Na Karama Kenyunko Michuzi TV
MSHITAKIWA Sarah Joseph anayekabiliwa na kesi ya kusafirisha dawa za kulevya pamoja na mmiliki wa Kituo cha michezo cha Cambiasso, Kambi Zuber na wenzake wanne ameuomba upande wa Jamuhuri kuharakisha upelelezi wa kesi hiyo ili kujua hatma yake kwani mpaka sasa hajui watoto wake wanaishi mazingira gani uraiani.
Sarah ametoa ombi hilo wakati kesi hiyo ilipoitwa mahakamani hapo mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Mary Mrio kwa ajili ya kutajwa huku upande wa Jamuhuri ukiongozwa na Caroline MTemu ukidai upelelezi katika kesi hiyo bado haujakamilika .
"Nipo gerezani na sijui watoto wangu wako katika hali gani naomba upande Jamuhuri waharakishe upelelezi maana mpaka sasa hivi sijui muafaka wa kesi hii," amedai Sarah.
Baada ya kueleza hayo, Hakimu Mrio amemuuliza Sarah kama hana ndugu wanaokuja kumtembelea na kumjulisha hali za watoto na kumtaka kuwa mvumilivu.Hata hivyo mshtakiwa Sarah alidai ndugu wanaenda lakinj hajui mazingira wanayolelewa watoto wake.
Mbali na Sarah washtakiwa wengine katika kesi hiyo ni, aliyewahi kuwa Kocha wa makipa wa Klabu ya Simba Muharami Sultan, Maulid Zungu, Said mwantiko na John Andrew wote wakazi wa Dar es salaam.
katika kesi hiyo washitakiwa wanadaiwa Oktoba 27, mwaka huu maeneo ya Kivule wilayani Ilala Dar es Salaam walikutwa na dawa za kulevya aina ya Heroin zenye uzito wa kilogramu 27.10.
Pia Novemba 4, mwaka huu maeneo ya Kamegele Mkuranga mkoani Pwani, walikutwa na dawa hizo zenye uzito wa Kilogramu 7.79.Hakimu Mrio ameahirisha kesi hiyo hadi Machi 2,2023 kwa ajili ya kutajwa.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...