Na Karama Kenyunko Michuzi TV
WIZARA ya Katiba na Sheria kwa kushirikiana na Taasisi za Serikali, Asasi za Kiraia na Washirika wa Maendeleo, imezindua kampeni ya huduma ya msaada wa kisheria ya iitwayo (Mama Samia Legal Aid Campaign) itakayosaidia wananchi kutambua kupata haki ni haki yao ya msingi.

Waziri wa Katiba na Sheria, Dkt. Damas Ndumbaro, amesema hayo leo Februari 15, 2023 jijini Dar es Salaam wakati wa uzinduzi wa kampeni hiyo itayofanyika katika kipindi cha miaka mitatu mfululizo kwenye mikoa ya Tanzania Bara na Zanzibar, huku ikilenga kugusa maeneo matano.

Amesema, kampeni hiyo italenga zaidi kwa watu wasiojiweza, wanawake na watoto ambao wamekuwa waathirika wakubwa wa kukosa haki zao za msingi.

Amesema lengo kubwa la kuanzishwa kwa kampeni hiyo ni Kuimarisha upatikanaji wa haki kwa Umma na utoaji wa msaada wa kisheria kuongeza uelewa wa kisheria na haki za binadamu kwa jamii hususan haki za wanawake na watoto,

"Vilevile, kampeni itahusisha masuala mengine muhimu yanayoigusa jamii katika mfumo mzima wa haki kama vile usimamizi wa mirathi na Urithi, sheria ya ardhi na haki ya kumiliki mali, utatuzi wa migogoro kwa njia mbadala, hususani kwa viongozi wa Serikali za Mitaaa, Watendaji wa Kata, Vijiji, na Wajumbe wa Mabaraza ya ardhi, Wazee wa kimila na Wazee maarufu, na Viongozi wa dini" amesema waziri Ndumbaro.

Ameongeza kuwa, kampeni hiyo itafika kila kijiji na mkakati hivyo kuifanya kampeni hiyo ya msaada wa kisheria kugusa maeneo mengi husasani sehemu ambazo hazijawahi kufikiwa na wataenda kuwagusa wanyonge ambao wamekuwa wakiachwa nyuma katika mikoa yote bara na Zanzibar.

Aidha Waziri Ndumbaro ametaja maeneo matano ambayo yatatekelezwa kupitia kampeni hiyo itakayomalizika Februari 2026, ikiwemo utoaji elimu ya haki za binadamu kwa wananchi.

“Eneo la kwanza ni kutoa elimu ya haki za binadamu, itakayoelezea kwa kina haki zilizotolewa kati ya Ibara ya 12 mpaka 30 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Ibara ya 12 hadi 25 ya Katiba ya Zanzibar. Miongoni mwa haki zitakazoelezwa ni haki ya kupata maji, umeme, mazingira, kushiriki shughuli za demokrasia na tunaamini wakielewa watazipambania haki zao,” amesema Dk. Ndumbaro.

Ametaja eneo la pili kuwa ni kampeni ya kupambana na vitendo vya ukatili wa kijinsia, huku la tatu ikiwa ni kushughulikia changamoto ya migogoro ya ardhi na mirathi.

Waziri Ndumbaro amesema eneo la nne ni elimu kwa umma kuhusu mifumo ya kisheria inavyofanya kazi.

“mifumo hii ni misingi mingine ambapo wananchi hawajui matatizo yao wayapeleke wapi. Mwananchi akiwa na tatizo la kisheria anapeleka kwenye majukwaa ambayo siyo ya kwake. Lazima wananchi wajue mifumo ya kisheria.”amesema.

Amelitaja eneo la mwisho kuwa ni kuwaelimisha wananchi juu ya utatuzi wa migogoro kwa njia ya Usuluhishi inayowakabili na kwamba siyo kila jambo ni la kukimbilia mahakamani na kufuatilia mifumo ya kisheria.

Amesema ili kutekeleza hayo yote Serikali itashirikiana na wadau mbalimbali ikiwemo asasi za kiraia ambao watajengewa uwezo katika kutekeleza jukumu hilo.

Pia Waziri Ndumbaro ametoa wito kwa wananchi na wadau kushirikiana na wizara katika kampeni hiyo kwa kutoa taarifa sahihi na kwa wakati ili kuhamasisha utii wa sheria, kutoa elimu sahihi kwa umma, kutoa unasihi kwa waathirika wa ukatili, kutoa ushirikiano kwa vyombo vya utoaji haki, kutoshiriki matukio ya uvunjifu wa sheria,kuwalinda watoto katika maeneo yote (nyumbani, shuleni, njiani, kwenye vyombo vya usafiri na kwa njia nyingine zitakazoonekana zinafaa.

Naye, Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Legal Services Facility (LSF), Lulu Ng’wanakilala, amesema taasisi yake itaendelea kushirikiana na Serikali kupitia Wizara ya Katiba na Sheria ili kuhakikisha kampeni hiyo inafanikiwa huku akimshukuru Rais Samia kwa kuipa nguvu.

“Tumekuwa wadau wakubwa sana wa Wizara ya Katiba na Sheria, sababu suala zima la upatikanaji haki na msaada wa kisheria ndiyo suala ambalo tunaishi kwa ajili hiyo na tunafurahi sana kwamba tumefanikiwa kuzindua kampeni hii ya msaada wa kisheria,” amesema Ng’wanakilala.

Katibu Mtendaji Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora, Patience Ntwina akizungumza wakati wa uzinduzi wa Kampeni ya Kitaifa ya Huduma ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia. Uzinduzi huo umefanyika leo Februari 15, 2023 jijini Dar es Salaam.
Waziri wa Katiba na Sheria Dkt. Damas Ndumbaro mwenye suti ya bluu, Naibu Waziri Wizara ya Katiba na Sheria  Geophrey Pinda mwenye suti nyeusi, Lulu Ngw'anakilala kutoka LSF wa kwanza kulia na, Mansura Kassim Katibu Mkuu Wizara ya Katiba, Sheria na Utawala Bora Zanzibar Zanzibar wameshata kitabu cha muongozo wa  Kampeni ya Kitaifa ya Huduma ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia. Uzinduzi huo wa kampeni hiyo umefanyika leo Februari 15, 2023 jijini Dar es Salaam.


Waziri wa Katiba na Sheria Dkt. Damas Ndumbaro katika uzinduzi wa Kampeni ya Kitaifa ya Huduma ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia.


Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...