NA MWANDISHI WETU, LUSHOTO

WAJUMBE wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ustawi na Maendeleo ya Jamii, wametembelea kiwanda cha kuchakata Chai Mponde kilichoko Wilaya ya Lushoto Mkoani Tanga Machi 16, 2023 ili kukagua utekelezaji wa miradi mitano inayotekelezwa na Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Ajira, Vijana na Wenye Ulemavu (OWM-KVAU) na taasisi zilizo chini yake.

Kiwanda cha Chai Mponde kinamilikiwa kwa ubia na Mifuko ya Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF) na Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF) taassi ambazo ziko chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Ajira, Vijana na Wenye Ulemavu (OWK-KVAU),  kila taasisi inamiliki asilimia 42% ya hisa na Msajili wa Hazina(TR) asilimia 16%.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Ajira, Vijana na Wenye Ulemavu, Mhe. Profesa Joyce Ndalichako, Naibu wake Mhe. Patrobas Katambi, Katibu Mkuu Profesa Jamal Katundu na Wakurugenzi Wakuu wa Taasisi hizo, CPA. Hosea Kashimba (PSSSF) na Dkt. John Mduma (WCF) pia walikuwepo wakati wa ziara hiyo.

Kiwanda cha Chai Mponde kilifanyiwa ukarabati mkubwa baada ya kusimama kufanya kazi kwa zaidi ya miaka 10 hali iliyosababisha mitambo na majengo kuchakaa sana.

Hali hiyo iliifanya Serikali kutafuta njia ya kukifufua kiwanda hicho ili kiweze kuwanufaisha wakulima wa Chai wa Halmashauri ya Bumbuli na wilaya ya Lushoto kwa ujumla wake, Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Profesa Joyce Ndalichako alisema.

Baada ya uwekezaji mkubwa uliofanyika kiwanda kimeanza kazi ambapo kilo 24,460 zimeuzwa na tani 50 zinategemewa kuuzwa mwishoni mwa mwezi Machi, 2023, Meneja wa kiwanda hicho, Sane Kwilabya alisema.

Wajumbe hao wa Kamati walitembezwa maeneo mbalimbali ya kiwanda kuanzia sehemu ya kupokelea majani ya chai kutoka kwa wakulima, sehemu ya kunyausha (Withering), jinsi majani ya chai yanavyochakatwa (Processing) na kupata aina mbalimbali za unga wa chai iliyochakatwa (grading) sehemu ya Boiler inayotumika kukaushia chai (Dryer), sehemu ya kuhifadhi magogo ya miti na sehemu inayotenganisha chai iliyochakatwa kulingana na madaraja mbalimbali (ukubwa wa chengachenga  za chai)

Aidha baada ya wajumbe kutembelea kiwanda na kupatiwa maelezo ya kina kuhusu uendeshaji wa kiwanda hicho, wameipongeza Serikali kwa uamuzi wake wa kuruhusu uwekezaji kwenye kiwanda hicho kwani kitanufaisha wakulima wa Chai wa Halmashauri ya Bumbuli na maeneo yanayozunguka wilaya nzima ya Lushoto na Korogwe.

“Kwa niaba ya Wajumbe wa Kamati nichukue fursa hii kuipongeza Serikali kwa kukubali uwekezaji huu, kwani unakwenda kuleta manufaa makubwa kwa wakulima wa chai.”Alisema Mhe. Fatma Tawfiq, Mwenyekiti wa Kamati ya kudumu ya Bunge ya Ustawi na Maendeleo ya Jamii.

Mheshimiwa Tawfiq pia alisema kamati yake itaweka msukumokwa mamlaka husika ili changamoto zinazokikabili kiwanda ziweze kupatiwa ufumbuzi na hivyo kuwepo na uendelevu wa utendaji kazi wa kiwanda bila ya vikwazo

Alisema Kamati imebeba ombi la kiwanda la kurejeshewa umiliki wa shamba la miti la Sakare ambalo hapo kabla ya kiwanda kusitisha shughuli zake, lilikuwa ndio tegemeo la uzalishaji wa miti inayotumika kama nishati ya kukaushia chai.

Aidha Makamu Mwenyekiti wa Kamati hiyo Mhe. Riziki Lulida licha ya kupongeza alishauri uongozi wa kiwanda kutoa ajira kwa makundi mbalimbali wakiwemo wenye ulemavu.

Akiongea kwa niaba ya wawekezaji Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF), Dkt. John Mduma alisema, kusudio kubwa la kukifufua kiwanda ni kuwawezesha wananchi wa Lushoto, Bumbuli Korogwe na maeneo jirani kupata kipato na hivyo kuwainua kiuchumi kwani wengi wanategemea zao hilo.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu), Mhe. Profesa Joyce Ndalichako (katikati) na Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ustawi na Maendeleo ya Jamii, Mhe. Fatma Tawfiq (mwenye miwani katikati) wakielezwa jinsi chai inavyochakatwa wakati wajumbe wa Kamati walipotembelea kiwanda cha Chai Mponde kilichoko Lushoto Mkoani Tanga Machi 16, 2023.
Meneja wa Kiwanda cha Chai Mponde, Bi.Sane Kwilabya (kulia) akiwapa maelezo wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ustawi na Maendeleo ya Jamii kuhusu aina mbalimbali ya chai iliyochakatwa wakati wa ziara ya Kamati kwenye kiwanda hicho Machi 16, 2023.
Meneja wa Kiwanda cha Chai Mponde, Bi.Sane Kwilabya (kulia) akiwapa maelezo wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ustawi na Maendeleo ya Jamii kuhusu kazi ya kuchakata chai inavyoendeswha wakati wa ziara ya Kamati kwenye kiwanda hicho Machi 16, 2023. Wakwanza kushoto ni Mkurugenzi Mkuu wa PSSSF, CPA. Hosea Kashimba.

Mkurugenzi Mkuu wa WCF, Dkt. John Mduma akizunguzma mbele ya wajumbe.
Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ustawi na Maendeleo ya Jamii, Mhe. Fatma Tawfiq (wapili kulia) na baadhi ya wajumbe w aKamati hiyo, wakiangalia chai ambayo tayari imechakatwa. Kushoto ni Meneja wa kiwanda cha Chai Mponde Bi. Sane Kwilabya.
Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ustawi na Maendeleo ya Jamii, Mhe. Fatma Tawfiq, akionja chai ili kupata ladha halisi ya chai inayozalishwa kiwanda cha Chai Mponde
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Ajira, Vijana na Wenye Ulemavu, Mhe. Profesa Joyce Ndalichako (watano-Kulia) na Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ustawi na Maendeleo ya Jamii, Mhe. Fatma Tawfiq (nyuma ya waziri Ndalichako) pamoja na baadhi ya wajumbe wa kamati, wakipatiwa maelezo ya jinsi chai inavyochakatwa.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Ajira, Vijana na Wenye Ulemavu, Mhe. Profesa Joyce Ndalichako 9watatu kulia) na Naibu wake, Mhe. Patrobas Katambi (wakwanza kulia) wakiwaongoza wajumbe wa Kamati wakati wa ziara hiyo.





Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...