Na Munir Shemweta, WANMM MOROGORO

Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula ameitaka Bodi ya Chuo cha Ardhi Morogoro (ARIMO) kuwa wabunifu wa vyanzo vya mapato na kuweka msukumo kuhakikisha chuo hicho kinafanikiwa katika kutekeleza majukumu yake kisheria.

Aidha, ameitaka Bodi ya Chuo cha ARIMO kuhakikisha inapata taarifa kuhusiana na fedha za mkopo wa riba nafuu iliyopatiwa kwa ajili ya kazi za urasimishaji makazi holela ili mkopo huo uweze kurudishwa kwa wakati.

Dkt Mabula amesema hayo tarehe 16 Februari 2023 wakati akizindua Bodi mpya ya Chuo cha Ardhi Morogoro (ARIMO) iliyofanyika chuoni hapo.

Bodi mpya ya Chuo cha Ardhi Morogoro inaongozwa na Balozi Job Masima na imeanza kazi yake tarehe 1 Februari 2023 hadi tarehe 31 Januari 2026.

Kwa mujibu wa Dkt Mabula, katika mwaka wa fedha 2020/2021 na 2022/2023 wizara ya Ardhi ilikipatia chuo mkopo usio na riba wa shilingi bilioni 1.273 zilizotumika katika utekelezaji wa mradi wa urasimishaji makazi katika mji wa Mbalizi halmashauri ya wilaya ya Mbeya.

Amesema Wizara yake imekuwa ikikisaidia Chuo katika masuala mbalimbali kama vile kukipatia msaada wa vifaa vya kisasa vya upimaji kwa ajili ya kufundisha na kutekeleza miradi mbalimbali.

‘’Wizara itaendelea kukisaidia Chuo cha ARIMO katika kuboresha miundombinu kupitia mradi wa uboreshaji usalama wa milki za ardhi, kupitia mradi huu ni vizuri ukatumika kama fursa ya wanafunzi kujifunza kwa vitendo’’. Alisema Dkt Mabula

Aliukumbusha uongozi wa Chuo cha ARIMO katika kuwatumia wanafunzi kwenye miradi ya kupanga na kupima ambapo alisema pamoja na utaratibu huo kuwa mzuri kutokana na kuongeza umahiri kwa wanafunzi lakini utekelezaji wake unapaswa kuzingatia ratiba ya wanafunzi wakati wa kwenda uwandani.

‘’Chuo pamoja na kupata kazi kihakikishe kazi zitakazopatikana na zinazoendelea kufanyika kufanya kwa mujibu wa malengo na kutekeleza kwa wakati na weledi ili mradi wasiharibu ratiba ya chuo’’ alisema Dkt Mabula.

Aidha, Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi aliutaka uongozi wa Chuo cha Ardhi Morogoro kuchukua kazi katika maeneo ambayo itakuwa rahisi kwa chuo kusimamia bila kuvuruga ratiba za masomo.

Kwa upande wake Kaimu Makamu Mkuu wa Chuo cha Ardhi Morogoro Charles Saguda alieleza kuwa, Chuo chake kimeshiriki kikamilifu katika program ya urasimishaji makazi nchini ambapo kati ya mwaka 2016 na 2023 kimefanikiwa kutekeleza miradi ya urasimishaji katika mitaa 80 iliyopo mikoa saba ya Arusha, Dar es Salaam, Iringa, Kilimanjaro, Mbeya, Morogoro na Mtwara.

‘’katika mitaa tuliyotekeleza urasimishaji jumla ya viwanja 67646 (65%) vimeidhinishwa kati ya viwanja 103,972 vilivyopimwa na viwanja vilivyosalioa yaani 36,326 (35%) vina changamoto mbalimbali ambazo tunaendelea kuzishughulikia kwa kushirikiana na mamlaka za upangaji’’ alisema Saguda.

Aidha, alisema Chuo chake kimefanikiwa kufanya upimaji katika maeneo mapya jijini Dodoma na halmashauri ya wilaya ya Chamwino na kuongeza kuwa hivi karibuni chuo kimeingia mkataba na Shirika la Reli unaolenga kuweka miundombinu ya upimaji katika maeneo 26 ya reli kuandaa topografia, kupanga na kupima viwanja pamoja na kuweka alama za mipaka ya reli katika maeneo ya mradi.

Pamoja na mafanikio, Saguda alisema chuo kina changamoto za uhaba wa watumishi hasa wakufunzi, uhaba wa vifaa vya kufundishia pamoja na miundombinu.

Waziri Mabula alisema wizara yake itaendelea kuboresha mazingira ya chuo cha ardhi hatua kwa hatua kadri bajeti inavyoruhusu na kutoa rai kwa wajumbe wa Bodi mpya ya Chuo cha Ardhi Morogoro kuwa wabunifu katika kubuni vyanzo vya mapato.

Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimali watu wa Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Sheushi Mburi ambaye alimuwakilisha Katibu Mkuu wa Wizara hiyo alieleza kuwa Wizara ya Ardhi itashirikiana na chuo kutatua changamoto zote ikiwemo suala la watumishi na kuongeza kuwa, wakati mchakato wa kupata watumishi ukiendelea chuo kinapaswa kuainisha watumishi walio katika taasisi nyingine walio tayari kufundisha katika chuo hicho.


Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...