Na Immaculate Makilika – MAELEZO, Dar

Shirika la Utangazaji la Taifa (TBC) limeendelea kufanya jitihada mbalimbali ili kuhakikisha kuwa Watanzania wanapata haki ya kupata habari kwa kufikisha usikivu wa redio zake nchi nzima.

Hayo yameelezwa na Naibu Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhandisi Kundo Mathew wakati wa ufunguzi wa Mkutano wa Baraza la Wafanyakazi wa TBC leo jijini Dar es salaam.

“TBC imekuwa na mikakati ya kuhakikisha kuwa usikivu unafika nchi nzima hususani maeneo ya pembezoni ya nchi yetu, hakikisheni mnajadili mipango na mikakati itakayowezesha usikivu wa redio za TBC kuwafikia wananchi wote”. Ameeleza Naibu Waziri Kundo.

Aidha, ametaja maeneo mengine ambayo TBC inatakiwa kujadili ili kuongeza usikivu kuwa na watumishi wenye weledi, kuwa na mitambo na vifaa vya kisasa, mazingira bora ya kufanyia kazi, mikakati ya kuongeza mapato ya Shirika, kuandaa vipindi vyenye ubunifu, na kuwa na habari zinazovutia wakigusa nyanja mbalimbali na makundi yote katika jamii.

“Ninawapongeza Bodi, Menejimenti na wafanyakazi wote wa TBC kwa maendeleo makubwa na maboresho mengi yaliyofanyika maeneo ya studio, vipindi vyenye ubunifu na maslahi ya wafanyakazi. TBC ni chombo cha Utangazaji cha Taifa, hakikisheni mnakuwa mbele muda wote katika kuleta furaha kwa watanzania kupitia vipindi na huduma zote mnazozitoa ili vyombo vingine vya habari viendelee kujifunza kupitia TBC” . Amebainisha Naibu Waziri huyo.

Katika hatua nyingine, Naibu Waziri Kundo amesema kuwa Wizara itahakikisha kuwa TBC inakuwa na uwezo wa kifedha na raslimali watu muda wote na kuwa Serikali imeendelea kuipatia TBC fedha za kutosha kwa ajili ya miradi ya maendeleo na matumizi mengineyo.

Fauka ya hayo, Naibu Waziri huyo ameipongeza TBC kwa ubunifu wa kuwa na Aridhio, Jambo Tanzania Mpya na Taarifa ya Habari ya Kiingereza yenye lengo la kueleza habari kwa mtazamo wa kiafrika, ambapo kupitia taarifa hiyo itasaidia kuifungua nchi kimataifa.


 

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...