Na Mwandishi wetu, Simanjiro
MWENYEKITI wa Kijiji cha Komolo, Wilayani Simanjiro Mkoani Manyara, Saning’o Somii, ameishukuru Taasisi ya ECLAT Foundation, kwa kuahidi kukarabati shule ya msingi Komolo na kujenga madarasa mapya ya shule shikizi ya Olembole.
Somii akizungumza mbele ya Mwenyekiti wa Taasisi ya ECLAT Foundation Peter Toima, amesema wanashukuru hatua hiyo kwani itafanikisha maendeleo kwenye eneo lao la Komolo.
Amesema shule ya msingi Komolo ni kongwe hivyo hatua ya ukarabati utakaofanywa na ECLAT Foundation ni ya kupongezwa kwani wanafunzi watasoma kwa utulivu zaidi.
“Eneo la Olembole ni kubwa linazidi kuchangamka kwa watu kuongezeka hivyo ujenzi wa madarasa mapya ya shule hiyo shikizi utakaofanywa na ECLAT Foundation utasaidia mno,” amesema Somii.
Amesema kwa niaba ya wakazi wa eneo hilo hawana kitu cha kumlipa Toima ila watamkumbuka daima kwa ujenzi wa madarasa shule ya Olembole na ukarabati shule ya Komolo.
Diwani wa kata ya Komolo ambaye pia ni Mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya ya Simanjiro, Baraka Kanunga amesema Toima ni mwana maendeleo aliyefanya makubwa.
“Mzee Toima na shirika lake la ECLAT Foundation chini ya wajerumani wa shirika la Upendo wamefanikisha maendeleo mengi Simanjiro kwa kujenga shule katika kata mbalimbali,” amesema Kanunga.
Mdau wa maendeleo Swalehe Mpinga ambaye ni mchimbaji wa madini ya Tomarine amepongeza hatua hiyo kwani alifanikisha ujenzi wa darasa moja wa shule shikizi ya Olembole.
“Mimi kama mdau wa maendeleo wa eneo hili, baada ya kuelezwa changamoto ya madarasa, nilikutana na wenzangu tukakusanya shilingi milioni 20 na kujenga darasa,” amesema Mpinga.
Hata hivyo, Toima ambaye pia ni Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Manyara, amesema baada ya kuelezwa hitaji la ujenzi wa shule ya Olembole na ukarabati wa shule ya Komolo aliridhia mara moja.
“Tutakarabati shule kongwe ya msingi Komolo na ujenzi wa madarasa ya shule shikizi ya msingi Olembole, hivyo wakazi wa Komolo wakae mkao wa kula,” amesema Toima.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...