Waandaaji wa Kilimanjaro Premium Lager International Marathon wametangaza utaratibu wa uchukuaji namba na vesti za kukimbilia kwa waliojisajili.

Hatua hii inakuja baada ya waandaaji hao kutangaza kufungwa kwa usajili wa mbio hizo kwani nafasi zilishajaa kwa mbio za KM 42 na 21 kabla ya Februari 6, 2023 ambayo ilikuwa tarehe ya mwisho ya kujisajili.

Taarifa iliyotolewa na waandaaji hao imesema kuwa zoezi hilo litaanzia Jijini Dar es Salaam Jumamosi Februari 18 na 19 mwaka huu katika viwanja vya Mlimani City kuanzia saa sita mchana hadi saa kumi na mbili jioni.

Baada ya Dar es Salaam, zoezi hilo litahamia Arusha katika hoteli ya Kibo Palace Februari  21 na 22 kuanzia saa nane mchana hadi saa moja jioni.

Kituo cha mwisho ni Moshi Mjini ambapo zoezi hilo litafanyika Februari 23 (saa sita mchana hadi saa kumi na moja jioni), Februari 24 (kuanzia saa nne asubuhi hadi saa kumi na mbili jioni) na Februari 25 (kuanzia saa tatu asubuhi hadi saa kumi na moja jioni) katika uwanja wa Chuo Kikuu Cha Ushirika Moshi (MoCU).

Waandaaji hao wametoa wito kwa washiriki kuzingatia muda katika kila kituo ili kuepusha usumbufu na pia walitoa wito kwa wanaowachukulia washiriki wengine namba zao wahakikishe wanaenda na nakala ya kitambulisho au barua kutoka kwa mshiriki halisi.

“Ni matumaini yetu kuwa washiriki watajitokeza kwa wingi Jijini Dar es Salaam na Arusha ili kupunguza msongamano Mjini Moshi,” imesema sehemu ya taarifa ya waandaaji hao.

Waandaaji hao pia wamesisitiza kuhusu hatua zitakazochukuliwa dhidi ya watu wanaodaiwa kuuza tiketi mtandaoni kwa njia isiyo halali. “Wau hawa watachukuliwa hatua za kisheria kwa sababu ni marufuku kuuza tiketi bila idhini ya waandaaji na hata hivyo usajili umeshafungwa,” imesema taarifa hiyo.

Watakaokimbia na namba feki zikiwemo za miaka iliyopita pia watachukuliwa hatua ikiwemo kuondolewa mashindanoni, kufutiwa matokeo na pia kufungiwa kushiriki katika Kilimanjaro Marathon kabisa.

Wadhamini wa mbio hii ni pamoja na Kilimanjaro Premium Lager-42km (Mdhamini Mkuu), Tigo- 21km Half Marathon, Grand Malt – 5Km Fun Run, wadhamini wa meza za majiTPC Sugar, Simba Cement, Kilimanjaro Water, TotalEnergies na wasambazaji maalumu Kibo Palace Hotel, CMC Automobiles, KK Security na Keys Hotel.


Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...