majanga.
Hayo yamebainishwa leo na Waziri wa Afya Mhe. Ummy Mwalimu wakati wa kufungua mkutano kujadili namna bora ya utekelezaji wa mradi huo. Mkutano umewajumuisha wataalamu kutoka sekta mbalimbali nchini unaofanyika jijini Dodoma.
Waziri Ummy amesema kuwa katika mradi huo unaojulikana kama “Flagship Initiative” utaisaidia nchi kuwa na mfumo sahihi wa kukabiliana na dharura na majanga kwa kuimarisha mpango kazi wa uwezo wa kujiandaa, kugundua na kukabiliana na dharura na majanga pamoja na kujizatiti katika kuimarisha mipango yao.
“Tunashukuru kwamba tunakuwa kati ya nchi tano (5) za Afrika ambazo zitaanza kufaidika kutekeleza Mradi huu, tunaamini tutafanikiwa kujengewa uwezo wetu wa kuandaa, kugundua na kukabiliana na dharura za afya kwa jamii na kuwezesha kujenga miundombinu iliyopo na kuweka mifumo sahihi itakayosaidia kuongeza uwezo wa Kitaifa katika kujiandaa kukabiliana na dharura na maafa”.
Waziri ummy ameongeza kuwa hivi sasa nchi imekua ikikumbwa na majanga mbalimbali pamoja na dharura na wakati mwingine wanapata changamoto kwa kukosa mfumo imara wa afya wa kukabiliana na changamoto hizo.
Akitolea mfano wakati wa janga la UVIKO-19 amesema kuwa wamejifunza kwa kuimarisha mfumo wa dharura ikiwemo huduma za hewa ya Oksjeni na hatua hiyo imefanya sekta ya afya kufunga mifumo ya hewa tiba kuanzia hospitali ya taifa, kanda, hospitali za Rufaa za Mikoam rufaa pamoja na baadhi ya hospitali za Halmashauri.
“Janga la UVIKO-19 pia imetufundisha kufanya kazi kwa pamoja kwa kushirikiana na sekta mbalimbali na hivyo tuliweza kuratibu kama sekta na sasa tunaangalia mbele katika utayari wa kukabiliana na maafa na majanga nchini” Alisisitiza Waziri Ummy.
Aidha, Waziri Ummy amesema Magonjwa mengi ya milipuko yanayowapata binadamu yanatoka kwa wanyama kwa hivyo ushirikiano wa sekta mbalimbali ni muhimu katika kujitayarisha kukabiliana na magonjwa ya milipuko kwani hata mabadiliko ya tabia nchi nayo yanachangia pia kuibuka kwa magonjwa yanayoathiri afya ya jamii.
Amesema utekelezaji wa mradi huo unalenga kwa pamoja kuboresha uwezo wa nchi wanachama kujiandaa, kugundua na kukabiliana na magonjwa ya milipuko yanayoathiri afya ya jamii na hivyo ameishukuru WHO Afrika kwa mafunzo ya kuwajengea uwezo wataalamu wa sekata mbalimbali hapa nchini.
“Mafunzo haya yamekuja wakati sahihi na itatusaidia kuangalia utayari wetu na tunaishukuru WHO kwa kuendelea kusapoti Serikali hususani katika utayari wa kukabiliana na dharura na majanga nchini, na kuhakikisha nchi yetu inaendelea kuwa salama, tunaahidi ushirikiano katika kutekeleza mradi huu kwa kushirikiana na sekta nyingine”.
Akiongea katika mkutano huo Mwakilishi Mkazi wa Shirika la Afya duniani nchini Tanzania (WHO ) Dkt. Zabron Yoti amesema asilimia 70 ya magonjwa ya milipuko yanayowapata binadamu yanatoka kwa wanyama hivyo usalama wa afya ni kipaumbele cha dunia na kama nchi inahitaji kujengewa uelewa kwa kushirikisha sekta zote.
Amesema ni vyema kuwalinda wananchi na dharura na majanga kwani mabadiliko ya tabia nchi nayo huchangia magonjwa ya milipuko.
“Ni vyema kujiandaa mapema kwani kutojiandaa ni hatari na hivyo kama WHO wapo tayari kushirikiana na Serikali katika kukabiliana na magonjwa ya milipuko yakiwemo yanayotokana na wanyama.
Naye, Kaimu Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya Bw. Edward Mbanga amewashukuru WHO kuwa washirikia wazuri wa kuisadia serikali ya Tanzania kwani hivi sasa tunaishi dunia yenye dharura hivyo hatuwezi kuzuia yasitokee ila ni vyema kujiweka tayari katika kukabiliana nayo.
Nchi nyingine zitakazotekeleza mradi huo ni Botswana, Mauritania, Niger,Nigeria,Togo,Chad,Congo, DRC pamoja na nyinginezo
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...