Na Karama Kenyunko, Michuzi TV

UPANDE wa mashtaka katika kesi inayomkabili Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya JATU Public limited Peter Gasayan Peter umeiomba  Mahakama kutupilia mbali ombi la kufanyia marekebisho masharti ya dhamana lililoombwa na upande wa utetezi kwa sababu Mahakama haiwezi kutengua amri iliyojiwekea yenyewe.

Wakili wa Serikali Caroline Matemu amewasilisha maombi hayo leo Februari 16, 2023 mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu Mary Mrio wakati kesi hiyo ya jinai ilipofikishwa Mahakamani kwa ajili upande wa mashtaka kujibu hoja za utetezi kutaka masharti ya dhamana yafanyiwe marekebisho kwani masharti yaliyowekwa ni makubwa sana.

Katika kesi hiyo, mshtakiwa Peter anakabiliwa na shtaka la  kujipatia fedha zaidi ya Sh. Bil. 5 kwa njia ya udanganyifu.

Awali upande wa utetezi katika kesi hiyo ukiongozwa na wakili Kung'he Wabeya aliiomba mahakama kupitia upya masharti ya dhamana iliyoyaweka awali na kumpa mteja wao masharti nafuu kwani masharti aliyopewa mteja wake ni makubwa na kwamba lengo la kutoa dhamana kwa kuweka kiasi cha fedha au bondi ni kuihakikishia Mahakama mshitakiwa anafika  mahakamani pale anapohitajika.

Kwa upande wake Wakili wa utetezi Nafikile Mwamboma ameiomba  Mahakama ipitie upya uamuzi wake kuhusu dhamana ya mshtakiwa na kabla mshtakiwa hajahukumiwa anahaki ya kupata dhamana kwa mujibu wa kifungu cha 13 (6) (b) na 15 (1,2) cha Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Pia Wakili Kambona katika maombi yao ameiomba Mahakama iangalie hadhi ya  mshtakiwa katika na kuweza hata kumpatia sharti nafuu ikiwemo kusaini bondi.

"Mshitakiwa alikuwa Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni ya umma , hivyo ni wazi mshitakiwa ni mtu anayefahamika na umma wa Tanzania, kwa hadhi yake alistahili kupata masharti nafuu ya dhamana, ni mtu anayeaminika kwa jamii,"amedai Wakili Kambona.

Akijibu hoja hizo, Wakili Matemu amedai Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu imefungwa mikono na haina mamlaka ya kupitia upya masharti ya dhamana ambayo imeyaweka yenyewe kwani kufanya hivyo ni kukiuka haki lakini kama hawaridhiki na masharti hayo waende mahakama Kuu.

Kutokana na hoja hizo, Hakimu Mrio ameahirisha kesi hiyo hadi Februari 27,2023 itakapofikishqa Mahakamani kwa ajili ya kutolewa maamuzi.

Kwa mujibu wa hati ya mashtaka inadaiwa kati ya Januari Mosi na  Desemba 31, 2021 mkoani  Dar es salaam mshtakiwa Peter alijipatia Sh. 5,139,865,733.00 kutoka  Saccos ya Jatu kwa madai kuwa angezalisha  kiasi hicho cha fedha kwa kuwekeza fedha katika kilimo cha faida wakati akijua  si kweli.





Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...