Na Mwandishi Wetu, Rukwa
WANANCHI wameombwa kujiunga na huduma za Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF), ili waweze kupata huduma za matibabu bila kikwazo chochote.
Rai hiyo imetolewa na Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya NHIF Juma Muhimbi wakati akifungua Mkutano wa wadau wa Mkoa wa Rukwa ambao ulilenga kujadili maboresho ya huduma za Mfuko pamoja na kupokea maoni ya wadau juu ya utendaji kazi wake.
Ameeleza kuwa Serikali ya Awamu ya Sita imefanya kazi kubwa katika uboreshaji wa huduma za matibabu ikiwemo ujenzi wa vituo vya kutolea huduma kila mahali hivyo akawaomba wananchi kutumia fursa ya kunufaika na huduma hizo kupitia NHIF.
“Serikali ya awamu ya sita chini ya uongozi mahiri wa Mama yetu Mhe. Samia Suluhu Hassan imefanya kazi kubwa mno katika Sekta ya Afya, huduma vituoni kwa sasa zinapatikana kwa urahisi mno kutokana na uwekezaji mkubwa uliofanywa kuanzia vifaa vya kisasa, dawa lakini pia uboreshaji wa miundombinu hivyo kazi iliyobaki ni wananchi kujiunga na Mfuko ili watumie hizo huduma bila kikwazo,” amesema Muhimbi.
Alisema kuwa maboresho hayo yamewezesha upatikanaji wa huduma za Kibingwa nchini ambazo awali Serikali ililazimika kulipia mabilioni ya fedha kupeleka wagonjwa nje ya nchi lakini kwa sasa huduma hizo zinapatikana nchini.
“Maendeleo haya ya kihuduma pia yamesababisha ongezeko la gharama za matibabu hivyo ili kila mmoja aweze kunufaika na huduma hizi bila kikwazo ni vyema sana wananchi tukajua umuhimu wa bima ya afya na kuchukua hatua za kujiunga ili tuepukane na kuingia kwenye umasikini wa kuuza mali zetu ili tupate fedha za kujitibia,” amesema Muhimbi.
Alizungumzia namna Mfuko ulivyojipanga kuwahudumia wanachama wake, amesema kuwa maboresho makubwa yamefanyika katika maeneo mbalimbali yakiwemo ya kusogeza huduma kwa wanachama, maboresho ya kihuduma kupitia kitita chake cha mafao pamoja na Mifumo ya TEHAMA inayosaidia katika uharakishaji wa huduma kwa wanachama vituoni na watoa huduma kwa upande wa uwasilishaji wa madai yao.
Akitoa taarifa ya Mkoa wa Rukwa, Meneja wa NHIF Dkt. Janeth Pinda amesema kuwa kwa sasa Mfuko umeboresha zaidi huduma zake ambapo huduma ya vitambulisho inapatikana ndani ya muda wa siku tatu tofauti na awali ambapo ilipatikana ndani ya siku 14.
“Tumeboresha sana huduma zetu na mfano mzuri ni eneo la vitambulisho na ulipaji wa madai kwa watoa huduma, kwa sasa madai tunalipa ndani ya siku 39 tangu madai hayo yawasilishwe hivyo nawaomba sana wadau wetu tuendelee kushirikiana ili huduma hizi ziwe rahisi zaidi,” amesema Dkt. Pinda.
Kwa upande wa wadau wakizungumza katika mkutano huo, wameupongeza Mfuko kwa namna unavyosikiliza Wadau wake na kuyafanyia kazi maoni yanayotolewa lakini pia namna ulivyoimarisha mahusiano na wadau wake hususan Watoa huduma na wanachama.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...