Mamlaka ya Usimamizi wa
Wanyamapori Tanzania (TAWA) imekutana na kufanya kikao kazi na Maafisa
Ikolojia na Ujirani mwema kutoka Kanda za Uhifadhi zinazoisamamia.
Kikao
kazi hicho kimefanyika leo Novemba 16, 2022 katika Wilaya ya Kilombero,
Mkoani Morogoro kwa lengo la kuwapatia mafunzo Maafisa hao ili waweze
kuongeza ufanisi katika utekelezaji wa majukumu yao.
Akizungumza
katika ufunguzi wa kikao kazi hicho, Kamishna Msaidizi Mwandamizi
anayehusika na shughuli za tafiti, ikolojia na ujirani mwema, Gloria
Bideberi amesema "kikao kazi hiki kimelenga kufahamu majukumu yenu kwa
ufasaha na kuweka mpango mkakati wa utekelezaji wa shughuli za utoaji wa
elimu kwa jamii na ufuatiliaji wa mifumo ikolojia katika kanda
tunazosimamia"
Vilevile mafunzo haya yanalenga kuhakikisha
wananchi wanaoishi pembezoni na maeneo ya hifadhi wanapatiwa elimu zaidi
juu ya umuhimu wa shughuli za uhifadhi na jinsi ya kujilinda na
wanyamapori wakali na waharibifu.
Kamishna Bideberi ameongeza
kuwa sambamba na mafunzo hayo, TAWA itafanya ziara ya utoaji elimu na
kufanya tathmini ya kiikolojia katika vijiji vinavyoizunguka Pori
Tengefu Kilombero.
"Kikubwa ni kuhakikisha rasilimali maji na
wanyamapori waliopo katika Pori Tengefu Kilombero yanatuzwa vyema ili
tuweze kupata maji ya kutosha yatakayotosheleza kwenye uzalishaji wa
umeme katika Bwawa la Nyerere na kuhakikisha mifumo ikolojia inafanya
kazi vizuri" amesema Kamishna Bideberi.
Naye, Kamishna Msaidizi
wa Uhifadhi, Nyanda za Juu Kusini Japhary Lyimo ameongeza kuwa utoaji wa
elimu utakaofanyika baada ya kikao kazi hiki katika vijiji
vinavyoizunguka Pori Tengefu Kilombero ni matokeo ya utekelezaji wa
Maazimio tisa (9) ya Kikao Kazi cha Mkuu wa Mkoa wa Morogoro na wadau wa
Uhifadhi wa Bonde la Kilombero kilichofanyika Julai 8, 2022, katika
Wilaya ya Kilombero. Maazimio hayo yalilenga kutatua changamoto
zinazolikabili Bonde la Mto Kilombero na kuweka makubaliano ya pamoja na
wadau wa uhifadhi katika utatuzi wa changamoto hizo.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...