Na Benny Mwaipaja, London
WAZIRI wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba, amesema Tanzania amelishauri Shirika la Kimataifa la Uwekezaji la Uingereza (British International Investment- (BII), kuongeza kiwango cha uwekezaji nchini Tanzania ili kukuza biashara
Dkt. Nchemba ametoa wito huo Jijini London, nchini Uingereza, alipoongoza Ujumbe wa Tanzania uliokutana na Menejimenti ya Shirika hilo, ambalo limewekeza katika baadhi ya miradi nchini hapa.
Alisema Tanzania ina fursa nyingi za uwekezaji katika sekta mbalimbali ikiwemo nishati, kilimo, utalii, madini, viwanda na huduma pamoja na rasimali za asili kama vile gesi na maji kwa ajili ya kuzalishaji wa nishati, ardhi yenye rutuba kwa ajili ya kilimo, madini pamoja na hali ya amani nchini, ambavyo kiujumla vinaweka mazingira ya kuvutia kiuwekezaji.
Dkt. Nchemba ameialika timu ya wataalamu kutoka BII kuitembelee Tanzania na kufanya mazungumzo na taasisi na mashirika mbalimbali pamoja na sekta binafsi ili kuangalia maeneo ya kuwekeza kwa faida ya pande zote zinazohusika.
Naye Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Fedha na Mipango Zanzibar, Dkt. Juma Malik Akil, alisema kuwa Zanzibar, ikiwa sehemu ya Tanzania, inatekeleza program ya uchumi wa bluu inayohitaji uungwaji mkono wa Taasisi za fedha za Kimataifa na kuiomba Taasisi hiyo kushiriki katika ujenzi wa uchumi wa Zanzibar
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Uingereza la Uwekezaji (BII) Bw. Chris Chijiutomi, aliihakikishia Tanzania kwamba iko tayari kuongeza uwekezaji kwa kushirikiana na Sekta binafsi ikiwa ni sera ya Serikali ya Uingereza ya misingi ya kuanzishwa kwa Shirika hilo.
Alisema kuwa Shirika lake lina mtaji wa zaidi ya dola za kimarekani bilioni 11 lakini imewekeza Tanzania kiasi cha dola za kimarekani milioni 215 pekee hivyo kuitaka Tanzania kuainisha miradi ya kipaumbele ambayo shirika hilo litachambua na kutoa fedha kwa kushirikiana na sekta hiyo binafsi.

Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb), akimkabidhi Kamishna wa Biashara Kanda ya Afrika wa Serikali ya Uingereza, Mhe. John Humphley, jarida linaloonesha mafanikio ya miaka miwili madarakani ya Serikali ya Awamu ya Sita, ya Samia Suluhu Hassan, , walipokutana kwa mazungumzo ya kikazi katika Ofisi za Ubalozi wa Tanzania, jijini London, Uingereza.



Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb), akiwa na Kamishna wa Biashara Kanda ya Afrika wa Serikali ya Uingereza, Mhe. John Humphley, walipokutana kwa mazungumzo ya kikazi katika Ofisi za Ubalozi wa Tanzania, jijini London, Uingereza.(Picha na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini-Wizara ya Fedha na Mipango, London)
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...