Tanzania itakuwa mwenyeji wa mkutano mkubwa wa Afrika wa masuala ya chakula na kilimo utakaofanyika Septemba 5 mpaka 8 mwaka huu.

Ijumaa wiki hii (Machi 17), Rais Samia Suluhu Hassan atazindua maandalizi ya mkutano huo Ikulu, Dar es Salaam, hii ni kwa mujibu wa Mkurugenzi wa Mawasiliano wa Ikulu, Zuhura Yunus.

Mkutano wa Afrika wa chakula wa Septemba unatarajiwa kuhudhuriwa na watu takribani 3,000 kutoka sehemu mbalimbali barani Afrika na duniani, ikiwemo marais, mawaziri na wakuu wa taasisi za kimataifa.

Mkutano huo utaweka msisitizo kwenye Vijana na Wanawake kama Msingi wa Mfumo Endelevu wa Chakula.

Tanzania imechaguliwa kuwa mwenyeji wa mkutano huo kutokana na hatua kubwa za kimageuzi ambazo serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan imezichukua tangu alipoingia madarakani miaka miwili iliyopita.

Hatua hizo ni pamoja na kuongeza bajeti ya Wizara ya Kilimo kwa mara nne kwa mwaka wa fedha 2022/2023, jambo ambalo halijawahi kutokea tangu tupate uhuru.
Serikali ya Rais Samia pia imetambuliwa kwa mradi wake wa ubunifu wa Jenga Kesho Iliyo Bora (BBT), ambao unalenga kuwawezesha vijana, ambao ndiyo nguvu kazi kubwa nchini, kuingia katika kilimo.

Serikali yake pia imewekeza kwenye miundombinu ya umwagiliaji, huduma za ugani, pembejeo na ruzuku ya mbolea na mbegu kwa viwango ambavyo havijawahi kufanyika miaka ya nyuma.

Serikali ya Rais Samia pia imekuwa ikitekeleza mpango wa kilimo unaojulikana kama Ajenda 10/30 yenye lengo la kufanya kilimo kiwe cha biashara na kikue kwa wastani wa asilimia 10 kwa mwaka ifikapo 2030.





Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...