Serikali kwa kushirikiana na Washirika wa Maendeleo wamefanya majadiliano ya uboreshaji mazingira ya ufanyaji biashara na uwekezaji nchini illi kuwavutia wawekezaji.
Hayo yameelezwa na Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb), wakati akifungua Mkutano wa ngazi ya juu wa Majadiliano ya kimkakati kati ya Serikali na Washirika wa Maendeleo uliofanyika jijini Dar es Salaam.
Serikali imesema itaendelea kuwekeza nguvu kwenye maeneo yanayohitaji uwezeshwaji fedha kama vile kilimo, uvuvi na mifugo ili kukuza uchumi, ajira na maendeleo ya jamii.
Aidha, alisema Serikali itaendelea kuboresha mazingira ya uwekezaji ili kuvutia wawekezaji wengi zaidi na kutoa wito kwa wawekezaji wote kuja kuwekeza nchini na kutumia fursa zilizopo kupata faida yao na nchi kwa ujumla.
“Miaka kadhaa iliyopita kulikuwa na malalamiko ya wafanyabiashara kuhusu utitiri wa kodi, Rais Samia alipoingia madarakani alifuta tozo na kodi zaidi ya 114, katika sekta za uzalishaji,”, alisema Dkt. Nchemba.
Alisema moja ya hatua ambazo Serikali ya Awamu ya Sita pia imechukua ni kurekebisha sheria za kikodi na sheria za uwekezaji ili kuwepo na mazingira mazuri ya ufanyaji biashara nchini.
Dkt. Nchemba alisema kuwepo kwa ushirikiano kati ya Serikali na Washirika wa Maendeleo kumewezesha ufanisi wa utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo ambayo Washirika hao wa Maendeleo wamekuwa wakiifadhili.
“Tulisaini makubalinao kwenye ziara ya Rais Samia nchini China kuhusu samaki, parachichi, kwenye ziara yake ya Ulaya makubaliano yalisainiwa katika masuala ya nafaka ambapo mchele wa Tanzania unauzwa mpaka Ubelgiji, pia tulisaini na Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE) na nchi nyingine zinazotuzunguka,”alisema Dkt. Mwigulu.
Kuhusu uzalishaji katika kilimo, mifugo na uvuvi, alisema lengo la serikali ni kuhakikisha ifikapo mwaka 2030 mchango wa sekta hizo uwe umezidi asilimia 10 ili Pato la Taifa linapopanda na pato la mtu mmoja mmoja nalo lipande.
Alisema mpaka sasa vijana zaidi ya 27,000 wamejiandikisha kwa ajili ya kutaka kwenda kuwekeza kwenye mashamba maalumu ambayo serikali imepanga vijana wawekeze.
Naye, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Fedha na Mipango Zanzibar, Mhe. Dkt. Saada Salum Mkuya, alisema pamoja na mambo mengine mkutano huo umejadili mambo mbalimbali ikiwemo uwezeshwaji wa wanawake kiuchumi na namna bora ya kuboresha mazingira ya ufanyaji biashara na kuishirikisha Sekta Binafsi.
Dkt. Mkuya aliongeza kuwa katika majadiliano hayo walisistiza suala la utunzaji mazingira ambayo yatawezesha kufanya kilimo endelevu kwa ajili ya utunzaji mazingira na upatikanaji wa chakula.
Kwa upande wake Mwenyekiti Mwenza wa Washirika wa Maendeleo nchini, Mhe Balozi wa Uingereza David Concar, alisema washirika wa maendeleo wataendelea kushirikiana na Serikali ya Tanzania katika sekta mbalimbali ili kuhakikisha uchumi wan chi na wananchi unaongezeka.
Alisema washirika wa maendeleo pia wanaipongeza Serikali kwa kuwa na uongozi bora unao zingatia haki za binadamu pamoja na jitihada mbalimbali inazochukua kuboresha maendeleo ya kiuchumi na kijamii kwa kusimamia vizuri uchumi wa nchi.
Mkutano huo wa siku moja umewakutanisha Mawaziri, Mabalozi, Makatibu Wakuu, Washirika wa Maendeleo, Sekta Binafsi na Viongozi Mbalimbali wa Serikali.
Waziri
wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb), akiongoza
Mkutano wa Ngazi ya Juu wa Majadiliano ya Kimkakati kati ya Serikali na
Washirika wa Maendeleo, katika Ukumbi wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT),
Jijini Dar es Salaam. Kushoto ni Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Fedha na
Mipango-Zanzibar, Mhe. Dkt. Saada Salum Mkuya, wa pili kulia ni Balozi
wa Uingereza na Mwenyekiti Mwenza wa Mkutano huo, Mhe. David Concar, na
kulia ni Balozi wa Canada nchini Tanzania, Mhe. Kyle Nunas, aliyekuwa
akitoa mada.
Waziri
wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb) akizungumza
na vyombo vya habari baada ya kufungua Mkutano wa Ngazi ya Juu wa
Majadiliano ya Kimkakati kati ya Serikali na Washirika wa Maendeleo,
katika Ukumbi wa Benki Kuu ya Tanzania, Jijini Dar es Salaam
Waziri
wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb), akizungumza
na vyombo vya habari baada ya kufungua Mkutano wa Ngazi ya Juu wa
Majadiliano ya Kimkakati kati ya Serikali na Washirika wa Maendeleo,
katika Ukumbi wa Benki Kuu ya Tanzania, Jijini Dar es Salaam
Baadhi
ya Washiriki wa Mkutano wa Ngazi ya Juu wa Majadiliano ya Kimkakati
kati ya Serikali na Washirika wa Maendeleo, wakiwa katika picha ya
pamoja nje ya Ukumbi wa Mikutano wa Benki Kuu ya Tanzania, Jijini Dar es
Salaam, wakiongozwa na Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Mwigulu
Lameck Nchemba (Mb) (aliyeketi mbele-katikati)
Balozi wa Uingereza na
Mwenyekiti Mwenza wa Mkutano wa Ngazi ya Juu wa Majadiliano ya Kimkakati
kati ya Serikali na Washirika wa Maendeleo, Mhe. David Concar,
akifafanua mambo mbalimbali mbele ya wanahabari baada ya ufunguzi rasmi
wa Mkutano huo uliofanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Benki Kuu ya
Tanzania (BoT), Jijini Dar es Salaam
Baadhi
ya Wajumbe kutoka Jumuiya ya Kimataifa na Tanzania, wakifuatilia
majadiliano wakati wa Mkutano wa Ngazi ya Juu wa Majadiliano ya
Kimkakati kati ya Serikali na Washirika wa Maendeleo, uliofanyika katika
Ukumbi wa Mikutano wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Jijini Dar es
Salaam.
(Picha na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini-WFM-Dar es Salaam
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...