NA FARIDA MANGUBE,MOROGORO

Wakulima wa zao la Mpunga katika Kijiji cha Mkindo Wilaya ya Mvomero mkoani Morogoro wamefanikiwa kuzalisha mpunga ambao mchele wake umekubalika katika soko la kimataifa, matokeo ambayo yamechagizwa na utumiaji wa zana bora za kilimo pamoja na kuzingatia kanuni za kitaalam za kilimo cha zao hilo.

Adam Omary ni miongoni mwa wakulima 151 wa zao la mpunga katika skimu ya umwagiliaji Kijiji cha Mkindo yenye ukubwa wa hekta 200, amesema, pamoja na kukabiliwa na changamoto mbalimbali katika kilimo hicho ikiwemo miundombinu mibovu ya skimu hiyo na uhaba wa vifaa vya kupandia na kuvunia wamefanikiwa kuzalisha mpunga ambao mchele wake umekubalika katika masoko.

Amesema tangu waanzishe kikundi chao na kujiunga na Kampuni ya Kilimo ya Syngenta kupitia mradi wa MAP ambao waliwapatia mafunzo na kanuni bora, ndiyo yamewazesha kuzalisha kwa mara ya kwanza mpunga wenye kiwango kinachokubalika pamoja na kuongeza kiwango cha uzalishaji kutoka gunia 7-10 hadi kufikia wastani wa gunia 25-30 kwa hekari moja.

Ofisa Kilimo wa Mradi wa MAP Tanzania Jackson Mayingu amesema mradi huu ulilenga kumwezesha mkulima kulima kilimo bora, malengo ambayo wamefanikiwa kuyafikia baada ya kupeleka sampuli ya mpunga maabara na majibu kuonyesha kuwa mchele wake umekidhi viwango vya kuwa mchele Grade One.

Amesema mbali na skimu hiyo ya Mkindo, wamelenga kuwafikia wakulma zaidi ya 500 kwa mkoa wa Morogoro katika Halmashauri za Wilaya Kilosa, Mvomero. Kilombero na Ifakara ambapo tayari wameshaanza mashamba darasa ya kuwanoa wakulima wa zao la mpunga.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji Kampuni ya Syngenta Tanzania Edwin Zacharia amesema maoja ya malengo yao makubwa ni kuwaelimisha wakulima kupitia mashamba darasa kuanzia hatua ya kuandaa shamba hadi mavuno pamoja na uchaguzi sahihi wa aina za viuatilifu.

Amesema kwa kuzingatia hayo, ndiko kumewazesha wakulima hao kupiga hatua kwenye kiwango cha uzalishaji, Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania ikiwa ni moja ya Taasisi iliyoridhia ubora wa mpunga huo, wakati kiwanda cha MW Rice Millers ambao huchakata mpunga na kusambaza mchele katika Nchi za Indonesia, China, India na Malaysia nao wakithibitisha ubora wake.

Mkuu wa Wilaya ya Mvomero Judith Nguli akiwa katika ziara yake ya kwanza wilayani humo, amefika katika skimu ya kilimo cha Umwagiliaji Mkindo kuzungumza na wakulima katika skimu hiyo, ambapo amewapongeza kwa namna walivyothubutu kujikita katika kilimo.

Amesema kuwa serikali imedhamiria kumkomboa mkulima kwa kuhakikisha inafanya jitihada za makusudi katika kuboresha miundombinu ya umwagiliaji katika skimu mbalimbali kwa kuzitengea bajeti ya shilingi bilioni 5.6.

Aidha Mkuu huyo wa Wilaya, aliagiza Idara ya Kilimo wialayani humo kushirikiana kwa karibu na wadu wa kilimo kuwawezesha wakulima wanapata mbolea za ruzuku na zinawafikia kwa urahisi na haraka kwenye maeneo yao huku akiwasisitiza wakulima kutunza miundombinu iliyopo kwa kuwa imetumia gharama kubwa.


Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...