Na. Josephine Majura WFM, Dar es Salaam
Naibu
Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Hamadi Hassan Chande, amewataka
wahitimu wa vyuo mbalimbali nchini hususani Chuo Cha Usimamizi wa Fedha
(IFM), kufanya kazi kwa ubunifu, uaminifu na uadilifu na kujiepusha na
vitendo vya rushwa, ufisadi, wizi na matumizi ya madawa ya kulevya.
Rai
hiyo imetolewa, jijini Dar es Salaam wakati wa mahafali ya 48 ya Chuo
Cha Usimamizi wa Fedha katika Kampasi Kuu ya Dar es Salaam, ambapo zaidi
ya wahitimu 4,000 wametunukiwa tuzo mbalimbali
Alisema kuwa IFM
imekuwa mstari wa mbele katika kuongeza idadi ya watanzania wenye
taaluma na utaalamu katika Sekta ya Fedha, Uhasibu, Bima na Hifadhi za
Jamii hivyo ni vema idadi hiyo iendane na kukidhi mahitaji ya soko
ambayo yanahitaji wanataaluma wenye weledi na uadilifu.
Mhe.
Chande ameupongeza uongozi wa chuo hicho kwa kuzalisha wataalamu katika
fani mbalimbali na kuliwezesha Taifa kufikia malengo yake ya
kujitosheleza katika fani za fedha kwa ajili ya maendeleo ya kiuchumi,
kiteknolojia, kisiasa na kijamii.
Kwa upande wa Mikopo ya
wanafunzi wa elimu ya juu, Mhe. Chande, alisema Serikali ya Awamu ya
Sita chini ya Rais Mhe. Samia Suluhu Hassan itaendelea kuongeza kiwango
cha wanafunzi wanaopata mikopo mwaka hadi mwaka ili wanafunzi wenye sifa
waweze kunufaika.
Alisema jambo hilo litawezekana endapo wale
wote waliopata mkopo wa Serikali kwa ajili ya kuwasaidia kuweza kutimiza
ndoto zao watarejesha mikopo waliyopata kwa wakati hivyo kuiongezea
Serikali uwezo wa kutoa fursa za mikopo kwa wanafunzi wengi zaidi.
Katika
mahafali hayo Kaimu Mkuu wa Chuo Cha Usimamizi wa Fedha (IFM), Dkt.
Imanueli Mnzava, alisema Chuo kimeendelea kurahisisha upatikanaji wa
mafunzo kwa wananchi kwa kusogeza huduma za mafunzo hayo karibu na
wahitaji.
“Chuo kina kampasi Mwanza, Dodoma, Simiyu na sasa
tunamalizia ujenzi Kampasi ya Geita kwa ufadhili wa Serikali, kama
tunavyofahamu elimu ni chachu ya mabadiliko ya kitabia, kiutendaji na
uwezo wa kubadilisha mazingira yanayotuzunguka”, Alisema Dkt. Mnzava.
Aliongeza
kuwa licha ya mafanikio mbalimbali yaliyopatikana chuoni hapo, alieleza
kuwepo kwa uhaba wa madarasa, ofisi na mabweni ya wanafunzi hivyo
kuiomba Serikali isaidie kupata majengo yaliyo karibu na Chuo ili
kurahisisha utoaji wa elimu bora kulingana na mahitaji ya soko.
Kwa
upande wake, Mwenyekiti wa Baraza la Uongozi la Chuo, Prof. Emanuel
Mjema, alisema Baraza la Uongozi la Chuo litaendelea kusimamia
utekelezaji wa malengo ya Chuo na kuainisha vipaumbele kwa kuzingatia
misingi ya tija na upatikanaji rasilimali ili kuboresha viwango vya
wahitimu w2atakaoweza kujiajiri wenyewe na kujitegemea na pia kushindana
katika soko la ajira ndani na nje ya nchi.
Chuo cha Usimamizi wa
Fedha (IFM) kilianzishwa mwaka 1972 kikiwa na uwezo wa kutoa kozi
mbili, ambapo jumla ya wahitimu 59 walihitimu mwaka huo. Chuo hicho
kinatoa zaidi ya kozi 33 katika fani mbalimbali ikiwemo Fedha, Bima,
Uhasibu na nyinginezo ambapo hadi mwaka 2021 jumla ya wahitimu 39,723
walitihimu chuoni hapo katika kozi mbalimbali.
Naibu
Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Hamad Hassan Chande (Mb) akizungumza
jijini Dar es Salaam wakati wa mahafali ya 48 ya Chuo Cha Usimamizi wa
Fedha (IFM) ambapo aliwataka kufanya kazi kwa ubunifu, uaminifu na
uadilifu mahali popote.
Baadhi
ya wahitimu wakifuatilia hotuba ya Naibu Waziri wa Fedha na Mipango
Mhe. Hamad Hassan Chande (Mb), wakati wa mahafali ya 48 ya Chuo Cha
Usimamizi wa Fedha (IFM), jijini Dar es Salaam.(Picha na Kitengo cha
Mawasiliano Serikalini,WFM Dar es Salaam)
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...